TAARIFA KWA UMMA
Pamoja na taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania mnamo tarehe 20 Julai 2014 kuhusiana na Benki ya FBME, Benki Kuu inapenda kuujulisha umma kuwa Benki Kuu ya Cyprus mnamo tarehe 18 Julai 2014, kupitia notisi yake kwa umma iliyotolewa siku hiyo hiyo, ilichukua jukumu la menejimenti ya uendeshaji wa shughuli za tawi la Benki ya FBME iliyopo Cyprus. Hii ni kutokana na taasisi ya Financial Crimes Enforcement Network (FinCEN) ya Marekani kutoa Notisi iliyoihusisha Benki ya FBME na uhalifu wa kutakasa fedha haramu.
Kutokana na uamuzi huo wa Benki Kuu ya Cyprus kuchukua jukumu la menejimenti ya uendeshaji wa shughuli za tawi la Benki ya FBME lililopo Cyprus na athari zinazoweza kujitokeza katika mfumo wa kibenki hapa nchini, umma unataarifiwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania, kwa mujibu wa kifungu namba 56(1)(g)(iii) cha Sheria ya Mabenki ya Vyombo vya Fedha ya mwaka 2006, imechukua jukumu la menejimenti ya uendeshaji wa benki ya FBME Tanzania kuanzia tarehe 24 Julai 2014.
Umma unataarifiwa pia kuwa wakati wote Benki ya FBME Tanzania itakapokua chini ya uendeshaji wa Benki Kuu, shughuli zake za kibenki zitaendelea kama kawaida. Benki Kuu ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha usalama wa amana za wateja kadri ya matakwa ya sheria.
BENKI KUU YA TANZANIA
24 JULAI 2014
No comments:
Post a Comment