Sehemu ya Nyumba hizo za Ghorofa za Shirika la Nyumba la Taifa NHC katika eneo la Raha Leo mkoani Mtwara. |
Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Waheshimiwa Mawaziri mliohudhuria hafla hii (Angalia Mawaziri waliopo)
Mheshimiwa Halima Omari Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Mheshimiwa Atashasta Nditiye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira,
Ndugu Balandina Salome Joseph Nyoni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa,
Mheshimiwa Gavana wa benki Kuu ya Tanzania na Uongozi wote wa Benki Kuu uliopo hapa
Waheshimiwa Makatibu Wakuu Mliohudhuria hafla hii
Waheshimiwa Wabunge mliopo hapa,
Ndugu Evod Mmanda, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
Wajumbe wa Menejimenti ya Shirika,
Ndugu Viongozi mbalimbali mliopo hapa,
Waandishi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Mheshimiwa Rais, naomba nianze kwa kukukaribisha wewe na ujumbe wako kwenye mradi huu wa ujenzi wa nyumba za makazi uliotekelezwa na Shirika hapa Rahaleo Mkoani Mtwara. Karibuni sana.
Pili, Mheshimiwa Rais, naomba nitumie fursa hii pia kuwakaribisha wananchi na wageni wote waliokuja kujumuika nawe kwenye shughuli hii ya leo. Wote nasema karibuni sana.
Mheshimiwa Rais, kwa niaba ya Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Shirika, naomba nikushukuru sana kwa kukubali kutenga muda wako adimu na kuja kutufungulia rasmi mradi huu wa nyumba za makazi na biashara. Kipekee nakupongeza kwa dhati kwa kazi na mageuzi makubwa ya Serikali yako ya Awamu ya Tano ambayo umeyafanya na kuleta dira sahihi ya maendeleo ya Tanzania tunayoitaka. Ni ukweli usiopingika na kila mpenda maendeleo kuwa katika kipindi kifupi cha uongozi wako kwa Taifa letu, umeweza kusukuma mbele suala la uwajibikaji, utawala bora na kuhimiza matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa. Hivyo, kwa niaba ya Bodi na Menejimenti ya Shirika tunakuhakikishia kuwa tupo bega kwa bega na Serikali yako ili tuweze kufikia matarajiyo ya watanzania hususan katika kuwapa makazi bora. Kadhalika, natoa shukrani za dhati kwako kwa kuipa sekta ya nyumba kipaumbele kikubwa tangu ulipokuwa Waziri mwenye dhamana na sekta hii. Tunakumbuka juhudi zako ulizofanya ambazo zilifanikisha kuwa na sheria za hati pacha na mikopo ya nyumba ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya sekta ya nyumba. Aidha, kama unakumbuka wewe ndiye uliyekuwa chachu ya kulifanya Shirika hili kuwa na sura ya kitaifa kwa kuhimiza ujenzi wa nyumba katika mikoa mbalimbali nchini badala ya kujikita tu Dar es Salaam. Kwa ujumla uongozi wako katika Wizara na Shirika ulichagiza vilivyo kulibadilisha Shirika hili kuwa na utendaji wenye tija zaidi kwa kuhimiza uchapakazi na uadilifu mkubwa. Kutokana na maelekezo yako uliyoyatoa wakati wa Uongozi wako, hivi leo hakuna wapangaji hewa katika nyumba zetu maana ulishasimamia uhakiki wa wapangaji na nyumba wanazopanga. Ulibadilisha mtizamo wa wapangaji wa Shirika kwa kuwahimiza kulipa kodi kwa wakati ili isaidie watanzania waliyo wengi. Ndiyo maana sote katika Shirika tunauona ujio wako hapa ukitukumbusha alama imara uliyotuachia ya uchapakazi, umakini na uadilifu katika utendaji wetu wa kazi.
Mheshimiwa Rais, nimeamua kuyasema haya kwa dhati kabisa ili kukushukuru na kukutanabaisha kuwa sisi katika Shirika tutaukumbuka daima mchango wako mkubwa uliyotupatia katika sekta ya nyumba. Kuja kwako hapa hii leo umetupatia heshima kubwa sisi uliotupa dhamana ya kusimamia sekta ya nyumba hapa nchini. Tunakushukuru sana kwa nia njema ambayo umekuwa ukituonyesha, ambayo kwa hakika imetutia moyo na shime kubwa ya kuendelea kuchapa kazi kwa bidii kwa manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Rais, waswahili husema ukikutana na jumbe sema yote. Napenda kuchukua nafasi hii kukupa kwa muhtasari maendeleo ya sekta ya nyumba. Mpango wa ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu, kati na juu ulibuniwa na Shirika katika mpango mkakati wake wa miaka mitano 2010/11- 2014/15, kwa lengo la kupunguza uhaba wa nyumba nchini unaokadiriwa kufikia nyumba milioni 3 hivi sasa. Katika mpango huu ambao umehuishwa mwaka jana kwa kuwa na mpango mwingine wa miaka kumi(2015/16-2024/25) , tumejikita katika kujenga nyumba za watu wa kipato cha kati na chini katika Halmashauri za Miji na Wilaya. Tunafanya hivyo tukitambua kuwa nyumba humpa binadamu utu wake, humpa furaha ya maisha na huleta amani, kwani mtu mwenye makazi yake huthamini uwepo wa amani ya nchi yake. Hii inarejesha dhamira njema aliyokuwa nayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kulianzisha Shirika hili mwaka 1962, ili liwezeshe watu wa kipato cha chini na kati kuwa na nyumba bora. Napenda kukuhakikishia kuwa ni azma ya Shirika kuona kuwa linafuata nyayo alizoacha Mwalimu Nyerere ili kupunguza uhaba wa nyumba katika maeneo ya Miji na Wilaya. Aidha, katika kufanya hivyo tunatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya mwaka 2015 ambayo inatuelekeza kujenga nyumba elfu kumi(10,000) katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Nikuhakikishie kuwa nia tunayo, uwezo tunao na sababu ya kutekeleza jukumu hilo tunayo, nayo ni kuboresha maisha ya watanzania hususan wa kipato cha chini. Kwa sasa nyumba yetu ya gharama ya chini ni shilingi milioni 30 na tumejipanga kufanya ubunifu zaidi wa kihandisi ili kupunguza gharama hiyo angalau ifikie milioni 20 hadi 25 bila kuathiri ubora wa nyumba zetu. Katika kutekeleza ujenzi huo, Mji Mkuu wa Dodoma utakuwa ni kipaumbele chetu ili kuisaidia watumishi wa serikali kupata makazi bora. Tumeshaanza kujenga nyumba katika eneo la Iyumbu mjini Dodoma ambapo awamu ya kwanza itakayokamilika katika muda mfupi ujao itakuwa na nyumba mia tatu(300). Aidha, ili kuwezesha ujenzi wa nyumba nyingi za gharama nafuu na kuwanufaisha wananchi wengi wa kipato cha chini, naleta ombi kwako kuwa Shirika la Nyumba na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) tupewe mtaji wa bilioni 100 kila mwaka za kuwezesha lengo hilo. Hii itasaidia kuwa na ushindani wa kitaasisi na uwajibikaji huku ikipunguza gharama za nyumba kwa kuwa fedha hiyo haitakuwa na riba. Fedha hizi zitakuwa zikirejeshwa serikalini baada ya kuuza nyumba kwa wananchi.
