Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa taasisi yake imekuwa ikitekeleza Program ya Imbeju inayotoa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake.
Kwa kushirikiana na wabia, Tully amesema kilimo kinapewa msisitizo zaidi kwa kutambua mchango wake katika kuliingizia taifa fedha za kigeni, kutoa ajira kwa Watanzania pamoja na kuihakikishia Tanzania usalama wa chakula.
Tangu kuanzishwa kwake, SUGECO huwapeleka nje ya nchi wahitimu wa SUA hasa katika mataifa ya Ulaya, Amerika na Asia ambako hujifunza namna nzuri ya kufanya kilimo chenye tija lakini mchakato huo huhitaji fedha za awali kumwezesha mhitimu husika kujiandaa ipasavyo.
Kwa mwaka huu wa kwanza, Tully amesema wanatarajia kuwawezesha zaidi ya wahitimu 2,500 kwa kati ya dola 3,500 za Marekani (shilingi milioni 8.7) mpaka dola 4,500 (shilingi milioni 11.29) zinazotosha kwa mahitaji yao yanayojumuisha gharama za pasi ya kusafiria, visa pamoja na fedha ya kujikimu kabla ya kuanza kulipwa huko waendako.
“Mpango wa uwezeshaji baada ya mafunzo pia umeshaandaliwa kwa kushirikiana na SUGECO pamoja na USAID kwa kutenga maeneo maalum ya kuwekeza katika kilimo cha kisasa, na chenye tija zaidi. Taasisi yetu imejipanga kikamilifu pia katika hatua hiyo ya pili ya uwezeshaji kwa kutoa mitaji wezeshi, pamoja kuwapa mafunzo ya ujasirimali,” amesisitiza Tully.
“Ushirikiano huu, tunaamini utakuwa na tija kubwa kwani ili ufanye biashara endelevu ni muhimu kuwekeza kwa watu unaowahudumia. Mkataba huu ni kati ya uwekezaji mkubwa kwa Benki ya CRDB kwani si wahitimu peke yao watakaonufaika bali wafanyakazi wao, familia hata ndugu, jamaa na marafiki zao,” amesema Kimario.
“Kwa kuwa sisi tunawahudumia zaidi vijana na wanawake, tuliona CRDB Bank Foundation wenye Program ya Imbeju ni wabia muhimu wa kufikisha malengo yetu kwa jamii,” amesema Dkt Anna.
No comments:
Post a Comment