Kwa ufupi
Acacia, kampuni tanzu ya Barrick na inayomiliki migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi, imezuiwa tangu mwezi Machi kusafirisha mchanga huo wa
madini kwenda kuuyeyusha nje ya nchi kwa ajili ya kupata mabaki ya dhahabu,
shaba, fedha na madini mengine yaliyoshindikana kuchenjuliwa migodini.
Dar es Salaam. Licha ya kupata hasara kwenye robo ya tatu ya
mwaka, kampuni ya Barrick imetenga dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh660
bilioni) kuilipa Serikali, lakini imeweka sharti; inataka iruhusiwe kusafirisha
makinikia.
Acacia, kampuni tanzu ya Barrick na inayomiliki migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi, imezuiwa tangu mwezi Machi kusafirisha mchanga huo wa
madini kwenda kuuyeyusha nje ya nchi kwa ajili ya kupata mabaki ya dhahabu,
shaba, fedha na madini mengine yaliyoshindikana kuchenjuliwa migodini.
Baada ya majadiliano baina ya Serikali na Barrick, kampuni
hiyo ya Canada ilikubali kulipa dola 300 milioni “kuonyesha uaminifu”.
Taarifa ya miezi mitatu ya Barrick (Julai-Septemba)
iliyotolewa juzi, inaonyesha kuwa ilipata hasara ya dola 11 milioni (zaidi ya
Sh24 bilioni) tofauti na faida ya dola 175 milioni (zaidi ya Sh385 bilioni)
iliyopata katika kipindi kama hicho mwaka jana (dola moja ya Kimarekani ni sawa
na takriban Sh2,200 za Tanzania).
“Kupungua kwa mapato kunatokana na kushuka kwa uzalishaji na
bei ya dhahabu pamoja na zuio la kusafirisha makinikia ambalo Serikali ya
Tanzania iliiwekea Acacia,” inasema ripoti hiyo.
Vilevile, Barrick inasema kupungua kwa mapato yake
kumechangiwa na ongezeko la makadirio ya kodi yanayofika dola 172 milioni
(zaidi ya Sh378 bilioni) zilizopendekezwa kwenye majadiliano ya mustakabali wa
operesheni za Acacia nchini.
Wakati Barrick ikitenga kiasi hicho cha kodi, Acacia ina
dola 128 milioni (zaidi ya Sh282 bilioni) na kufanya jumla ya dola 300 milioni
zilizokubaliwa kwenye mazungumzo yaliyofanyika kwa miezi mitatu iliyopita.
Masharti hayo si ya kwanza, itakumbukwa kwamba siku chache
baada ya mkutano wa kukabidhi ripoti ya majadiliano hayo, kampuni ya Acacia
ilisema haiwezi kulipa Dola 300 milioni kwa mkupuo na kwamba Barrick inajua
hilo.
Ofisa fedha mkuu wa Acacia, Andrew Wray alinukuliwa na
vyombo vya habari akisema: “Hatuna huo uwezo kuilipa Tanzania ili tumalizane
kwenye mgogoro wa kodi uliopo.”
Wray alisema hayo Oktoba 20 wakati Acacia ilipokuwa
ikiwasilisha ripoti yake ya fedha kwa robo ya tatu ya mwaka iliyoishia
Septemba, ikionyesha kushuka kwa mapato na faida ikilinganishwa na kipindi kama
hicho mwaka jana.
Barrick imeiunga mkono Acacia kwenye msimamo wake kuhusu
malipo hayo ya dola 300 milioni ikisema: “Kutokana na hali ya Acacia kifedha,
malipo haya yanapaswa kufanywa kwa awamu yakitegemea mauzo ya dhahabu na
usafirishaji wa makinikia.”
Katika robo hiyo ya tatu, faida ya Acacia imeshuka kwa
asilimia 70 kutoka dola 52.878 milioni (zaidi ya Sh116.331 bilioni) mpaka dola
16.038 (zaidi ya Sh35.283 bilioni).
Wakati wa mkutano na vyombo vya habari uliofanyika Ikulu,
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alikuwa
mwenyekiti wa wawakilishi wa Serikali alisema Barrick wamekubali kutekeleza
masharti yote ya sheria mpya ya madini.
Lakini kwenye taarifa yake, kampuni hiyo inasema itaendelea
kuzungumza na Serikali ili kuondoa zuio la kusafirisha makinikia na kwamba
mazungumzo hayo yataenda sambamba na kutafuta suluhu ya deni la kodi la kiasi
cha dola 190 bilioni (zaidi ya Sh424 trilioni) ambazo Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imeitoza Acacia ikiwa ni malimbikizo ya kodi, faini na riba.
