Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday 26 November 2014

MTENDAJI MKUU BRN BW. OMARI ISSA ATUNUKIWA TUZO YA MBIA BORA YA MWAKA


MTENDAJI Mkuu wa Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji na Usimamizi wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Bw. Omari Issa (pichani) ameanza kutambulika mchango wake hapa nchini baada ya kutunukiwa Tuzo ya Mbia Bora wa Umma wa Mwaka (Public Partner of the Year).

Tuzo hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na Taasisi ya Maafisa Watendaji Wakuu (CEOs-Roundtable) inayojumuisha watendaji waandamizi kutoka sekta binafsi.

Bw. Issa, ambaye ni  mmoja wa watanzania wanaoheshimika kimataifa baada ya kufanyakazi kwa muda mrefu katika taasisi kubwa za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia, IFC na Celtel International aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Juni, 2013 kuwa Mtendaji Mkuu wa PDB.

Katika mwaka mmoja wa utendaji wake Bw. Issa amekuwa akihakikisha Mpango wa BRN unaoweka vipaumbele katika maeneo ya kimakakati kitaifa unatekelezwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya sekta ya umma na binafsi.

Katika mwaka mmoja wa kuwepo PDB mbali ya kuifanya BRN kuanza kutekeleza miradi yake kwa ufanisi, Bw. Issa pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha BRN inakuwa chachu ya kuchagiza uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

Julai mwaka huu sekta ya saba ya kimkakati ya uboreshaji wa mazingira ya biashara iliingizwa katika BRN ikiwa na lengo la kuhakikisha vikwazo katika usajili wa makampuni, utozaji wa kodi nyingi na rushwa katika biashara vinaondoshwa ili kuifanya Tanzania kuwa sehemu bora zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

BRN pia hivi karibuni iliendesha kongamano lililokusanya wawekezaji mbalimbali ambapo walioneshwa maeneo ya uwekezaji ili kuwafanya washirikiane na Serikali katika mageuzi yanayoletwa na mfumo huo.

Mbali ya hatua hizo katika eneo la uwekezaji na hasa ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi BRN imechangia utaalamu na msukumo wa kurekebishwa kwa Sheria ya Ushirikiano wa Sekta za Umma na Binafsi kwa lengo la kuhakikisha ufanisi na usimamizi.

Katika hafla hiyo pia Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alipewa Tuzo ya Mafanikio ya Wakati Wote kwa mchango wake katika kuboresha na kuipa nafasi sekta binfsi nchini.

No comments:

Post a Comment