DAR ES SALAAM, Oktoba 5, 2026: Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi Mwezi wa Huduma kwa Wateja 2026 kwa kusisitiza dhamira yake ya kwenda hatua ya ziada katika kuwafikia wateja kwenye maeneo yao ya biashara na shughuli za kiuchumi, kusikiliza mahitaji yao na kutumia mrejesho huo kuboresha huduma na suluhisho za kifedha.
Mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu “Extra Mile – Hatua ya Ziada,” inayolenga kuakisi dhamira ya NBC ya kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za kawaida kwa kuelewa mahitaji ya wateja, kufuatilia changamoto hadi zinapatiwa ufumbuzi na kuendelea kubuni huduma zinazorahisisha maisha na biashara zao.
| Mkurugenzi wa Biashara wa NBC, Bw. Jacob Kashimba (kushoto), akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mwezi wa Huduma kwa Wateja wa NBC, iliyofanyika jijini Dar es Salaam. |
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NBC, Bi. Alelio Lowassa, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Theobald Sabi, alisema Extra Mile si kaulimbiu ya mwezi mmoja, bali ni sehemu ya utamaduni wa huduma ambao NBC inalenga kuutekeleza kila siku.
“Kwetu NBC, Extra Mile si kaulimbiu ya mwezi mmoja. Ni namna tunavyotaka kuwahudumia wateja wetu kila siku. Ni kusikiliza na kuelewa hitaji la mteja, kufuatilia jambo hadi lipatiwe ufumbuzi, kuheshimu muda wa mteja, kutimiza ahadi zetu na kuendelea kubuni huduma zinazorahisisha maisha na biashara za wateja wetu,” alisema.
Bi. Lowassa alisema NBC imeamua kuendesha maadhimisho hayo kwa mwezi mzima ili kupata muda zaidi wa kusikiliza wateja, kujifunza na kuboresha huduma, huku ikiendelea kuwekeza katika teknolojia na kupanua mtandao wa huduma ili kukidhi matarajio ya wateja wanaohitaji huduma zenye kasi, usalama na urahisi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, NBC imefungua wastani wa matawi matano mapya kila mwaka, huku mtandao wa NBC Wakala ukifikia zaidi ya mawakala 26,000 nchini.
Aidha, benki hiyo imeendelea kuboresha huduma zake za kidijitali, ikiwemo NBC Kiganjani, NBC Connect, GePG na NBC Lipa Namba, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa mikopo, ikiwemo mikopo ya muda mfupi ya hadi siku 30 kupitia NBC Kiganjani.
“Lengo ni moja: kupunguza muda na hatua anazotumia mteja kupata huduma. Hii ndiyo maana ya ahadi yetu ya Daima Karibu Nawe,” alisema.
Wateja Watoa Maoni Kuhusu Huduma za NBC
Hafla hiyo pia ilihusisha mjadala maalum wa jopo uliowakutanisha wateja wa NBC pamoja na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali, waliopata fursa ya kujadili uzoefu wao na mchango wa huduma za kifedha katika kukuza shughuli za kiuchumi.
Akizungumza kwenye mjadala huo, Mkuu wa Idara ya Bima wa NBC, Bw. Benjamin Nkaka, alieleza kuridhishwa na ongezeko la makundi mbalimbali ya jamii, wakiwemo wakulima, kutumia huduma za bima, ikiwemo bima ya afya na kilimo.
Alisema ongezeko hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarika kwa elimu kuhusu umuhimu wa bima pamoja na utayari wa jamii kukabiliana na hatari zinazoweza kuathiri shughuli zao za uzalishaji.
“Zaidi kwa sasa tunaelekea kwenye mvua za El Niño na Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamewekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari, hususani kwenye maeneo ya miundombinu na mahitaji mengine muhimu ikiwemo chakula.
“Sisi wadau wa bima tunaunga mkono jitihada hizo kwa kuwahamasisha wananchi wawekeze pia kwenye bima ili waweze kupata ulinzi wa mali zao pindi watakapokumbana na athari za mvua hizo, ili kulinda mitaji, mazao, mifugo na biashara zao,” alisisitiza.
NBC Yapongezwa kwa Kuwafikia Wateja
Akizungumza kwa niaba ya wateja wengine wa benki hiyo, mfanyabiashara na mteja wa muda mrefu wa NBC, Bw. Assaa Simba Haroun, aliipongeza benki hiyo kwa hatua ya kuwafikia wateja katika maeneo yao.
Alisema wafanyabiashara wanahitaji uangalizi na ushauri wa karibu kutoka kwa taasisi za fedha ili kuwawezesha kuendesha biashara zao kwa ufanisi na kulinda mitaji yao.
“Hatua hii ya NBC kuwatembelea wateja wake inakwenda kuondoa changamoto ya muda mrefu inayowakabili wafanyabiashara wengi ambao baada ya kukopeshwa tu, taasisi za fedha huwa zinawaacha bila uangalizi wowote hadi pale mambo yanapokwenda kombo.
“Tunawapongeza sana NBC kwa mkakati huu muhimu unaolenga kuwalea wafanyabiashara wasiwe wapweke dhidi ya changamoto zinazowakabili,” alisema.
NBC Yasisitiza Huduma za Kidijitali
Akifafanua zaidi kuhusu maadhimisho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa NBC, Bi. Salama Mussa, aliwashukuru wateja kwa muitikio wao kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
Aliwataka wafanyakazi wa NBC kutumia maadhimisho hayo kama fursa ya kuwafikia wateja katika maeneo yao, kutatua changamoto za kihuduma na kuendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali.
Alisema matumizi ya huduma hizo yataendelea kuwa muhimu katika kuwawezesha wateja kupata huduma za kifedha kwa kasi, usalama na urahisi zaidi.
Kwa NBC, ujumbe wa Extra Mile – Hatua ya Ziada unaenda sambamba na dhamira ya benki hiyo ya kujenga uhusiano wa karibu zaidi na wateja, kuelewa mahitaji yao na kuhakikisha huduma za kifedha zinaendana na uhalisia wa maisha na shughuli zao za kiuchumi.
NBC – Daima Karibu Nawe.
FUATILIA KITOMARI BANKING & FINANCE BLOG
Kwa habari zaidi kuhusu benki, fedha, biashara, uchumi, uwekezaji na sekta mbalimbali nchini Tanzania, endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog.



No comments:
Post a Comment