Dar es Salaam – Vodacom Tanzania Foundation imeendelea kuimarisha juhudi zake za kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia za kifedha, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuchangia maendeleo endelevu ya jamii nchini.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika banda la Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha makundi hayo yanapata maarifa na nyenzo zitakazowawezesha kukuza biashara zao.
Sandra alisema kupitia ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania Foundation, CEO Roundtable na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC), taasisi hiyo inatekeleza mradi wa Thinking Equal, Leading Smart (TELS) unaolenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara wadogo katika usimamizi wa biashara, uongozi na matumizi ya teknolojia za kifedha.
Alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa mradi huo, zaidi ya washiriki 800 wamepatiwa mafunzo kuhusu uongozi wa biashara, matumizi ya huduma za fedha kidijitali kama M-Pesa na M-Koba, pamoja na mbinu za kupata fursa za kifedha na mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Kwa mujibu wa Sandra, Vodacom Tanzania Foundation kwa ujumla imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wanawake 500,000 kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi zinazolenga kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Aidha, alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mazingira ya sera yanayochochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs), hatua inayolenga kuwajengea wafanyabiashara mazingira bora ya kufanikiwa.
Akizungumzia awamu ya kwanza ya mafunzo ya TELS yaliyofanyika jijini Dodoma, Sandra alisema vijana walipatiwa elimu kuhusu misingi ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara na matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashara zao na kuwasaidia kuzifikisha katika hatua nyingine ya ukuaji.
Katika kuhitimisha hafla hiyo, Sandra Oswald alikabidhi vocha mbili zenye thamani ya Shilingi 500,000 kila moja kwa washindi wa mashindano ya TELS Biashara Kiosk, Fatma Omar Kibwana na Fadhila Athumani Mgumia. Washindi hao watatumia fedha hizo kama mtaji wa kuendeleza na kukuza biashara zao.
Mpango wa TELS unaendelea kuwa sehemu ya juhudi za Vodacom Tanzania Foundation za kutumia ubunifu, teknolojia na ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, huku ukichangia kujenga jamii yenye uwezo mkubwa wa kushiriki katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment