Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameliambia Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwamba utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali unaathiriwa na hali mbaya ya hewa inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambapo kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kinaelekezwa kukabiliana na athari za mafuriko yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kufuatia mvua za el nino zinazoendelea kunyesha.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika kikao na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Willie Nakunyada, kando ya mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoendelea jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Alisema kuwa wakati wa utekelezaji wa Bajeti inayoendelea ya mwaka 2023/2024 mabadiliko ya tabianchi yameathiri mtiririko wa utoaji wa fedha kwenda kwenye miradi ambayo ingesaidia kwa kiasi kikubwa kuchachua shughuli za kiuchumi badala yake zinatumika kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko ikiwemo madaraja, barabara, na miundombinu mingine ya huduma za jamii.
Alitoa wito kwa washirika wa Maendeleo likiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kusaidia namna ya kusaidia bajeti ya Serikali ili kukabiliana na majanga hayo pamoja na kufanikisha mipango ya Serikali ya kuimarisha uchumi wake na kuhudumia wananchi.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika ambapo alisema mwaka huu 2024 unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.4 pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei ukue kwa wastani wa asilimia 3.0 licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza duniani ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, UVIKO-19, mizozo ya kisiasa na vita vinavyoendelea sehemu mbalimbali duniani.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa AfG1, Bw. Willie Ndakunyada ametoa pole kwa Serikali kufuatia madhara ya mvua yanayotokea kutokana na athari za mabadiliko hayo ya tabianchi.
Aidha, ameishauri Serikali kufanya tathmini ya kina ya athari iliyosababishwa na mafuriko na kuishirikisha IMF chini ya mpango wa ECF ili ione namna ya kusaidia utekelezaji wa bajeti ya serikali katika kutatua changamoto hizo.
Katika kikao hicho tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania ilijadiliwa pamoja na utekelezaji wa program ya IMF chini ya mpango wa "Extended Credit Facility-(ECF)" inayofanikisha utekelezaji wa Sera za kiuchumi na upatikanaji wa mikopo nafuu kwa nchi kutoka kwa wahisani wa maendeleo.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Bw. Mcha Hassan Mcha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF AfG1 Bw. Dickson Lema, na Viongozi waandamizi wa Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment