Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Tuesday, 7 July 2026

NMB YAIMARISHA UFADHILI WA KILIMO, YALENGA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO

Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, akizungumza na Theresia Mbilinyi kuhusu huduma na suluhisho za kifedha kwa sekta ya kilimo katika Banda la NMB kwenye Maonesho ya SabaSaba jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam – Benki ya NMB imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini kwa kuwasilisha suluhisho mbalimbali za kifedha zinazolenga kuwawezesha wadau wote wa mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia wakulima, wanunuzi wa mazao, wachakataji, wasafirishaji hadi waagizaji wa pembejeo.

Akizungumza katika Banda la NMB kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB, Christopher Mwalugenge, alisema benki hiyo imejikita katika kutoa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wadau wa sekta ya kilimo ili kuongeza tija, thamani ya mazao na ukuaji wa biashara.

Alisema NMB hutoa mikopo inayowawezesha wanunuzi wa mazao kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuyachakata na kuyafikisha kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi, hatua inayosaidia kuongeza thamani ya mazao pamoja na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Kwa mujibu wa Mwalugenge, huduma hizo zina umuhimu mkubwa hasa katika kipindi cha mavuno ya mazao ya biashara kama kahawa, tumbaku, ufuta na pamba, ambapo mahitaji ya mtaji kwa wanunuzi na wafanyabiashara huongezeka kwa kiwango kikubwa.

Alifafanua kuwa Benki ya NMB huandaa mikopo hiyo kulingana na aina ya biashara ya mteja, mahitaji yake ya kifedha na mzunguko wa mapato, ili kuhakikisha suluhisho zinazotolewa zinaendana na shughuli halisi za kila mteja.

Aidha, alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao, kupanua fursa za masoko kwa wakulima na kuchochea uwekezaji katika shughuli za uchakataji wa mazao.

Mwalugenge alisisitiza kuwa sekta ya kilimo inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania na chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo NMB itaendelea kubuni na kuboresha huduma za kifedha zinazochangia maendeleo ya sekta hiyo.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, Benki ya NMB inaendelea kuonesha dhamira yake ya kuwa mshirika wa maendeleo kwa sekta ya kilimo, kwa kuwezesha upatikanaji wa mitaji na suluhisho za kifedha zinazochochea ukuaji wa biashara za kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya Tanzania.






No comments:

Post a Comment