“Tunatarajia mazungumzo haya yatakamilika ndani ya nusu ya
kwanza ya mwaka ujao,” inasema Barrick.
Pamoja na hasara hiyo ya robo ya tatu, kwa miezi yote tisa,
Barrick imepata faida ya dola 1.752 bilioni (zaidi ya Sh3.854 trilioni) ambayo
ni zaidi ya mara saba ikilinganishwa na iliyopata kwa muda kama huo mwaka jana.
Mwaka uliopita, ilitangaza faida ya dola 230 milioni (zaidi ya Sh506 bilioni).
Mbali na taarifa hiyo ya fedha, Barrick imefafanua kwa wadau
wake kuhusu makubaliano yaliyoafikiwa kwenye majadiliano ya miezi mitatu baina
yake na Serikali.
Makubaliano
Kwenye ripoti hiyo, Barrick inasema imekubaliana na Serikali
kuhusu mfumo mpya wa uendeshaji ambao, endapo utaridhiwa, utatoa mwelekeo mpya
wa shughuli za Acacia nchini.
Barrack imefanya mazungumzo hayo kwa niaba ya Acacia kwa kuwa ndiye mmiliki mkuu wa hisa, ikimiliki asilimia 63.9.
Barrack imefanya mazungumzo hayo kwa niaba ya Acacia kwa kuwa ndiye mmiliki mkuu wa hisa, ikimiliki asilimia 63.9.
Lakini, pamoja na ukweli huo, inasema chochote
kitakachoafikiwa kitapaswa kutathminiwa na kuthibitishwa na Acacia kabla ya
utekelezaji, ingawa Barrick inaamini makubaliano yaliyofikiwa yataleta suluhu
ya mgogoro uliopo kwenye uchimbaji wa dhahabu nchini.
Mgogoro kati ya kampuni ya Acacia, mchimbaji na msafirishaji
mkubwa wa dhahabu ya Tanzania, na Serikali ulishika kasi Machi baada ya kampuni
hiyo kuzuiwa kusafirisha mchanga wa madini.
Baadaye Rais John Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza
kiwango cha madini kilichokuwa katika makontena 270 yaliyokuwa Bandari ya Dar
es Salaam, athari za kuusafirisha kwenda nje, sheria na mikataba.
Kamati hizo zilisema zimebaini kiwango cha dhahabu ni mara
kumi ya kile kilichotangazwa na Acacia, kukwepa kodi na kukiuka sheria, huku
mikataba ikionekana kunufaisha wawekezaji.
Ripoti hizo zilisababisha mawaziri kuwajibishwa na baadaye
Serikali na Barrick kukubaliana kuunda timu za majadiliano, ambayo yalijikita
katika muundo na mfumo mpya wa uendeshaji wa kampuni tanzu za Barrick,
kubadilisha uendeshaji wa biashara ya madini na kuwanufaisha zaidi wananchi
wanaoizunguka migodi.
Mengine ni kubadilisha mikataba ya madini (MDA) ili iendane
na sheria mpya kwa lengo la kuongeza ushiriki na mapato ya Serikali, pamoja na
kuainisha fidia ya makosa ya Acacia. Makubaliano manne yalipata muafaka na la
mwisho bado linajadiliwa.
“Kwa makubaliano haya tunaamini tutapata suluhu ya kudumu na
operesheni za Acacia nchini Tanzania zitaendelea kama kawaida,” inasema taarifa
hiyo.
Mgawanyo wa mapato
Alipokuwa akiwasilisha ripoti ya majadiliano hayo kwa Rais
Magufuli, Profesa Kabudi alisema Barrick wamekubali kutekeleza masharti yote ya
sheria mpya za madini.
Alisema kuanzia sasa mapato au faida itagawanywa sawa kati
ya Acacia na Serikali.
Siku ya pili alitoa ufafanuzi zaidi ikisema: “Mgawanyo wa
asilimia 50 kwa 50 wa faida ni baada ya tozo na kodi nyingine zote kulipwa. Kwa
ujumla, Tanzania itapata asilimia 70 na Barrick asilimia 30. Kwingineko
wanagawana asilimia 50 kwa 50 zikiwamo kodi, sisi tulikataa hilo.”
Lakini Barrick ikasema: “Mgao wa asilimia 50 za Serikali
utahusisha mrabaha, kodi na asilimia 16 ya hisa itakazopewa kukidhi matakwa ya
sheria mpya za madini.”
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment