Aprili 21, 2026 - Katika hatua nyingine muhimu ya kukuza usawa wa kijinsia na kuimarisha uongozi wa wanawake ndani ya sekta ya fedha, Equity Bank Tanzania imezindua rasmi Equity Bank Women in Leadership Development Programme—mpango wa kimkakati unaotekelezwa kwa ushirikiano na International Finance Corporation (IFC) pamoja na Impact Leadership Academy.
Programu hii ya miezi minne inalenga kujenga safu imara ya viongozi wanawake wa baadaye ndani ya benki, huku ikisisitiza kuwa ajenda ya watu ni msingi wa kujenga taasisi imara, jumuishi na yenye matokeo endelevu.
Kupitia mpango huu, wanawake wafanyakazi 80 watanufaika—sawa na asilimia 32 ya wafanyakazi wanawake wa benki—wengi wao wakiwa wataalamu vijana wenye matarajio makubwa ya ukuaji wa kitaaluma. Washiriki watapitia safari ya kina ya maendeleo ya kiuongozi, itakayojumuisha tathmini binafsi, warsha za uongozi, uongozi elekezi (coaching), pamoja na malezi ya kitaaluma (mentorship). Hii inaakisi dhamira ya Equity ya kuwekeza kwa makusudi katika rasilimali watu wake na kuwaandaa kwa nafasi za juu zaidi za uongozi na uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Bank Tanzania, Bi. Isabella Maganga, alisisitiza kuwa programu hiyo si tukio la kawaida, bali ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa taasisi.
“Kwetu sisi, kuendeleza viongozi wanawake si jambo la ziada; ni sehemu ya kujenga taasisi yenye nguvu, yenye mtazamo mpana, na inayoweka watu wake katika nafasi ya kuleta matokeo ya muda mrefu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Rasilimali Watu wa benki hiyo, Bi. Martha Stephen Kimweri, alibainisha kuwa uzinduzi huu ni hatua ya kugeuza dhamira kuwa vitendo.
“Katika Equity tunaamini kuwa vipaji vipo kila mahali, lakini fursa lazima ziundwe kwa makusudi, zikuziwe na zidumishwe. Kupitia programu hii, tunafungua njia zitakazowawezesha wanawake zaidi kukua, kuongoza na kuchangia kikamilifu katika mafanikio ya pamoja ya taasisi,” alieleza.
Ushirikiano na IFC unaipa programu hii uzito wa kipekee wa kimataifa, ukiakisi dhamira ya pamoja ya kuendeleza uongozi wa wanawake kupitia ushirikiano na rasilimali za kitaalamu. Akizungumza kwa niaba ya taasisi hiyo, Meneja wa Kanda wa IFC, Paula Phillipe, alisema:
“Kuwekeza katika wanawake viongozi si suala la uwakilishi pekee, bali ni njia ya kuimarisha taasisi, kupanua uwezo wa uongozi, na kujenga mazingira ya ukuaji jumuishi na endelevu.”
Ikiwa chini ya mwavuli wa Equity Inspire Program (EQUIP), mpango huu unaimarisha dhamira ya Equity ya kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi, huku ukijenga taasisi yenye utofauti, ujumuishi na utendaji wa hali ya juu.
Kwa kuwekeza kwa makusudi katika wanawake 80, Equity Bank Tanzania inaweka bayana kwamba maendeleo ya watu ndiyo msingi wa mafanikio ya biashara—na kwamba viongozi wa kesho hujengwa leo.
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment