Dar es Salaam. Benki ya Ecobank imesaini makubaliano na Kampuni ya
Kimataifa ya Kuhudumia Shehena za Kontena Bandarini (Ticts) ili kurahisisha
ulipiaji wa mizigo kwa watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Hatua hiyo imeelezwa itaongeza
ufanisi na kuwavutia watu wengi zaidi kutumia bandari hiyo kwa kuwa mizigo
itatolewa kwa haraka zaidi.
Akizungumza leo, Julai 11 wakati wa
kusaini makubaliano hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Ecobank, Raphael Benedict amesema
hatua hiyo itapunguza muda wa kupata kibali kwa kuwa hakutakuwa na usumbufu.
Katika huduma hiyo, mteja wa Ticts
anaweza kulipia mizigo au makontena akiwa nje ya nchi kupitia matawi
zaidi ya 36 duniani.
"Tumeangalia ni changamoto
zipi zinawapata wateja na kuja na suluhisho la kujenga mfumo ili wateja waweze
kufanya malipo yao kwa urahisi zaidi," amesema Benedict.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ticts
nchini, Jered Zerbe amesema huduma hiyo ni muhimu kwa kuwa itapunguza gharama
za kutuma fedha na itaboresha mazingira ya biashara.
Amsema pia itaongeza ufanisi katika
kulipia kodi ya mizigo inayoingia nchini.
Meneja Malipo wa Ecobank, Isaac
Kamuta amesema mbali na kurahisisha malipo hatua hiyo itawaondolea gharama
zisizo za lazima zitokanazo na kuchelewa kutoa mizigo bandarini.
Kwa sasa huduma hiyo itafanyika
kupitia matawi ya benki hiyo lakini itapanua wigo zaidi ili kuwezesha kutumia
simu.
"Hii itarahisisha katika
uboreshaji wa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam. Mtu akiagiza mzigo akiwa
Congo, analipia invoice (stakabadhi ya malipo) na zitaonekana Ticts,"
amesema.
No comments:
Post a Comment