Dar es Salaam – Vodacom Tanzania imeendelea kudhihirisha ukaribu wake na wateja kwa kuendeleza zoezi la kugawa makapu ya zawadi za sikukuu, ikiwa ni sehemu ya kampeni maalum ya kuwashukuru wateja wake huku ikiadhimisha miaka 25 ya kuwahudumia Watanzania.
Zoezi hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, ambapo wateja mbalimbali walipokea makapu ya vyakula kama ishara ya shukrani na kuthamini mchango wao kwa kampuni hiyo katika kipindi cha miaka mingi.
Akizungumza wakati wa utoaji wa zawadi hizo, Meneja wa Vodacom Kariakoo, Charles Makola, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya utamaduni wa Vodacom wa kusherehekea msimu wa sikukuu pamoja na wateja wake kila mwaka.
“Katika msimu huu wa sikukuu, tumeamua kuwapa wateja wetu makapu ya vyakula kama ishara ya kuwashukuru kwa kuendelea kuwa nasi. Ni utamaduni wetu kila mwisho wa mwaka kuwathamini wateja wetu, lakini mwaka huu tumekuwa na utofauti kwa kuwapatia makapu yaliyojaa vyakula muhimu,” alisema Makola.
Aliongeza kuwa makapu hayo yamejaa vyakula mbalimbali ikiwemo mchele, kitoweo na nyama, yakilenga kusaidia wateja kusherehekea sikukuu kwa furaha zaidi.
“Mwaka huu ni wa kipekee kwetu kwani Vodacom Tanzania imetimiza miaka 25 tangu kuanza kuwahudumia wateja wake. Zaidi ya makapu 600 yanagawiwa nchi nzima, na leo tupo hapa katika Soko la Machinga Complex kuwapatia wateja wetu zawadi hizi,” aliongeza.
Mbali na Dar es Salaam, kampeni hiyo pia imefanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Moshi, Mwanza, Dodoma, Morogoro, Mbeya na maeneo mengine nchini, ikionesha dhamira ya Vodacom ya kuwafikia wateja wake kote Tanzania.
Kupitia kampeni hii, Vodacom Tanzania inaendelea kuimarisha uhusiano wake na wateja pamoja na kudumisha nafasi yake kama kampuni inayojali jamii na kuthamini mchango wa wateja wake katika safari yake ya mafanikio.

.jpeg)

No comments:
Post a Comment