Na Mwandishi Wetu
Kampuni inayoshughulika na masuala ya teknolojia iliyoanzishwa na Watanzania 'EMOTEC', imebuni mfumo wenye uwezo wa kumtambua mtu mwenye homa kali, ndani ya muda mfupi.
Homa kali ni miongoni mwa dalili za mtu aliyeathirika na Ugonjwa wa COVID-19, unaosababishwa na Virusi vya Corona.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa teknolojia hiyo, tarehe 7 Aprili 2020 jijini Dar es Salaam, Moses Hella, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, amesema mfumo huo unafanya kazi pindi unapowekwa katika kamera.
Hella amesema kamera yenye mfumo huo, ina uwezo wa kutambua watu wengi wenye homa kali, ndani ya muda mfupi. Ambapo hutambua joto la mtu mmoja, ndani ya sekunde chache.
"Sasa hivi mtu anawekea kipimo karibu sana kitendo cha hatari. Kutokana na hilo tumewaletea kamera hizi ambazo zinaweza kutambua joto la mtu, kutoka umbali wa kutosha. Kamera ionyesha mfano yule mwenye nguo fulani ana joto lisilo la kawaida.
Inaweza kumtambua kila mmoja kwa sekunde, na kutambua watu wengi kwa wakati mmoja," amesema Hella.
Hella amesema EMOTEC imeamua kuvumbua teknolojia hiyo, ili kuunga juhudi dhidi ya mapambano ya kudhibiti ueneaji wa virusi hivyo.
"Hizi camera zinaweza kuwa mbali mita 1.5, wakati vile vifaa vya kupima, mtumishi huwa karibu zaidi, lazima umsogelee zaidi mhusika. Ni hatari zaidi," amesema Hella.
Hella amesema kamera hizo zinauzwa kulingana na ubora wake, ambapo kima cha chini, kamera moja inauzwa kuanzia Sh. 1 milioni.
"Zipo kamera za kushika mkononi zenye uwezo wa kutambua umbali mrefu na za kufunga. mara nyingi kamera hizi zinatumika maeneo yenye mkusanyiko," amesema Hella.
Wakati huo huo, Hella amesema kampuni yake imebuni kamera kwa ajili ya ulinzi wa nyumba, barabarani na kwenye sehemu za biashara.
Amesema kamera hizo zina uwezo wa kutoa taarifa pindi linapotokea tatizo katika maeneo zilipofungwa.
Amesema mmiliki wa kamera hizo ana uwezo wa kuzungumza na mgeni aliyeko nje, huku yeye akiwa ndani.
"Kwa wafanyabaishara, umeajiri watu tunakupa kifaa cha kufungua milango. Ambacho hakitumii nyilwa 'password'. Kwa kuzingatia changamto hii tumebuni kifaa kinachofungua kulingana na sura ya mtu. Ambaye imeorodheshwa katika kifaa hicho.
Pia, tunawafungia kamera ambazo zina uwezo mkubwa zaidi ya nyumbani. Zina uwezo wa kutambua kitu fulani kimeingia na kutoka. Zina uwezo wa kutambua kama ni gari au mtu. Kama ni kiumbe kisicho na athari haiwezi piga kelele," amesema Hella.
Amesema mmiliki wa kamera hizo ana uwezo wa kufahamu kila kinachojiri hata akiwa mbali na nyumbani kwake.
"Kwa kutumia kamera hii, mtu akiingia kwenye mpaka wako ulioweka kwenye mfumo huo, inakuanbia mtu kaingia, na unaweza kuamuru kamera ipige kelele na kupelekea mtu kukimbia.
Chochote kinachoingia ndani ya eneo lako kamera inapiga kelele," amesema Hella.
Amesema kamera hizo zimeboreshwa kiasi kwamba zinaonyesha picha vizuri hata wakati wa usiku.
"Kamera tumeziboresha kiasi kwamba, usiku unaona clear na ukisafiri mikoani, unaangalia mubashara 'live' kinachoendelea. Tumeshusha gharama kwa sababu inarekodi pale ambapo tukio linatokea," ameeleza Hella.
No comments:
Post a Comment