Akizungumza katika hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya mkopo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema mkopo huo ni mahususi kwa ajili ya kuiwezesha TTCL kusimika mitambo mipya na ya kisasa kuboresha huduma zake kwa kujenga na kusambaza huduma za Mitandao ya 3G na 4G LTE nchini kote.
Dk. Kazaura alisema hatua hiyo ni habari njema kwa Watanzania, hasa wateja na wadau wa huduma za kampuni ya TTCL. “…TTCL inaishukuru sana Benki ya TIB kwa kutuamini na kukubali kushirikiana nasi baada ya kujiridhisha kuwa tunao uwezo na nia thabiti ya kufanya mageuzi makubwa ya kibiashara ili kuboresha huduma zetu,” alisema Dk. Kazaura akizungumza.
“Kupatikana kwa mkopo na dhamana hizi kutapunguza tatizo la ukosefu wa fedha lililokuwa linatukabili na sasa tutaweza kutekeleza kwa kasi mpango wetu wa mageuzi ya Ki biashara ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu, kuleta mitambo na vifaa vya kisasa vitakavyoongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa na TTCL kwa Wateja wa ndani na nje ya nchi. Natoa wito kwa Watanzania na Wateja wetu wote kwa ujumla waendelee kutegemea huduma na bidhaa zenye viwango vya juu kabisa vya ubora, uhakika na gharama nafuu kutoka TTCL.” Amesema Dk. Kazaura.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Jaffer Machano amesema katika kutimiza wajibu wa TIB kama benki ya maendeleo, ujenzi wa miundombinu umepewa kipaumbele na hii ni pamoja na miundombinu ya sekta ya Mawasiliano.
“Kama alivyosema Dk. Kazaura, lengo la mpango mzima ni kuwapatia Dola milioni 329 na TIB ipo tayari kuhakikisha mradi huu unafanikiwa kwa kushirikisha kampuni zote za TIB group. Mfano mzuri ni mradi huu wa kwanza ambao umefanywa na kampuni tanzu ya TIB group- TIB Corporate Bank, amesema Jaffer Machano.”
Baadhi ya huduma za TTCL zitakazoimarika baada ya uwezeshaji huu ni pamoja huduma za simu na intaneti yenye kasi kubwa inayowezesha huduma za kijamii kufanyika kwa urahisi kwa njia ya mtandao. Huduma kama vile za Elimu kwa njia ya mtandao (E education), Afya kwa njia ya mtandao (E health) na huduma katika Sekta nyingine za kiuchumi kama vile Biashara, Viwanda na Kilimo nazo zitanufaika sana ambapo wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali watapata Mawasiliano ya uhakika katika kufanikisha shughuli zao.
Kampuni ya Simu Tanzania TTCL ipo mbioni kuanzisha huduma ya kusafirisha fedha kwa njia ya Mtandao ifikapo robo ya pili ya mwaka huu ili kutekeleza ombi la muda mrefu la Wateja wake wanaohitaji sana kuanzishwa kwa huduma hii kutokana na Mtandao mpana wa Kampuni uliosambaa ndani na nje ya nchi na unafuu wa gharama.
Michuzi Blog
No comments:
Post a Comment