Mheshimiwa Rais, ili nyumba zetu na za wajenzi wengine ziendelee kuwa nafuu ni muhimu wadau wanaohusika washiriki kuweka miundombinu katika maeneo ya ujenzi, kuwepo na sera rafiki za taasisi za fedha(fiscal policy review), kupungua kwa riba ya mikopo ya benki ili kuwezesha wakopaji wengi kunufaika na kuwa na ardhi nafuu ya kujenga nyumba za watu wa kipato cha chini. Tuna imani kuwa serikali yako makini na mahiri itaweza kusimamia, kuelekeza na kuhimiza ipasavyo mabadiliko ya changamoto hizo ili kuleta unafuu mkubwa katika sekta ya nyumba.
Mheshimiwa Rais, ujenzi wa nyumba huhitaji fedha nyingi ambazo mara nyingi duniani kote hupatikana kupitia mikopo ya benki. Katika ujenzi wa nyumba tunaoufanya tulianza kujenga nyumba nyingi za watu wenye kipato cha juu ili faida inayopatikana iweze kutumika kujenga nyumba za gharama ya kati na chini zitakazowezesha wananchi wa kipato kidogo kuweza kumudu kuzinunua. Aidha, tukijuwa kuwa wananchi wetu wana uwezo mdogo wa kununua nyumba, tumeweza kuzishawishi benki na taasisi za fedha zipatazo 16 kutoa mikopo kwa wanunuzi na hata wajenzi wa nyumba hapa nchini, utaratibu ambao huko nyuma haukuungwa mkono na benki nyingi. Hata hivyo, pamoja na benki na taasisi za fedha kuwa tayari kutupatia mikopo bila dhamana ya serikali, kwa ajili ya kutuongezea kasi kubwa ya ujenzi wa nyumba nchini, kumekuwa na ukiritimba mkubwa wa kupata vibali vya kukopa. Hali hii licha ya kuzorotesha kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati, inaweza kuongeza gharama kwa kudaiwa na wakandarasi tutakaoshindwa kuwalipa kwa wakati.
Mheshimiwa Rais, sekta ya nyumba ina manufaa makubwa sana katika ukuaji wa uchumi maana ni sekta mtambuka inayochochea ukuaji wa sekta zingine, hutoa ajira kubwa sana, huwezesha serikali kupata kodi kubwa, huharakisha ukuaji wa sekta ya fedha na inao uwezo mkubwa wa kusukuma mbele sekta ya viwanda ambayo ndiyo kipaumbele cha serikali yetu ya Awamu ya Tano. Kuwepo kwa kasi kubwa ya ujenzi wa nyumba hakika ndiko kulikochochea kuanzishwa kwa viwanda vingi vya saruji ikiwemo Tanga Cement, Dangote Cement Industry na Twiga Cement ambaavyo navyo vinatoa ajira kubwa. Ni kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta ya nyumba Mheshimiwa Rais, siku zote tumekuwa tukililia sekta hii itambuliwe kama moja ya sekta za mkakati katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano ambao mhimili wake mkubwa unajengwa na uchumi wa viwanda.
Hata hivyo, Mheshimiwa Rais, pamoja na umuhimu mkubwa wa sekta ya nyumba, katika Mpango wa sasa wa Taifa wa Maendeleo, sekta ya nyumba haijabainishwa kabisa katika mpango huo. Tupo tayari tukiongozwa na Bodi ya Wakurugenzi kuleta mawazo Serikalini ili kuona namna bora ya kuingiza sekta ya nyumba katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo ili kusukuma mbele maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi yetu. Kwa kuanzia natoa ombi kwako kuwa mradi wa nyumba wa Kitovu cha mji wa Kawe utambuliwe kuwa moja ya vipaumbele vya miradi ya kimkakati ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa kuwa mradi huu ni mkubwa na wenye manufaa makubwa ya nchi.
