Pia makubaliano hayo yatasaidia kutekeleza tafiti na bunifu zinazozalishwa na wahitimu na wataalam wa NM-AIST, kwa lengo la kutatua changamoto katika jamii na kuleta suluhisho la kiteknolojia, hasa katika sekta ya kifedha, ujasiriamali na ajira.

Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Afisa Mkuu wa rasilimali watu wa benki ya NMB, Emmanuel Akonaay amekishukuru chuo cha NM-AIST kwa kukubali mashirikiano hayo na kusema kuwa makubaliano hayo ni muendelezo taasisi hizo katika kukuza sekta ya elimu na ubunifu sambamba na maswala ya teknolojia.
“Lengo letu hapa ni kukuza teknolojia zinazohamasisha ujasiriamali, utatuzi wa changamoto mbalimbali katika sekta ya fedha lakini pia kuzalisha ajira kwa vijana katika kuajiriwa au kujiajiri, ndio maana tunaegemea zaidi katika kuendeleza Vipaji katika Teknolojia za Kidijitali na kusaidia kutekeleza tafiti na ubunifu” amesema.
Nae Makamu Mkuu wa chuo cha NM-AIST Profesa Maulilio Kipanyula ameishukuru Benki ya NMB kwa kujitokeza kusaidia wanafunzi na wahitimu chuoni hapo na kusema kuwa italeta chachu kubwa katika sekta ya elimu hasa kwa vijana wenye vipaji vya ubunifu katika Nyanja ya teknolojia na Tehama.
“Taasisi yetu ambayo imejikita kwenye kutoa mafunzo katika ngazi ya uzamili na uzamivu na mafunzo baada ya ngazi ya uzamivu, tumejikita zaidi kwenye maswala ya utafiti na ubunifu, na Ili kutimiza malengo hayo tunahitaji kufanya kazi na wadau ili kuleta tija ya elimu yetu ndio maana tunasema tena asante kwa benki ya NMB,” amesema.
Amesema sehemu ya makubaliano waliyosaini ni namna ambavyo watashirikiana kuendeleza vipaji katika eneo la teknolojia za kidigitali itakayojumuisha kutambua vipaji, kuyatamia na kuviendeleza na jinsi ya kutumia NMB kama sehemu ya Chuo kufanya mafunzo kwa vitendo.
“Tunalenga vijana wajue teknolojia na ubunifu ni fursa ndio maana tunaangalia namna ya kuwa na mchango katika kuzalisha ajira mpya kupitia eneo la teknolojia”.
Mmoja wa wanafunzi katika chuo hicho, Erica Kimei amesema kuwa changamoto kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu ni uwezeshaji wa kufanya tafiti yenye tija.
“Pia unaweza kujitoa kufanya utafiti mzuri lakini kutokana na ukata wa fedha ikaishia kwenye makabrasha, hivyo tunaomba taasisi za elimu ya juu na kifedha ziendeleze mashirikiano kama haya ili kukuza bunifu, teknolojia na vumbuzi mbalimbali za kitafiti,” amesema.
No comments:
Post a Comment