![]() |
| Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Benki ya Stanbic, Omari Mtiga, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba. |
Pwani, Oktoba 10, 2025 — Benki ya Stanbic imekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 60 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani – Tumbi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuboresha huduma za afya nchini.
Msaada huo, unaojumuisha kompyuta, vitanda, viti vya wagonjwa (wheelchairs), matoroli, na vifaa vya usafi, ulikabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Stanbic Bank, Bw. Omari Mtiga, kwa niaba ya benki hiyo, na kupokelewa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Tumbi, Dk. Amani Malima.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Bw. Mtiga alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya mpango endelevu wa uwajibikaji wa kijamii (CSR) wa Stanbic Bank, unaolenga kurudisha fadhila kwa jamii, sambamba na maadhimisho ya Miaka 30 ya Kukua Pamoja tangu benki hiyo ianze kutoa huduma nchini Tanzania.
“Tunatambua mchango mkubwa wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu, tunalenga kusaidia hospitali kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi wa watoa huduma. Hii ni moja ya njia tunazosherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania,” alisema Bw. Mtiga.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirya Ukio, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo, akibainisha kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka, kwani hospitali inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa baadhi ya vifaa muhimu. Tunawashukuru Stanbic Bank kwa moyo huu wa kizalendo,” alisema Dk. Ukio.
Hafla hiyo pia ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja 2025, inayoongozwa na kaulimbiu “Mission Possible”, ambapo wafanyakazi wa Stanbic Bank walijitolea kufanya usafi katika baadhi ya maeneo ya hospitali kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.



No comments:
Post a Comment