Mheshimiwa Rais, kabla ya kumalizia maelezo yangu ni vema nikakupa maelezo mafupi ya mradi huu unaoufungua rasmi leo. Nyumba za mradi huu wa Rahaleo zilianza kujengwa rasmi Juni 29, 2015 na unakamilika mwezi huu Machi, 2017. Mradi huu una majengo matatu ya ghorofa. Kati ya majengo haya matatu, mawili yenye ghorofa sita kila moja yana nyumba 40 za makazi zilizouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania, ambazo zina uwezo wa kukaliwa na watu 240. Jengo la biashara lenye ghorofa nne litatumika kwa ajili ya Ofisi mbalimbali na shughuli za kibiashara. Hadi kukamilika, mradi huu umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 12 ikiwa ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani(VAT) iliyogharimu shilingi 1.9 bilioni. Huduma nyingine zitakazokuwepo kwenye mradi huu ni pamoja na matanki makubwa ya kuhifadhia maji ya wakazi watakaoishi hapa, kiwanja cha michezo na maegesho ya kutosha ya magari.
Mheshimiwa Rais, kama ilivyo miradi mingine, mradi huu wa Rahaleo umetengeneza ajira za moja kwa moja 2,711 na ajira shirikishi 1,356 na kuwanufaisha wananchi wa Mtwara wakiwemo wafanyabiashara.
Mheshimiwa Rais, kutokana na mahitaji makubwa ya nyumba hapa Mtwara na kupanuka kwa fursa za kiuchumi katika Mkoa huu, Shirika limewekeza ujenzi mwingine wa nyumba za makazi 30 katika eneo la Shangani Manispaa ya Mtwara. Mradi huo wa nyumba za kisasa nao umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.8 na umekamilika. Kadhalika, tunakamilisha ujenzi wa nyumba 54 za gharama nafuu katika Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa gharama ya shilingi bilioni 2.4.
Mheshimiwa Rais, katika miradi hii Shirika linafanya shughuli mbalimbali ikiwemo uwekaji wa miundombinu ya maji, umeme na barabara, kazi ambazo zingepaswa kufanywa na Mamlaka husika. Kwa mfano katika mradi huu wa Rahaleo unaoufungua rasmi hii leo, Shirika limelazimika kutumia shilingi milioni 755.9 kugharamia uletaji wa miundombinu ya umeme na maji. Aidha, katika mradi wa Shangani wenye nyumba 30 zenye makazi ya watu 180, miundombinu yake ya umeme na maji imegharimu shilingi milioni 161.5. Ni imani yetu kuwa wakati tunawekeza nguvu kubwa kuendeleza makazi ya watanzania hususan katika maeneo muhimu kama ukanda wa Mtwara, tunaziomba Mamlaka husika zitii agizo la Mtangulizi wako alilolitoa tarehe 1 Septemba, 2014 alipokuwa ukifungua nyumba za makazi huko Medeli- Dodoma na kuzitaka Mamlaka hizo kutimiza wajibu wao ili kupunguza gharama za nyumba kwa watanzania. Sisi tunaunga mkono agizo hilo na tunafarijika kuwa sasa wewe unaweza kulipa msukumo mpya. Ni ukweli uliyo wazi kuwa mamlaka hizo ndizo zinazonufaika na uwekezaji wa huduma hizo. Taasisi hizo zikifanya jukumu lao hilo itapunguza gharama za nyumba tunazojenga.
Mheshimiwa Rais, nisingependa kuchukua muda mwingi kwa hotuba ndefu. Yapo mambo mengi ambayo kila tunapokuomba utusaidie umekuwa ukiyapa kipaumbele. Tuna imani kuwa wadau mbalimbali zikiwemo Halmashauri za Miji na Wilaya zitaendelea kutuunga mkono ili juhudi za kuwapatia watanzania makazi bora na nafuu ziweze kutimia. Sisi katika Shirika tutaendelea kutekeleza azma na falsafa yako kuwapatia wananchi wa kipato cha chini makazi bora kwa kuipa msukumo mkubwa sekta ya nyumba.
Mheshimiwa Rais, baada ya kusema hayo, sasa nimkaribishe Mwenyekiti wa Bodi ili amkaribishe Mheshimiwa Waziri akukaribishe rasmi uwasalimie wananchi na kutufungulia mradi wetu. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment