Akizungumza wakati wa mkutano huo wa asubuhi ‘Power breakfast business meeting’ ulioandaliwa na benki hiyo mapema hii leo jijini Arusha, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Shughuli za Serikali wa NBC , Bw James Meitaron aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw Theobald Sabi alisema mkutano huo ni mwanzo wa mtiririko wa mikutano mingi kama hiyo mahususi kwa wateja wakubwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma.
“Hatua hii ya kukutana na wateja wetu wakubwa inatokana na maboresho makubwa tuliyofanya kwenye huduma zetu ikiwemo kutambulisha huduma mpya zilizorahisishwa zaidi kidigitali zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu wakiwemo hawa wakubwa. Tumeona tukutane nao ili tuweze kutambulisha kwao mapinduzi haya kihuduma sambamba na kupokea mrejesho kutoka kwao kuhusu huduma zetu’’.
“Kupitia mpango huu pia tunapata fursa ya kuelezea mikakati yetu mipana inayolenga kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wateja wetu, kuwasogezea huduma za kibenki karibu zaidi sambamba na kuwajengea mitandao ya kibiashara miongoni mwao.’’
“Tunayafanya haya kwa urahisi zaidi kwa kuwa sisi ni taasisi ya kifedha yenye uzoefu mkubwa zaidi nchini huku tukiwa na mtandao mpana wa matawi, mawakala na huduma za kidijitali. Uzoefu wetu sokoni unatupa faida ya kutoa huduma zinaendana na mahitaji stahiki ya wateja wetu.’’ Alisema.
Alitaja baadhi ya huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wateja wakubwa na serikali kuwa ni pamoja na huduma za masoko ya fedha (financial markets), usimamizi wa madeni (Dept management), mikopo ya mashirika (corporate finance) pamoja na huduma za malipo ya serikali (GePG na MUSE) ambapo benki hiyo inahudumia takribani asilimia10 ya makusanyo yote ya serikali huku lengo likiwa ni kuhudumia makusanyo hayo kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Bw Meitaron miongoni mwa sekta muhimu ambazo benki hiyo imekuwa ikitoa kipaumbele ni pamoja na miradi ya kimkakati ikiwemo miradi ya maliasili, miundombinu, nishati, kilimo pamoja na miradi ya mawasiliano.
Akizungumzia umuhimu wa hatua ya benki hiyo kukutana na wateja hao, Mkurugenzi wa jiji la Arusha Bw Hargeney Chitukuro alisema hatua hiyo imekuja wakati muafaka hasa katika kipindi hiki ambacho mkoa huo upo kwenye mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana ustawi mkubwa wa sekta ya utalii ikiwa ni matunda ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mkakati wa Royal Tour.
“Kwa sasa mkoa wa Arusha tupo kwenye kasi kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi yanayochagizwa na ukuaji wa sekta ya utalii, biashara, kilimo na viwanda. Ni habari njema kwetu kuona kwamba benki ya NBC ambayo inahudumia wadau wengi kwenye sekta hizi ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa serikali wanatuunga mkono kupitia huduma zao za kisasa ikiwemo zile za kidigitali ambazo kiukweli zimekuwa msaada mkubwa hususani kwenye huduma za miamala ya kifedha na makusanyo ya serikali,’’ alisema.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mkutano huo Bi. Jully Bede Lyimo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), aliishukuru Benki ya NBC kwa kuandaa mkutano huo akionesha kuguswa na maboresho makubwa ya kihuduma yanayoendelea kuoneshwa na benki hiyo huku benki hiyo akiisihi kufanya uwekezaji zaidi katika sekta ya utalii.
"Napenda kuwashukuru uongozi wa Benki ya NBC kwa kuja na wazo zuri la kukutana nasi, wateja wao, na kubadilishana maoni. Pia natoa wito kwa Benki kuipa kipaumbele zaidi sekta ya utalii nchini na hivyo kuwafikia kikamilifu na kutoa masuluhisho ya mahitaji ya kifedha ya wale walio katika mnyororo wa thamani wa sekta hiki muhimu ya utalii,” alisema.
No comments:
Post a Comment