SME Impact
Fund (SIF)-Mfuko wa wafanyabiashara wadogo na wa kati umezinduliwa rasmi (19 Juni, 2014) ndani ya hoteli ya New Africa, jijini Dar es salaam na kundi la
kampuni za Match Maker Group. Mjasiriamali mkongwe na Mwenyekiti wa Private
Sector Foundation (PSF) Dk. Reginald Mengi alikuwepo kama mgeni rasmi wa hafla
hiyo.
Kundi la
kampuni za Match Maker Group (MMG) lina miliki kampuni tanzu mbili ikiwemo
Match Maker Associates Ltd (MMA) na Match Maker Fund Management (MMFM). Ambapo
MMA Ltd ndio kampuni mama, yenye kushughulika na huduma za ushauri fasaha
kibiashara kwa zaidi ya miaka kumi sasa.
“Match Maker Associates Ltd ndio
msingi wa Match Maker Group, mimi na Henri Van Der Land tulisajili na kuendesha
MMA mnamo mwaka 2003, kama kampuni ya sekta binafsi inayotoa huduma za ushauri
fasaha na mafunzo ya biashara. Sasa miaka kumi baadae tumeshuhudia kukua vizuri
kwa MMA Ltd upande wa bidhaa na wateja wake. MMA inatoa huduma zake hususani
ndani ya nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Mpaka sasa, MMA Ltd imeshatoa
huduma za ushauri fasaha na mafunzo ya biashara kwenye miradi 140 ndani ya nchi
zaidi ya 15.”Alifafanua Bw Peniel Uliwa, Mkurugenzi Mshiriki wa MMG wakati
akitoa hotuba kuwataarifu waalikwa juu ya MMG na SIF.
“Chanzo cha kuwa na mfuko kama SIF kilitokana
na malalamiko mbalimbali tuliyokuwa tunakumbana nayo kwenye shuguli zetu ndani
ya MMA Ltd. Ambapo wafanyabiashara wadogo na wakati kwenye sekta ya kilimo
walituambia wanashindwa kuendeleza kibiashara zao kutokana na ugumu wa upatikanaji
wa mitaji ya kuendeleza biashara zao.
Hapa tukagundua kuna tatizo kubwa linalokosesha ukuaji kiuchumi kwa
wajasiliamali hawa na vivyo kuwakosesha kufikia ndoto zao kibiashara. Basi
tukaanza mchakato na hatimaye kuanzisha na kusajili MMFM Ltd”. Alielezea Bw
Henri Van Der Land, Mkurugenzi mshiriki wa MMG mzawa wa Uholanzi anayekaa na
kufanya kazi nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Mfuko wa ‘SME Impact Fund’ unatoa
mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na kati ndani ya minyororo
ya thamani katika sekta ya kilimo. Ikiwemo wasindikaji mazao, viwanda vya maziwa,
mafuta n.k. Mikopo inatolewa kwa wale wajasiriamali wanaoongeza thamani wenye
uhitaji wa mtaji au uwekezaji zaidi kwenye biashara zao. Mikopo ya SIF huanzia
toka millioni 100 TSHS mpaka Bilioni 1 TSHS, licha ya hii Mfuko wa SIF ndani ya
timu ya MMFM hutoa huduma za ushauri fasaha wa biashara kwa wateja wao wote ili
kuwawezesha kuendesha biashara zao kwa faida.
“MMG wamenipa taarifa kuwa kwenye
utafiti wao kabla ya kubaini mfuko huu, waligundua kuna tabaka wanaloliita
‘missing middle’. La wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati nchini ambao
hawapati huduma stahili kirahisi kwenye taasisi rasmi za fedha kama benki. Hili
lilithibitishwa kwenye mikutano ya wawekezaji mbalimbali nchini iliyofanyika
mwaka jana. Ambapo wajasiriamali wadogo na wa kati takriban 150,
walipewa fursa ya kuelezea miradi yao kwa taasisi rasmi za fedha mbalimbali
nchini na zaidi ya asilimia 80 ya hawa walifurahi sana kukutana na SIF.”
Aliongezea mgeni rasmi Dk Reginald Mengi.
Hadi sasa SIF imeshatoa mikopo 9 yenye
thamani ya 1.5 Billion Tshs (Euro 650,000) toka mwezi Julai mwaka jana. Kwenye
uzinduzi wa mfuko huu baadhi ya wafanyabiashara hawa walikuwepo wakitoa shuhuda
na taarifa fupi juu ya biashara zao; kupitia mkanda wa video uliyoonyeshwa kwa
wageni wote kwenye uzinduzi huo.
Wajasiriamali
wote waliopokea mikopo ya mfuko wa SIF ni watanzania na wameonyesha uzalishaji
endelevu kwa technolojia za kisasa wakitazamia kuwa biashara zao zitatoa faida
kwenye sekta nzima ya kilimo. Sambamba na vigezo vya SIF, wateja wake wanalazimika
kufikia viwango vilivyowekwa kwenye kanuni za kiuchumi, mazingira na jamii za
mfuko huu (SEEC).
“Naamini kabisa kwamba mfuko wa SIF
ambao tunauzindua rasmi leo, umekuja nchini kwa muda muafaka. Ikiwa ni sambamba
na kauli ya taifa ya Kilimo Kwanza na mikakati na miradi mingine ya kukuza
biashara za sekta binafsi na za jamii nchini.” Aliongezea Dk Reginald Mengi
kwenye hotuba yake kabla ya kuzinduliwa rasmi mfuko huu.
MMFM inawakaribisha wawekezaji
binafsi na taasisi mbalimbali Tanzania, kuwekeza kwenye mfuko huu kauli
iliyopewa msisitizo na mgeni rasmi. “Nawaalika wawekezaji Tanzania kuungana
mkono na wawekezaji wa SIF ili kufanikisha mpango huu bora wa huduma za fedha
na ushauri fasaha kibiashara.”
Alimalizia Dk Reginald Mengi.
Mfuko wa SIF unatarajia ndani ya
miaka kumi ya uwepo wake, kuwa utatoa mikopo kwa zaidi ya wafanyabiashara 150
nchini. Ikitoa fursa za nyongeza za kazi kwenye sekta ya kilimo na chakula
zipatazo 1000, ikiwemo na ongezeko la mapato kwa wakulima wadogo wapatao
50,000. Hii yote ikiambatana na utekelezaji wa mifumo bora ya kilimo kwa wadau
hawa. Pia wawekezaji wote ndani ya mfuko wa SIF watategemea kupata marejesho ya
mtaji wao na riba baada ya miaka kumi, wakati mfuko huu utasitishwa.
No comments:
Post a Comment