Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Tuesday, 5 May 2026

KAMPENI YA “NBC SHAMBANI” YAWASILI BABATI NA KARATU, WAKULIMA WAIKARIBISHA KWA MATUMAINI MAKUBWA

Picha ya juu: Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bw. Dominic Mbwette (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” inayoratibiwa na Benki ya NBC. Wengine pichani ni Mkuu wa Idara ya Bima wa NBC Bw. Benjamini Nkaka (wa pili kulia), Mkuu wa Kanda ya Kati wa NBC, Bw. Miraji Msuya (wa pili kushoto), Meneja wa NBC Tawi la Babati Bw Rogers Masolwa (wa tatu kushoto), Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha Rift Valley Cooperative Union (RIVACU) Bw. Yuda Peter Sulley (wa tatu kulia), Afisa Ushirika wilaya ya Hanang Bw. William Mbogoro (kushoto) na Meneja wa RIVACU, Bi. Pendoeli Valentine (kulia).
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mbwette (pichani) aliipongeza NBC kwa juhudi zake za kuwawezesha wakulima kupitia suluhisho bunifu za kifedha, akieleza kuwa kampeni hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa Babati na mkoa wa Manyara kwa ujumla.

Babati, Manyara | Mei 4, 2026 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” katika mikoa ya Manyara na Arusha, hususan wilaya za Babati na Karatu, ikiwa ni muendelezo wa jitihada zake za kuimarisha elimu ya fedha na kukuza kilimo biashara nchini.

Kupitia kampeni hiyo, benki inalenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama ufuta, dengu na mbaazi kwa kuwapatia wakulima—ikiwemo vyama vya msingi (AMCOS), vyama vikuu vya ushirika pamoja na wakulima mmoja mmoja—elimu ya kifedha na huduma za kibenki zilizobuniwa mahsusi kwa sekta ya kilimo.

Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki wilayani Babati, ukiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Dominic Mbwette, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo wakiwemo viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima. Viongozi waandamizi wa NBC walioshiriki ni pamoja na Benjamini Nkaka (Mkuu wa Idara ya Bima), Raymond Urassa (Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima), pamoja na Miraji Msuya (Mkuu wa Kanda ya Kati), wakiongoza timu ya maofisa wa benki hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mbwette aliipongeza NBC kwa juhudi zake za kuwawezesha wakulima kupitia suluhisho bunifu za kifedha, akieleza kuwa kampeni hiyo itachochea ukuaji wa uchumi wa Babati na mkoa wa Manyara kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa huduma jumuishi zinazotolewa, ikiwemo elimu ya fedha, bima na mikopo ya maendeleo kwa wakulima na vyama vyao.

Aidha, alibainisha kuwa mkakati wa elimu ya fedha ndani ya kampeni hiyo utasaidia kuimarisha vyama vya ushirika na kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu umuhimu wa kuweka akiba, kutumia bima—ikiwemo bima ya afya na mazao—na kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo ili kuongeza tija na kupunguza hatari.

“Mpango huu utahamasisha wakulima kujiunga na mifumo rasmi ya kifedha, jambo litakalosaidia kukuza uchumi jumuishi na kuimarisha sekta ya kilimo,” alisema Mbwette, huku akiwahimiza wakulima kufungua akaunti za NBC Shambani.

Kwa upande wake, Bw. Nkaka alisema NBC inaendelea kubuni suluhisho za kifedha zinazounga mkono azma ya Serikali ya kuongeza ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo mwaka 2030. Aliongeza kuwa benki hiyo pia inawekeza katika elimu ya fedha, huduma za kidijitali na bima ili kupunguza hatari zinazowakabili wakulima.

Akifafanua zaidi, Bw. Urassa alisema kampeni hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miezi minne kuanzia Juni hadi Septemba, ikijumuisha mafunzo ya kina kuhusu huduma za kifedha kwa sekta ya kilimo. Huduma hizo ni pamoja na bima ya mazao na afya, uwakala wa benki, suluhisho za kidijitali pamoja na mikopo ya pembejeo na zana za kilimo.

Mbali na hilo, kampeni hiyo imebeba motisha mbalimbali kwa washiriki watakaofanya vizuri, ikiwemo zawadi za simu janja, pikipiki na kompyuta mpakato kwa wakulima binafsi, AMCOS na vyama vikuu vya ushirika. Ili kushiriki, wakulima wanatakiwa kufungua akaunti ya NBC Shambani na kuitumia kikamilifu katika miamala yao ya kifedha.

“Lengo letu ni kuwahamasisha wakulima kutumia mifumo rasmi ya kifedha kwa kuhifadhi fedha zao na kupata huduma bora zaidi. Kupitia kampeni hii, tunahamasisha matumizi ya akaunti za ‘NBC Shambani’ zisizo na makato ya kila mwezi pamoja na mikopo ya zana za kilimo kama matrekta kwa wakulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika,” alieleza Urassa.

Kwa upande wao, wawakilishi wa wakulima wilayani humo, Margaret Simon na Yuda Sulley, walieleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo. Walibainisha kuwa akaunti ya NBC Shambani isiyo na makato, pamoja na elimu ya fedha na huduma za bima, ni hatua muhimu katika kuboresha shughuli zao za kilimo.

“Huduma za bima ya afya na mazao ni muhimu sana kwetu, hasa katika kukabiliana na changamoto zisizotarajiwa. Elimu ya fedha pia itatusaidia kupanga na kusimamia mapato yetu kwa ufanisi zaidi,”alisema Bi. Margaret.

Ikiwa tayari imefika katika mikoa kadhaa ikiwemo Ruvuma, Songwe na Singida katika awamu hii, kampeni ya “NBC Shambani” inaendelea kujidhihirisha kama chachu ya mabadiliko chanya kwa wakulima nchini—ikiwawezesha kifedha, kupunguza hatari za kilimo, na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.






No comments:

Post a Comment