Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuwajulisha wafanyabiashara wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla kuwa wanaweza kutumia fursa za biashara zinazopatikana katika soko la nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuuza bidhaa zao ndani ya nchi wanachama yaani Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda pamoja na sisi wenyewe Tanzania.
Wafanyabiashara wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya Jumuiya ambayo yemebainishwa katika Mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu namba 5 ambapo Jumuiya ilianzisha Itifaki ya Umoja wa Forodha (The East African Community Customs Union).
Chini ya Itifaki hiyo wafanyabiashara wa Nchi Wanachama wana uhuru wa kufanyabiashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kutozwa ushuru wa forodha ilimradi bidhaa zao zimezingatia vigezo na kufuata utaratibu ulioainishwa katika Itifaki hii.
Japokuwa Sudan Kusini imeridhia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki bado fursa za kufanya biashara nchini humo hazijakamilika. Hii ni kwasababu nchi hiyo imejiunga na Jumuiya hivi karibuni na hadi hapo itakaporejesha ‘Instrument’ yaani zile hati za kujiunga na Jumuiya baada ya kufuata utaratibu wa nchi hiyo, ndipo itakuwa mwanachama kamili ambaye atafurahia matunda haya tunayoyaongelea hapa. Yaani, Sudani Kusini itaingia kwenye utaratibu wa utekelezaji wa Itifaki na makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa katika Jumuiya.
Ili mfanyabiashara hasa mdogo aweze kufanya biashara katika Soko la Jumuiya hii anapaswa kufuata utaratibu ufuatao:
a. Mfanyabiashara/ Msafirishaji anatakiwa kufika kwenye kituo chochote cha forodha kilichopo mpakani akiwa na bidhaa yake anayotaka kuuza kwenye Soko la Jumuiya.
b. Akiwa Kituoni hapo, msafirishaji atatakiwa kupatiwa cheti cha Uasilia wa Bidhaa Kilichorahisishwa (Simplified Certificate of Origin) ambacho hutolewa bure na ofisi za Mamlaka ya Forodha Tanzania zilizopo mipakani.
c. Mfanyabiashara atatakiwa kujaza taarifa zinazotakiwa kwenye cheti hicho kama vile jina kamili la msafirishaji, anuani, nchi anayotoka, maelezo ya bidhaa na thamani ya bidhaa. Afisa forodha wa kituo husika atajaza maeneo yanayomhusu na kugonga muhuri katika cheti hicho.
d. Mfanyabiashara atatakiwa kuonesha cheti cha uasilia wa bidhaa wakati akiingia kwenye nchi mwanachama anapotaka kuuza bidhaa hiyo.
e. Cheti cha uasilia wa bidhaa ni kwa ajili ya mfanyabiashara mdogo mwenye bidhaa isiyozidi dola za Kimarekani 2000. Aidha, mfanyabiashara mdogo halazimiki kuwa na wakala wa Forodha.
f. Mfanyabiashara mdogo anatakiwa kufuata taratibu zinazohitajika na taasisi nyingine zinazohusika katika kuruhusu uingizaji / uagizaji wa bidhaa kama vile:
· Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA),
· Shirikia la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine.
Wizara inatoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla iwapo watakutana na vikwazo visivyo vya kiforodha wakiwa katika Nchi Wanachama, wawasilane na Wizara kupitia Mawasiliano yaliyoanishwa hapo juu.
Aidha, wafanyabiashara pia wanaweza kutoa taarifa za vikwazo wanavyokutana navyo kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika neno ‘NTB’ na kutuma kwenda namba 15539. Vilevile kwa madereva wa magari makubwa wanaosafirisha mizigo kwenda Nchi Wanachama utaratibu umewekwa ambapo madereva hao wanaweza kutoa taarifa za moja kwa moja kwa Jeshi la Polisi kupitia namba 0713631780iwapo watakutana na vikwazo visivyo vya Kiforodha vya barabarani. Kadhalika wafanyabiashara pia wanaweza kuwasilisha malalamiko yao juu ya Vikwazo visivyo vya Kiforodha kupitia tovuti ambayo ni www.tradebarriers.org
Wizara inahimiza wafanyabiashara kutumia njia halali za kuvusha bidhaa kwenye mipaka ya Nchi wanachama kwani njia zisizo halali (Njia za panya) hupelekea wafanyabiashara wengi kudhulumiwa bidhaa au mali zao, kuvamiwa, kuumia na wakati mwingine kuuza bidhaa kwa bei ya hasara. Watanzania wanaweza kufanya biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na bidhaa zao kutolipa ushuru wa forodha ilimradi wamezingatia taratibu zilizokubalika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, mfanyabiashara atatakiwa kuwa na hati ya kusafiria pindi anapotaka kuvuka mpaka kwenda Nchi Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 16 Juni 2016.
No comments:
Post a Comment