Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhe. Dkt. Akinwumi Adesina ameipongeza Tanzania kwa ukuaji mzuri wa uchumi wa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na hivyo kuendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi kubwa Duniani.
Mhe. Dkt. Adesina ametoa pongezi hizo tarehe 15 Mei, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu ushirikiano kati ya benki hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Dkt. Adesina amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake njema na msimamo wake wa kuwapigania Watanzania na amemtaka kuendelea na mwelekeo huo ambao umeendelea kuimarisha uchumi kwa ukuaji wa wastani wa asilimia 7 ikilinganishwa na wastani wa ukuaji wa uchumi wa dunia wa asilimia 3.5.
Halikadhalika amempongeza kwa ushirikiano na nchi jirani kama vile Uganda na hivyo kufanikisha ujenzi wa mradi mkubwa wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilometa 1,443 kati ya Hoima nchini Uganda na bandari ya Tanga nchini Tanzania kwa kushirikisha sekta binafsi.
Aidha, Mhe. Dkt. Adesina amesema wamezungumzia kuhusu kilimo na kwamba AfDB ipo tayari kusaidia kutatua tatizo la masoko ya mazao yanayozalishwa katika kanda mbalimbali za Tanzania na kuongeza thamani.
Kuhusu miradi mingine ya maendeleo amesema kwa hivi sasa AfDB imetoa ufadhili kwa miradi yenye thamani ya shilingi Trilioni 4.55 na kwamba hivi karibuni benki hiyo imeidhinisha ufadhili kwa miradi ya ujenzi wa barabara za mzunguko (ring road) za Jiji la Dodoma zenye urefu wa kilometa 110, ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato Mkoani Dodoma, na pia ameipongeza Tanzania kwa kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kutumia fedha zake na ameahidi kuwa benki hiyo itaunga mkono mradi huo hasa kwa ujenzi wa kuanzia Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda na hivyo kunufaisha nchi nyingine za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Dkt. Adesina kwa ushirikiano mkubwa ambao AfDB inautoa kwa Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itahakikishia fedha zinazotolewa na benki hiyo zinatekeleza miradi iliyokusudiwa kwa uhakika na inaleta matokeo yanayotarajiwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na miradi hiyo AfDB pia imekubali kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya Mpanda – Tabora yenye urefu wa kilometa 359, kujenga awamu ya pili ya mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kati ya Kariakoo na Mbagala Jijini Dar es Salaam na kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kati ya Sumbawanga – Mpanda – Kigoma – Nyakanazi.
Kuhusu AfDB kusaidia ujenzi wa reli ya kati kwa kipande cha kuanzia Isaka mpaka Kigali Mhe. Rais Magufuli amesema ufadhili huo utasaidia kuharakisha usafirishaji wa madini yaliyopo katika kanda ya kati na magharibi mwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment