Kwa ufupi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana wakati wa mjadala wa pamoja kuhusu
mchango wa kampuni za kati na ndogo katika kufikia nchi ya viwanda na
ushirikishaji wa wazawa.
Dar es Salaam. Serikali imesema haitakubali kuona bidhaa
kutoka Tanzania zinazuiliwa kuingia katika nchi yoyote ya Afrika Mashariki kwa
sababu Mkataba wa Soko la Pamoja wa nchi hizo (EAC) unaruhusu kufanya biashara
katika ukanda huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda alisema hayo jana wakati wa mjadala
wa pamoja kuhusu mchango wa kampuni za kati na ndogo katika kufikia nchi ya
viwanda na ushirikishaji wa wazawa.
Kabla ya mjadala huo, utafiti wa
kampuni 100 za kati Tanzania uliwasilishwa kwa wadau na kubainisha changamoto
mbalimbali ambazo kampuni hizo zinapitia katika ufanyaji wa biashara zao.
Shindano la kampuni 100 za kati
limeandaliwa na Kampuni ya KPMG kwa ushirikiano na Mwananchi Communications Ltd
(MCL) kupitia gazeti lake la The Citizen na tuzo zinatarajiwa kutolewa leo.
Utafiti uliofanywa na kampuni ya
Research Solutions Africa umebaini kwamba theluthi mbili ya kampuni 4,000
zilizoshindanishwa zilionyesha nia ya kupanua biashara zao mpaka nchi nyingine
za Afrika Mashariki.
Hata hivyo, zililalamikia upungufu
wa mitaji ya kuziwezesha kupanua biashara zao. Pia, zimelalamikia utitiri wa
kodi, jambo ambalo zilisema linaathiri mitaji yao na ufanyaji wa biashara
nchini.
Profesa Mkenda aliwahakikishia
wafanyabiashara hao kwamba Serikali imechukua hatua kumaliza sintofahamu ya
kuzuiliwa kwa bidhaa za Tanzania zinazoingia Kenya na kusisitiza kwamba suala
hilo likijirudia, itachukua hatua mara moja.
“Juhudi za viongozi wetu
zimefanikisha kumaliza mgogoro ule, sitarajii kama utajirudia tena. Bidhaa za
Tanzania zikizuiliwa tena tutachukua hatua, wanajua moto wetu. Kwa hiyo,
wafanyabiashara wasisite kupeleka bidhaa zao nchi yoyote,” alisema Profesa
Mkenda.
Kuhusu ujasiriamali, Profesa
Mkenda alisema ni vyema vijana wakachukua jukumu hilo badala ya kuwaachia wazee
ambao wakistaafu ndiyo wanakwenda kuanza ujasiriamali. Alisema hao hawawezi
kufanya vizuri kama wale ambao wanaanza ujasiriamali wakiwa bado wadogo.
“Ni dhana potofu kufikiri kwamba
ujasiriamali unatakiwa kufanywa baada ya kustaafu. Wafanyabiashara wakubwa
waliofanikiwa walianza wakiwa bado vijana wadogo, wakawekeza muda wao kwenye
biashara, ndiyo hao tunawaona sasa wakiwa na mafanikio makubwa,” alisema.
Mkurugenzi wa Resource Solutions
Africa, Dk Jasper Grosskurth alisema asilimia 51 ya kampuni zilionyesha nia ya
kupanua biashara kwenda Kenya wakati asilimia 38 zikitaka kwenda Uganda.
Hata hivyo, Dk Grosskurth
alizitaka kampuni hizo kuwa na rekodi nzuri ya ulipaji wa kodi kwa sababu hiyo
ni moja ya njia ya kujiongezea thamani na kuiwezesha kuhimili soko la
ushindani.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa
kampuni ya Tigo, Simon Karikari alisema maendeleo ya viwanda yanakwenda
sambamba na ukuaji wa teknolojia. Alisisitiza kwamba wao wakiwa ni wadau wa
mawasiliano ya simu, wametoa fursa ya kurahisisha miamala kwa wajasiriamali.
Alisema wanawaunganisha
wajasiriamali wakati wa kusambaza huduma zao kwa walaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL,
Francis Nanai alisisitiza juu ya umuhimu wa sekta ya kilimo kwenye dhana nzima
ya uanzishwaji wa viwanda akisema haviwezi kustawi kama kilimo kipo chini.
“Kutokana na umuhimu wa kilimo,
ningependa kuona kauli mbiu yetu inaitwa ‘Tanzania ya kilimo na viwanda’ ili
tusikiache kilimo nyuma wakati tunaelekea kwenye nchi ya viwanda,” alisema
Nanai.
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na
Uwekezaji wa Shirika la Viwanda Vidogovidogo (Sido), Titus Kyaruzi alisema ni
muhimu kuwajengea uwezo vijana ili washiriki kwenye ujasiriamali.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment