Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Wednesday, 2 November 2022
BENKI YA EXIM YAJA NA “CHANJA KIJANJA, KIMASTA ZAIDI’’ KUHAMASISHA MALIPO KWA NJIA YA KADI
Dar es Salaam, 1 Novemba 2022 - Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni maalum inayolenga kuwashawishi wateja wake wanaomiliki kadi za MasterCard kufanya miamala zaidi kwa kutumia kadi hizo badala ya malipo ya fedha taslimu pindi wanapohitaji kufanya malipo mbalimbali katika vituo vya mauzo (POS) au tovuti za biashara ya mtandaoni.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la “Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’ inatoa fursa kwa jumla ya washindi 185 miongoni mwa wateja wa benki hiyo wanaotumia kadi zao za Exim Mastercard kufanya miamala, kuwa kwenye nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, Simu janja (Smart Phones) na safari zilizolipiwa gharama zote kwenda mapumziko katika mataifa ya Falme za Kiarabu, Uturuki na Afrika Kusini wao pamoja na wenza wao.
Akielezea namna kampeni hiyo ya miezi mitatu itakavyoendeshwa katika hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi na bishara za kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo alisema, “Mtu yeyote ambaye ni mteja wa Benki ya Exim na ambaye ana kadi ya Exim Bank MasterCard yoyote anafuzu moja wa moja kushiriki katika kampeni hii.’’
Kwa mujibu wa Lyimo, wakati wa kampeni hiyo kila muamala wenye thamani ya Tsh 100,000/= na zaidi ukiwa umefanyika kwa mara moja au zaidi kupitia kadi ya MasterCard ya benki hiyo, muhusika ataingia kushiriki bahati nasibu ya kumpata mshindi.
“Kila wiki, kutakuwa na droo na wateja 15 watakaobahatika watapata nafasi ya kujishindia zawadi ya fedha taslimu Tshs. 100,000/=.’’ alitaja huku akiongeza, “Aidha, kila mwezi kutakuwa na droo ambapo wateja watapata nafasi ya kujishindia simu janja aina ya iPhone 14 Pro mpya kabisa huku sifa ya chini katika droo hii ya mwezi ikiwa ni muhusika kufanya matumizi yenye thamani ya Tshs 400,000 na zaidi katika risiti moja au kwa jumla.''
Akizungumzia zawadi kuu kwa washindi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Idara ya Huduma Mbadala Kupitia Mifumo ya Kidigitali, Silas Matoi alisema, washindi hao watazawadiwa safari ya mapumziko ya siku tano (5) wao pamoja na wenza wao, safari ambayo itagharamiwa kila kitu na benki ya Exim ikiwemo visa, tiketi ya ndege pamoja na pesa za matumizi.
“Hivyo basi mshindi wa kwanza atajishindia zawadi ya kwenda Dubai, yeye na mwenza wake na wakiwa huko watapata fursa ya kutembelea vituo mbalimbali ikiwemo ‘Museum Of The Future’ pamoja na Jangwa la Safari. Mshindi wa pili yeye atakwenda nchini Uturuki na mwenza wake na wakiwa huko watapata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa ikiwemo Msikiti maarufu wa Bluu uliopo kwenye jiji la Istanbul,’’ alisema.
Aidha, Matoi aliongeza kuwa mshindi wa tatu atapata fursa ya kutembelea nchi ya Afrika Kusini yeye na mwenza wake ambapo wakiwa huko pia watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo na Table Mountains ambao ni maarufu nchini humo. Kiujumla washindi wote watapatikana kupitia bahati na nasibu zitazofanyika chini ya usisamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo, Stanley Kafu alisema dhamira ya msingi ya benki hiyo ni kuandaa jamii yenye utamaduni wa kutotembea na pesa taslimu na badala yake wafanye malipo kwa njia za kielektroniki hatua ambayo pia imekuwa ikipigiwa chapuo na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia katika kufanya miamala ya kifedha.
“Benki ya Exim kihistoria imekuwa mstari wa mbele kuleta mageuzi ya kihuduma hapa nchini. Katika kufanikisha mageuzi hayo tumekuwa tukitumia namna mbambali ikiwemo kutoa zawadi kwa wateja wetu ili tu tuweze kwenda nao sambamba katika mageuzi haya. Tunaamini kupitia kampeni hii tunakwenda kuleta mabadiliko yenye tija na faida kubwa kwenye mfumo mzima wa sekta ya fedha hapa nchini… Chanja Kijanja, Kimasta Zaidi’’, alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment