Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 11 June 2026

KAMPENI YA “NBC SHAMBANI” YAWAFIKIA WAKULIMA WA MKONGE, WAVUVI NA WAFUGAJI TANGA

Afisa Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Bw. Alexander Mhando (katikati), akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” inayoratibiwa na Benki ya NBC kwa lengo la kuongeza tija, uzalishaji na ujumuishaji wa kifedha kwa wakulima wa mazao ya kimkakati, ikiwemo mkonge. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Bw. Saddy Kambona (wa tatu kulia), Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa NBC, Bw. Msafiri Shayo (wa tatu kushoto), Meneja wa NBC Tawi la Tanga, Bw. Moses Mng’ong’o (kulia), Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Tanga (TARECU), Bi. Rehema Mohamed (wa pili kulia), Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, Bw. Emmanuel Constantine (wa kwanza kushoto), na Mjumbe wa Bodi ya Mkonge, Bw. Shedrack Lugendo (wa pili kushoto).

Korogwe, Tanga; Juni 10, 2026 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi kampeni yake ya “Wekeza NBC Shambani Ushinde” mkoani Tanga, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa wakulima, wafugaji na wavuvi katika huduma rasmi za kifedha, sambamba na kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo, hususan zao la mkonge ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati kwa uchumi wa taifa.

Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika jana wilayani Korogwe na kuongozwa na Afisa Tarafa ya Mombo, Bw. Alexander Mhando, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Korogwe. Hafla hiyo iliwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi, wakiwemo viongozi wa Bodi ya Mkonge wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Bw. Saddy Kambona, pamoja na viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika.

Uongozi wa NBC katika hafla hiyo uliwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa benki hiyo, Bw. Msafiri Shayo, pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima, Bw. Raymond Urassa, wakiongozana na maofisa wengine wa benki hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Mhando aliipongeza NBC kwa kuanzisha kampeni hiyo, akisema inaenda sambamba na jitihada za Serikali za kuongeza uzalishaji wa mazao ya kimkakati, kuboresha kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya vijijini.

Alisema Serikali tayari imeweka mazingira wezeshi ya kukuza sekta ya mkonge kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo ugawaji wa miche zaidi ya milioni sita ya mkonge kwa wakulima kupitia Bodi ya Mkonge, uboreshaji wa viwanda vya uchakataji pamoja na kuimarisha miundombinu inayounga mkono mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo kupitia Wizara husika na diplomasia ya uchumi inayoendelezwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Jitihada hizi zimechangia kupatikana kwa masoko mapya ya kimataifa, ikiwemo kuongezeka kwa mahitaji ya zao la mkonge kutoka nje ya nchi, jambo linaloimarisha uhakika wa soko kwa wakulima wetu,” alisema Bw. Mhando.

Aliongeza kuwa juhudi za kufufua mashamba ya mkonge yaliyokuwa yameachwa pamoja na kuyagawa kwa wakulima zimeanza kuleta matokeo chanya katika kuongeza uzalishaji na ajira mkoani Tanga.

Bw. Mhando aliwahimiza wakulima, wafugaji na wavuvi kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia kampeni hiyo, ikiwemo akaunti maalum za NBC Shambani zisizo na makato ya kila mwezi, mikopo ya pembejeo na zana za uzalishaji, elimu ya fedha pamoja na huduma za bima ya afya na mazao.

Napenda kuwahimiza wananchi kutumia kikamilifu huduma za bima ya mazao na bima ya afya zinazotolewa kupitia kampeni hii. Vilevile, fursa za mikopo kwa ajili ya ununuzi wa zana na vifaa vya kisasa vya uzalishaji zitasaidia kuongeza tija na ushindani katika sekta hizi muhimu za uchumi,” alisema.

Aidha, aliipongeza NBC kwa kutangaza nia ya kuwezesha upatikanaji wa takribani Shilingi bilioni 4 kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kisasa za uchakataji wa mkonge (Korona), hatua itakayoongeza thamani ya zao hilo na kuboresha mapato ya wadau wake.

Akifafanua kuhusu kampeni hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa NBC, Bw. Msafiri Shayo, alisema benki hiyo inaendelea kubuni suluhisho za kifedha zinazolenga kuunga mkono azma ya Serikali ya kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa na kuongeza ukuaji wake kufikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2030.

Alisema NBC imeendelea kuwekeza katika huduma za kifedha zinazojumuisha elimu ya fedha, mifumo ya kidijitali, mikopo inayokidhi mahitaji ya wakulima pamoja na huduma za bima zinazosaidia kupunguza athari za vihatarishi vinavyoikabili sekta ya kilimo.

Katika kipindi cha miezi minne ya kampeni hii, wakulima binafsi pamoja na vikundi na vyama vya ushirika watapata fursa ya kushiriki na kushinda zawadi mbalimbali zikiwemo pikipiki na kompyuta mpakato (laptops), zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 35,” alisema Bw. Shayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa NBC, Bw. Raymond Urassa, alisema kampeni hiyo pia inalenga kuhamasisha wakulima kutumia huduma rasmi za kifedha kwa kuhifadhi fedha zao benki, hatua itakayowawezesha kujenga historia ya kifedha na kurahisisha upatikanaji wa mikopo na huduma nyingine za maendeleo.

Tunawakaribisha wakulima, wafugaji na wavuvi kufungua akaunti za NBC Shambani ili waweze kunufaika na huduma zote zinazotolewa kupitia kampeni hii, ikiwemo mikopo, bima, elimu ya fedha na zawadi mbalimbali,” alisema.

Baadhi ya wakulima walioshiriki uzinduzi huo walieleza matumaini yao kuwa kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha, kuboresha upatikanaji wa mitaji na kuimarisha ustawi wa kaya nyingi zinazotegemea sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.

No comments:

Post a Comment