- Zaidi ya wanafunzi 81,500 kufaidika na matumizi ya kompyuta zilizounganishwa na mtandao wa intaneti bure
Ushirikiano huu utawafaidisha zaidi ya wanafunzi 81,500 kutoka shule za msingi na sekondari 163 zilizoko maeneo mbalimbali nchini ambao wamekabidhiwa kompyuta 806, vipanga njia (router 163) ambavyo vimeunganishwa na muda wa maongezi kwa muda wa mwaka mmoja, vyote vikiwa na jumla ya TSh390,274,905.
Wakati huo huo zaidi ya wanafunzi 2,500 katika shule za sekondari za Chikola, Membe, Intela, Mumi na Mazae mkoani Dodoma watafaidika na matumizi ya kompyuta hizo kufuatia shule hizo kupewa msaada wa kompyuta, routers na printer katika mradi huu.
Mwaka jana, Vodacom ilishirikiana na UCSAF kutoa elimu ya kidijitali shuleni nchini kwa kuzingatia upana wa miundombinu ya mtandao wake. Hadi kufikia mwisho wa mradi huu zaidi ya wanafunzi 81,500 katika shule 163 watafaidika na msaada wa kompyuta na kuunganishwa na huduma ya intaneti bure.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Elias Kwandikwa, alisema mahitaji ya elimu bora kwa kutumia teknolojia ya kisasa hayaepukiki ikiwa taifa lina dhamira ya kuandaa vijana kwa ajili ya mfumo wa sasa wa kidijitali.
“Serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote, umeleta TEHAMA, na sasa kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Tanzania wanaziunganisha shule hizo na mtandao wa intaneti ambapo Walimu na Wanafunzi watapata nafasi ya kutafuta materials za kujifunzia” alisema Mh Kwandikwa.
Naibu Waziri aliongeza kwamba kwa sababu Vodacom wana portal iliyo chini ya mradi wa Instant Schools unaoitwa Instant School, aliwaomba Waalimu kuwapa nafasi wanafunzi ili wajifunze Zaidi kupitia vifaa hivyo.
“Sisi tumetoa baadhi ya vifaa, na tunawashukuru Vodacom Tanzania PLC kwa msaada huu utakaowawezesha walimu na wanafunzi kufundisha, kusoma na kuongeza uwezekano wa kupata taarifa mbalimbali.” Aliongeza Naibu Waziri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC Hisham Hendi, alisema msaada huo ni sehemu ya ajenda ya Vodacom kukuza elimu kupitia mfumo wa kidijitali hasa kwa sehemu za vijijini nchini..
“Vodacom Tanzania PLC tunaamini kwamba, katika wakati ujao teknolojia itakuwa kiungo muhimu katika kuunganisha fursa kwa kila mmoja ili kufikia mahitaji muhimu, sekta ya elimu ni mahala pa kuanzia. Tuna furaha kushirikiana na serikali ili kuhakikisha kwamba watu wengi wanashiriki katika mfumo wa sasa wa kidijitali. Pamoja na router hizi tulizotoa, ili kuhakikisha kwamba hawakosi intaneti, tumeamua kuwaunganisha na kifurushi cha mwaka mzima kwa kila shule, ili wajisomee bila tatizo lolote,” Hendi alisema
Halikadhalika kompyuta hizi zitawawezesha walimu na wanafunzi kutumia mfumo wa Portal kupitia mradi wa Instant School ambao pia unasimamiwa na Vodacom Tanzania Foundation kwa ajili ya kupata zana mbalimbali za kielimu bure kwa kutumia simu ya mkononi na kompyuta, hivyo kuchochea usomaji kidijitali.
“Hadi sasa mfumo wetu wa Instant School umetembelewa na wageni wapatao 65,916 ambapo wote wamejionea faida kwa kusoma kidijitali,” aliongeza Hendi.
“Ushirikiano huu unakwenda sambamba na mkakati wa kampuni wa kutoa rasilimali ili kusaidia upatikanaji wa maendeleo katika sekta ya elimu,” Hendi aliongezea kusema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema, “Tunashukuru kwa ushirikiano huu na Vodacom kuhakikisha mpango wetu unafanikiwa kwa kuunganisha shule za umma na upatikanaji intaneti ili kutumia vifaa vya ICT kikamilifu. Mchango huu unasaidia mpango wetu wa kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kila mahali haswa katika maeneo ya vijijini,”
Tukio la leo ni mwanzo wa awamu ya pili ya utoaji wa msaada wa kompyuta kwa shule za umma Tanzania Bara na Zanzibar chini ya ushirikiano wa Vodacom Tanzania Foundation na UCSAF.
Kupitia awamu ya kwanza ya mradi huu, Vodacom Tanzania PLC ilitoa kompyuta 48 kwa shule 24, hii iliwafaidisha wanafunzi Zaidi ya 15,000 nchini.
Mkurugenzi Hendi ametoa wito kwa wadau wengine kushirikiana na Vodacom Tanzania PLC ili kuhakikisha kwamba miundombinu ya kampuni hiyo inatumika kwa faida Watanzania wote.
Kwa upande mwingine, Hendi ameiomba serikali kuweka kidijitali mitaala iliyopitishwa na taasisi husika ili kuweza kutumika na watu wa rika zote wakiwemo wanafunzi ambao ndio wahitaji zaidi.
Kuhusu Vodacom Tanzania Foundation:
Vodacom Tanzania Foundation ni sehemu ya shughuli za kijamiii ya kampuni ya Vodacom Tanzania PLC ambayo ina simamia utoaji wa huduma kwa watu wenye uhitaji hususani kwa wanawake na vijana. Mfuko huu umejumuisha misaada ya hisani na ina tumia teknolojia ya simu za mkononi kutatua matatizo ya kijamii.
Katika kufanya kazi na mashirika yasio ya kiserikali na washirika, Vodacom Tanzania Foundation imeweza kusaidia miradi 120 mpaka sasa na imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 15 kuboresha maisha ya watanzania.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali tembelea:
https://vodacom.co.tz/en/vodacom_foundation_aboutus/?SID=1u5nsmti8ahqks35k9tds71652
No comments:
Post a Comment