Mkutano huu ambao umeandaliwa rasmi na Umoja wa vijana CCM kwa kushirikiana na Chama cha kikomunisti cha watu wa China (CPC) umekua na lengo la kuhamasisha ushirikiano na kujenga uhusiano mwema kwa ajili ya kukuza uchumi kati ya Afrika na China.
Mapema jioni ya juzi, Rais Mugabe aliwasili jijini Arusha na kulakiwa na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Gharib Bilal ambaye aliambatana na viongozi wengine wa Serikali akiwemo Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana na Naibu Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Stephen Masele.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Rais Mugabe ambaye wakati wa mkutano alipewa majina mbalimbali kama “Mtoto wa kweli wa Afrika” na “Kiongozi asiyetetereka” alisema anashukuru na pia anafurahia kualikwa kwenye mkutano wa viongozi vijana kama huu licha ya kwamba yeye ni mzee wa miaka 91. Alisema licha ya uzee wake akili na mawazo yake bado ni machanga kama walivyo vijana wenyewe na kuwapongeza kuwa wamefanya kitu sahihi.
“Katika ujana tunapambanua mapito yetu na katika uzee tunatengeneza yajayo”. Mkutano kama huu ni njia mojawapo ya kuwa na ushirikiano na uhusiano mzuri kati ya vizazi na vizazi na kuwafanya vijana kutengeneza kesho iliyo na matumaini... “Siwezi kukataa mwaliko wa kuja nchi kama ya Tanzania kwa kua tumekua bega kwa bega katika vita ya kupigania ukombozi na hapa ndipo mipango yote ya kupigania uhuru ilipo zaliwa”
Mkutano huo ambao ulianza mapema asubuhi ya tarehe 28 Machi 2015 mazungumzo yalianza kutoka kwa wawakilishi wa nchi mbalimbali za Afrika ambao walizungumzia mambo mbalimbali muhimu ya kimaendeleo, ushirikiano na urafiki kati ya China na Afrika.
Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Mhe. Bernad Membe ambaye nae alipata muda wa kuzungumza alianza kwa kuwakaribisha wageni wote nchini na kuongelea kile alichokiita “The Syndrome”(Uhusiano unaofanana) kati ya Afrika na China. Mheshimiwa Membe alisema anafurahia uhusiano mzuri ulipo kati ya Afrika na China huku akiitaja nchi ya Tanzania kama mfaidika mkuu wa uhusiano huo.
Tanzania ina kila sababu ya kuishukuru nchi ya China kwa kuwa uhusiano wao na wetu ni wa kudumu na wameonyesha mapenzi ya dhati kwa waafrika ya kutaka kutusaidia alisema Membe.
“Angalia mfano wa reli ya Tazara, uwanja wetu wa Taifa na Jengo la umoja wa Afrika (AU) ni baadhi ya maeneo na majengo ambayo wachina wametujengea bure bila kudai chochote” aliongeza Waziri Membe.
Hata hivyo Waziri huyo wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa alisema anatarajia kuwa kupitia mkutano huu vijana wataweza kujifunza na kujadili njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana. “Ningependa wajadili kuhusu njia gani ya kuongeza ajira nchini kwa mfano kama ni biashara au uwekezaji basi waongelee kuhusu biashara zenye kuajiri vijana wengi kama viwanda vya nguo, cement au vile vya kusindika ili kuweza kuwafaidisha watanzania walio wengi.
No comments:
Post a Comment