Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_170926_270926

Absa Banner_170926_270926

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Wednesday, 30 September 2026

NBC YAZINDUA MSIMU WA TANO WA NBC SHAMBANI, DC TANDAHIMBA ASISITIZA WAKULIMA KUWEKA AKIBA

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Mstaafu Michael Mtenjele (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa msimu wa tano wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde, Tunakuona Mbali Mkulima” katika mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Uzinduzi huo ulifanyika Mtwara na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na viongozi waandamizi wa NBC. Wengine ni viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na viongozi waandamizi wa NBC.
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Mstaafu Michael Mtenjele (katikati), akimpongeza Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke (kulia), wakati wa hafla ya uzinduzi wa msimu wa tano wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde, Tunakuona Mbali Mkulima”. Kushoto ni Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza.

MTWARA, Septemba 29, 2026 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua msimu wa tano wa kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde, Tunakuona Mbali Mkulima” katika mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ikiwa na lengo la kuimarisha elimu ya fedha, matumizi ya huduma rasmi za kifedha na kuongeza tija katika kilimo, hususan zao la korosho.

Uzinduzi huo ulifanyika Mtwara na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Mstaafu Michael Mtenjele, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa vyama vya ushirika, wakulima na viongozi waandamizi wa NBC, akiwemo Mkurugenzi wa Wateja Wadogo, Elibariki Masuke; Mkuu wa Masoko, David Raymond; Meneja wa Kanda ya Pwani, Zubeider Haroun; na Mkuu wa Kitengo cha Wakulima, Raymond Urassa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Mstaafu Mtenjele aliipongeza NBC kwa kuwawezesha wakulima kupitia huduma za kifedha na elimu ya fedha, akisisitiza kuwa utamaduni wa kuweka akiba ni muhimu kwa maendeleo ya mkulima, familia na uchumi wa taifa.

“Wakulima wanapaswa kuwa na utamaduni wa kuweka akiba. Akiba si kwa manufaa ya mkulima na familia yake pekee, bali pia ina mchango katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Mtenjele.

Alisema huduma kama bima ya afya zina umuhimu mkubwa kwa wakulima kwa kuwa kipato chao kinategemea misimu ya uzalishaji, huku elimu ya fedha ikiwa muhimu katika kuwawezesha kupanga matumizi, kununua pembejeo na kuwekeza katika shughuli zao.

NBC Yaendelea Kuwekeza kwa Wakulima

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo wa NBC, Elibariki Masuke, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki kuitikia ajenda ya Serikali ya 10/30, inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Kilimo ni biashara, na kwa kutambua hilo tunaendelea kubuni bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya mkulima ili kumwezesha kuongeza uzalishaji, kusimamia mapato yake na kuwekeza zaidi katika shughuli za kilimo,” alisema Masuke.

Alisema NBC imeendelea kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wakulima, ikiwemo akaunti za NBC Shambani zisizo na makato ya kila mwezi, bima ya mazao na afya, huduma za uwakala na kidigitali, mikopo ya pembejeo, mikopo ya matrekta na malori kwa AMCOS, ujenzi wa maghala pamoja na malipo ya awali kupitia stakabadhi ghalani.

Masuke alisema kampeni hiyo imeleta mabadiliko katika matumizi ya huduma rasmi za kifedha mkoani Mtwara, akibainisha kuwa wakulima wengi sasa wanaweka fedha zao benki, wanatumia huduma za kidigitali na kujiunga na bima za mazao na afya.

“Tunajivunia kuona fedha za wakulima sasa zikitulia benki, huku wengi wakianza kutumia huduma za kidigitali na kuchukua bima za mazao na afya. Haya ndiyo mabadiliko tuliyokusudia kuyafikia kupitia kampeni hizi,” alisema.

Zawadi kwa Wakulima na Vyama vya Ushirika

Kivutio kikubwa cha msimu huu ni mfumo wa zawadi unaowahusisha wakulima mmoja mmoja, AMCOS na Vyama Vikuu vya Ushirika (Unions).

Wakulima mmoja mmoja watapata nafasi ya kujishindia baiskeli na pikipiki, AMCOS zikiwania mashine za kufungia mifuko, huku Vyama Vikuu vya Ushirika vikishindania magari mawili aina ya double cabin pickup.

Ili kushiriki, wakulima, AMCOS na Vyama Vikuu vya Ushirika wanatakiwa kufungua akaunti ya NBC Shambani na kupitisha fedha zao kupitia akaunti hizo, huku zawadi zikitolewa kila mwezi.

Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi-Mtwara (MAMCU), Biadia Matipa, aliipongeza NBC kwa kurejesha thamani kwa wakulima kupitia kampeni hiyo, akisema MAMCU imejipanga kushiriki kikamilifu na kuwania zawadi kuu ya gari la double cabin.

“Tumejipanga kuhakikisha tunanufaika na zawadi hizi, na nina uhakika zawadi hii kuu ya gari la double cabin itakuja MAMCU,” alisema Matipa.

Naye Mwenyekiti wa RUNALI na KCJE Ltd, Odas Mpunga, alisema kampeni hiyo imeongeza uelewa wa wakulima kuhusu huduma za kifedha kupitia mawakala wanaowafikia moja kwa moja vijijini.

“Bima ya afya ni muhimu kwa mkulima kwa sababu afya ndiyo inayomwezesha kufanya kazi kwa ufanisi. Pia mashine za kushonea mifuko zitatusaidia sana AMCOS katika shughuli za kuhifadhi korosho,” alisema Mpunga.

Huduma za Benki Karibu na Mkulima

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wakulima wa NBC, Raymond Urassa, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu bima, mikopo, huduma za mawakala na huduma za kidigitali, huku akiwataka wakulima kutumia huduma hizo badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika matawi ya benki.

“Tunataka mkulima aweze kupata huduma za benki akiwa karibu na shughuli zake za uzalishaji. Matumizi ya mawakala na huduma za kidigitali yanamsaidia kuokoa muda na gharama za kusafiri kwenda kwenye matawi,” alisema Urassa.

Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, alisema kampeni hiyo itasaidia kuongeza ushiriki wa wakulima katika mfumo rasmi wa kifedha na kuimarisha ushirika.

“Kampeni hii ni fursa nzuri ya kuwashawishi wakulima zaidi kuingia kwenye huduma rasmi za kibenki na kuimarisha ushiriki wao katika vyama vya ushirika,” alisema Nsunza.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Mstaafu Michael Mtenjele (ndani ya gari), akipima ubora wa gari aina ya double cabin pickup itakayotolewa na benki ya Taifa ya biashara (NBC) kama zawadi kwa washindi wa kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde, Tunakuona Mbali Mkulima” katika mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Wakulima wa NBC, Raymond Urassa (kushoto).
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wakulima wa NBC, Raymond Urassa (pichani) alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza uelewa kuhusu bima, mikopo, huduma za mawakala na huduma za kidigitali, akiwataka wakulima kutumia huduma hizo badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika matawi ya benki.



No comments:

Post a Comment