Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 11 June 2026

AIRTEL AFRICA YAZIDI KUPUNGUZA PENGO LA KIDIGITALI NA KUCHOCHEA UTUNZAJI WA MAZINGIRA KUPITIA NISHATI SAFI


London, Juni 10, 2026: Airtel Africa Plc (“Airtel Africa”), kampuni inayoongoza katika utoaji wa huduma za mawasiliano na huduma za kifedha kwa njia ya simu katika nchi 14 barani Afrika ikiwemo Tanzania, imechapisha Ripoti yake ya Maendeleo ya 2026, inayobainisha mafanikio yaliyopatikana katika kupanua huduma za mawasiliano, kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kuchochea maendeleo endelevu katika jamii inazohudumia kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26.

Ripoti hiyo inaonesha jinsi uwekezaji wa Airtel Africa katika miundombinu ya kidijitali, huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, pamoja na ushirikiano wa kimkakati, ulivyoendelea kubadilisha maisha ya watu na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa jamii ambazo bado hazijafikiwa kikamilifu na huduma hizo, hususan katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha, ripoti hiyo inaeleza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Airtel Africa katika matumizi ya nishati mbadala, pamoja na mbinu zake za kuendesha biashara kwa kuzingatia uwajibikaji, uhifadhi wa mazingira na uwazi katika utoaji wa taarifa za maendeleo kwa wadau wake.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Sunil Taldar, alisema:

"Barani Afrika, upatikanaji wa mawasiliano, huduma za kifedha na elimu ya kidijitali unazidi kuwa muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi. Airtel Africa inaendelea kupanua huduma hizi kwa mamilioni ya watu, hususan katika maeneo ya vijijini na yale ambayo bado hayajafikiwa kikamilifu."

“Katika mwaka huu, tumeendelea kupanua huduma za mtandao, kuongeza matumizi ya simu janja na kuimarisha huduma za Airtel Money, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimkakati unaochangia mafanikio ya shughuli zetu. Maendeleo haya yameendelea kuwa sehemu muhimu ya mkakati wetu wa kukuza biashara na kutoa huduma bora kwa wateja. Aidha, kwa kuboresha matumizi ya nishati na kupunguza utegemezi wa dizeli, tunaimarisha ufanisi na ustahimilivu wa shughuli zetu, huku tukichangia ukuaji endelevu wa biashara na jamii.”

Vigezo muhimu vya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) kwa Mwaka 2025/26

1. Kupanua Mawasiliano na Kupunguza Pengo la Kidijitali

  • Watu wanaofikiwa na mtandao wa simu umefikia asilimia 81.9, kutoka asilimia 81.2 mwaka 2024/25.
  • Upatikanaji wa huduma za mtandao katika maeneo ya vijijini umeongezeka hadi asilimia 73.1, kutoka asilimia 72.2 mwaka uliotangulia.
  • Idadi ya wateja wanaotumia huduma za data umeongezeka hadi asilimia 45.9, kutoka asilimia 44.2.
  • Matumizi ya simu janja yaliongezeka hadi asilimia 49.5, kutoka asilimia 44.8, hatua inayowezesha watu wengi zaidi kupata huduma za mtandao na majukwaa ya kidijitali.
  • Thamani ya miamala iliyofanyika kupitia programu ya My Airtel imefikia dola za Marekani bilioni 8.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 80 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku watumiaji hai wa kila mwezi wakifikia milioni 10.5.
2. Kuimarisha Ujumuishaji wa Kifedha na Ushiriki wa Kiuchumi

  • Idadi ya wateja wa Airtel Money imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni 54, kutoka milioni 44.6 mwaka 2024/25.
  • Asilimia 44.1 ya wateja wa Airtel Money ni wanawake.
  • Thamani ya miamala iliyochakatwa kupitia Airtel Money ni takribani dola za Marekani bilioni 196, kutoka dola bilioni 136 mwaka uliopita.
3. Kusaidia Elimu, Ujuzi na Fursa za Ajira

  • Mtandao wa mawakala wa Airtel Money uliongezeka na kufikia mawakala milioni 2.4, kutoka milioni 1.7 mwaka 2024/25, hatua inayochangia ujasiriamali, ajira na upatikanaji wa huduma za kifedha.
  • Uwiano wa wanawake katika nguvu kazi ya Airtel Africa uliongezeka hadi asilimia 29.9, kutoka asilimia 29.2 mwaka uliopita.
  • Kufikia Machi 31, 2026, jumla ya shule 3,043 zilikuwa zimeunganishwa na huduma za intaneti bila malipo kupitia ushirikiano kati ya Airtel Africa Foundation na UNICEF, kutoka shule 2,176 mwaka 2024/25.
4. Kupunguza Athari za Mazingira Zinazotokana na Shughuli za Kampuni

  • Zaidi ya maeneo 950 ya miundombinu ya kampuni yalibadilishwa kutoka matumizi ya nishati isiyounganishwa na gridi ya taifa kwenda kwenye umeme wa gridi ya taifa, kutoka maeneo 500 mwaka uliopita.
  • Matumizi ya dizeli yalipunguzwa kwa lita milioni 9.1 katika kipindi cha mwaka mmoja.
  • Asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa zilirejelewa (recycled), ikilinganishwa na asilimia93 mwaka 2024/25.

Ripoti ya Maendeleo ya 2026 imeandaliwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Global Reporting Initiative (GRI) pamoja na miongozo ya sekta ya mawasiliano ya simu ya GSMA.

Kuhusu Airtel Africa

Airtel Africa ni mtoa huduma wa mawasiliano na huduma za fedha kwa njia ya simu anayehudumia zaidi ya wateja milioni 183.5 katika nchi 14 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kampuni inalenga kuendeleza ujumuishi wa kidijitali na kifedha kwa kuwafungulia wananchi fursa za maendeleo na kuboresha maisha yao kupitia huduma za mawasiliano na teknolojia.

No comments:

Post a Comment