Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 29 January 2026

NMB YAZINDUA AGENDA 2030, YAFUNGA MTP 2025 KWA FAIDA YA KIHISTORIA YA SH. TRILIONI 1.1

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (katikati), pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia), na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Benson Mahenya (wa pili kushoto), wakizindua kwa pamoja Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, unaojulikana kama Agenda 2030, wa Benki ya NMB. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB, Prof. Sylvia Temu, na kulia ni Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori.

Dar es Salaam — Benki ya NMB imezindua rasmi Mpango Mkakati wa Muda wa Kati wa miaka mitano kuanzia 2026 hadi 2030, unaojulikana kama Agenda 2030, sambamba na kutangaza mafanikio makubwa ya Mpango Mkakati uliopita (MTP 2025), uliomalizika kwa rekodi ya kihistoria ya faida kabla ya kodi (PBT) ya Sh. Trilioni 1.1 kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Agenda 2030, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo inajivunia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji wa MTP 2025, uliodumu kwa miaka mitano, ambapo ilivuna faida ya jumla ya Sh. Trilioni 1.1, sawa na ongezeko la asilimia 15.

Kwa mujibu wa Bi. Zaipuna, katika mwaka 2025 pekee, NMB ilirekodi Faida Baada ya Kodi (PAT) ya Sh. Bilioni 750, ikiwa ni ongezeko la asilimia 16, huku mapato yote ya benki yakifikia Sh. Trilioni 1.82 (ongezeko la asilimia 11). Aidha, mali zote za benki zilifikia thamani ya Sh. Trilioni 17.2.

Katika kipindi chote cha utekelezaji wa MTP 2025, NMB imepata matokeo madhubuti yaliyojumuisha utendaji imara wa kifedha na mchango mpana katika kuchochea na kuwezesha shughuli za kiuchumi nchini,” alisema Bi. Zaipuna.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitano, benki ilizalisha faida ya jumla ya Sh. Trilioni 2.7, ikitoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh. Trilioni 27.6, huku amana za wateja zikifikia Sh. Trilioni 12.4. Idadi ya akaunti za wateja pia iliongezeka hadi kufikia milioni 9.9.

Bi. Zaipuna alisema mafanikio hayo yanaipa NMB msingi imara wa kuingia katika Awamu mpya ya kimkakati ya Agenda 2030, ambayo inalenga kujenga benki yenye ukuaji endelevu unaoakisi mahitaji ya soko ya sasa na ya baadaye.

Mpango Mkakati huu mpya umejengwa juu ya mafanikio yaliyopatikana, na unaweka dira ya ukuaji endelevu unaoongozwa na Mteja, Teknolojia na Tija ya Kiutendaji,” alisema.

Katika Agenda 2030, NMB itaweka mkazo katika kuboresha kwa kiwango cha juu huduma kwa wateja, kuimarisha mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya kimkakati ya takwimu (data), pamoja na kufadhili sekta za kimkakati zinazochochea ajira, uzalishaji na ongezeko la thamani katika uchumi. Sekta hizo ni pamoja na kilimo, ujenzi, viwanda, utalii, nishati na madini.

Aidha, benki inapanga kupanua wigo wa shughuli zake nje ya huduma za kawaida za kibenki na kuvuka mipaka ya Tanzania kwa kuwekeza kimkakati nje ya nchi.

Tunakwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania katika viwango vya ubora na ufanisi nje ya mipaka ya nchi,” alisisitiza Bi. Zaipuna.

Kwa upande wake, Msajili wa HazinaNehemiah Mchechu, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na wafanyakazi wa NMB kwa mafanikio makubwa ya MTP 2025 pamoja na matokeo ya mwaka hadi mwaka.

Mchechu alisema NMB ni kiongozi sahihi wa Sekta ya Fedha katika kutafsiri na kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa Rais alimtuma kufikisha salamu za pongezi kwa benki hiyo kutokana na ufanisi mkubwa walioupata.

Mheshimiwa Rais anawasubiri kwa hamu kwenye gawio lake mwezi Juni mwaka huu. Kwa mafanikio haya, nina uhakika anatamani sana kukutana nanyi,” alisema Mchechu.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha MTP 2025, Serikali imepokea gawio la Sh. Bilioni 224 kutoka NMB, huku thamani ya uwekezaji wa Serikali katika benki hiyo ikizalisha jumla ya Sh. Bilioni 670 ndani ya miaka mitano.

Mchechu aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuisimamia NMB kwa ukaribu na kuhakikisha inakuwa na Bodi ya Wakurugenzi imara, yenye weledi na isiyoathiriwa na siasa, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Tutahakikisha NMB inalindwa dhidi ya siasa zisizoendana na biashara, na tutaendelea kusimama imara nanyi katika kila hatua,” alisisitiza.

Uzinduzi wa Agenda 2030 unaashiria hatua mpya kwa NMB katika safari yake ya ukuaji endelevu, ubunifu wa kidijitali na mchango mpana zaidi katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania na ukanda wa nje ya nchi.










No comments:

Post a Comment