Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday, 18 May 2023

BENKI YA I&M YAZINDUA ‘WAKALA’ KUPANUA WIGO WA HUDUMA ZA KIFEDHA

Mkurugenzi wa Benki ya I&M, Zahid Mustafa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa huduma ya wakala mtaani, ambao wateja wa benki hiyo watakuwa wakipata huduma hiyo popote. Kushoto ni Emmanuel Mnema na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja, Deepali Ramayaiya. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja, Zainab Maalim.

Dar es Salaam, Tanzania, Mei 17, 2023 – Benki ya I&M Tanzania imezindua huduma yake mpya ya kibenki inayojulikana kama ‘Wakala’ (Agency Banking) ili kukuza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Wateja wao. Huduma hiyo inayolenga kukuza wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha nchini imezinduliwa tarehe 17 Mei katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.

Huduma ya Wakala itawawezesha wateja kupata huduma za kibenki kwa urahisi kupitia mtandao mkubwa wa mawakala walioko kote nchini. Wateja wataweza kufanya aina mbalimbali za miamala ikiwemo kuweka na kutoa pesa, kuangalia salio, kutuma pesa, na kupata taarifa za miamala.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya I&M Tanzania, Bw. Zahid Mustafa, alisema, "Huduma yetu mpya ya ‘Wakala’ au Agency Banking ni hatua muhimu katika jitihada zetu za kukuza upatikanaji wa huduma za kibenki kwa Watanzania. Kupitia huduma hii, wateja wetu hawatalazimika kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma za kibenki. Benki imejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja wetu, na huduma hii mpya ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yetu."

Huduma ya Wakala itawezesha upatikanaji wa huduma za kibenki, hasa kwa wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa miji ambako hakuna matawi ya benki karibu nao. Huduma hii itawapa wateja urahisi na unafuu katika kufikia huduma za kibenki, ikiwa inaenda sambamba na dhamira ya Benki ya I&M Tanzania ya kutoa huduma za kiwango cha kipekee.

Naye Mkuu wa Idara ya Wateja, Bi. Zainab Maalim, alisema, "Hadi sasa, benki imefanikiwa kusajili mawakala zaidi ya 200 kote nchini, na idadi hiyo inazidi kuongezeka. Kupitia mawakala hawa, huduma zetu zitaweza kufikia wateja wengi zaidi.”

Akifunga kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Idara ya Wateja Rejareja, Deepali Ramaiya alisema kuwa huduma ya Wakala inalenga kuchangia katika juhudi za serikali katika kufanikisha malengo ya kitaifa juu ya huduma jumuishi za kifedha. Uzinduzi wa huduma hiyo mpya ya Wakala unakuja wakati ambapo Serikali ya Tanzania inaweka mkazo zaidi katika kukuza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha na malipo ya kidijitali.

Kuhusu I&M

Benki ya I&M Tanzania ni moja ya benki za kibiashara zinazokua kwa kasi, zikitoa huduma mbalimbali za kibenki kwa Wateja Wakubwa (Corporate), Wafanyabiashara, Wateja Maalumu na Watu Binafsi.

Ikiwa na Makao makuu jijini Dar es Salaam, I&M Bank ni kampuni tanzu ya I&M Group PLC ambayo imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Nairobi na inaendelea kukuza uwepo wake kikanda ambapo kwa sasa inapatikana nchini Mauritius, Rwanda, Kenya, na Uganda. Benki imesajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania na ilianza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 2002 kama CF Union Bank. Mnamo Septemba 2010, Benki ilibadilisha jina lake kutoka CF Union Bank na kuwa I&M Bank (Tanzania) Limited ili kuendana na mabadiliko ya umiliki. Kwa sasa Benki inafanya shughuli zake katika miji mikubwa ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Moshi ikiwa na mipango ya kupanua wigo wa huduma na kufikia mikoa mingi zaidi Tanzania.

Benki ya I&M Tanzania ina dhamira ya kuwa Mshirika wa Ukuaji kupitia Huduma za Kifedha nchini Tanzania kwa kutoa huduma za kibenki zenye ubunifu na zinazoendeshwa na mahitaji ya soko.

Kwa taarifa zaidi tembelea www.imbank.com/tz

Mawasiliano

Zainab Maalim
Head of Customer,
Zainab.Maalim@imbank.co.tz
+255 765 210014

No comments:

Post a Comment