Benki ya CRDB imezindua kampeni maalumu ya mifumo ya kidijitali kwa wateja wake ijulikanayo kama ‘POPOTE INATIKI’, inayolenga katika kuwaelimisha wateja na watanzania kwa ujumla juu ya matumizi ya mifumo hiyo katika upatikanaji wa huduma za benki popote pale walipo masaa 24.
Akizungumza juu ya kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa alhamisi iliyopita huku ikienda sambamba na kumtambulisha msanii ‘Harmonize’ kama balozi wa Benki ya CRDB, Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts amesema hadi kufikia mwezi machi mwaka huu 2020 zaidi ya asilimia 80 ya miamala inayofanywa na wateja wa benki hiyo inafanywa kwa njia za kidijitali kupitia mifumo ya SimBanking, SimAccount, Internet Banking, CRDB Wakala na TemboCard kupitia vifaaa vya manunuzi (PoS) na mtandaoni (e-commerce).
“Mwaka jana 2019, tumefanikiwa kuboresha mifumo hii yote ya utoaji huduma kidijitali kwa kiasi kikubwa sana hii ikiwa ni pamoja na kuongeza baadhi ya huduma katika mifumo hii, hivyo basi tumeona ni vyema tukajikita pia katika kutoa elimu kwa wateja,” alisema Dkt. Witts.
Dkt. Witts alisema Benki ya CRDB kupitia mkakati wake wa biashara wa 2018-2022 umejikita zaidi katika kuleta mabadiliko ya kidijitali ilikuendana na mahitaji ya wateja ambayo yamekuwa yakibadilika kila uchwao.
“Kupitia mifumo hii ya kidijitali hamlazimu mteja kufika katika tawi ili kupata huduma, popote pale Ulipo, uwe mjini, kijijini, nyumbani au mtaani, ndani ya nchi au nje ya nchi, muda wa kazi au muda ambao sio wa kazi, masaa 24 tunakuwezesha kufanya miamala yako ya kwa uharaka, unafuu na usalama, na ndio maana tunasema ‘POPOTE INATIKI’,” alisema Dkt. Witts.
Dkt. Witts alisema malengo ya kampeni hiyo ya ‘POPOTE INATIKI’ ni kuona wateja wengi zaidi wakitumia mifumo ya kidijitali jambo litakalo saidia kuongeza ufanisi katika sekta nyengine za maendeleo kwani muda ambao mteja angetumia kwenda benki sasa utatumika katika shughuli za uzalishaji. “Malengo yetu mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu ni kuona zaidi asilimia 90 ya miamala ya wateja inafanyika kupitia mifumo ya kidijitali,” alisema Dkt. Witts.
Dkt. Witts alisema Benki ya CRDB inajivunia mifumo hiyo ya kidijitali kwani imesaidia sana katika kutimiza azma ya Serikali ya kufikisha huduma kwa Watanzania wengi zaidi “Financial Inclusion” hususani wa vijijini ambapo uwekezaji kupitia mfumo wa matawi ungechukua muda mrefu kutokana na gharama za uwekezaji kuwa kubwa.
“Ukitazama kwa upande wa mawakala sasa hivi tuna Zaidi ya CRDB Wakala 14,000 nchi nzima ambao wamefika katika kila kila kijiji, kila tarafa, kila kata,” aliongezea Dkt. Witts huku akibainisha kuwa mbali na kusogeza huduma karibu zaidi na wateja CRDB Wakala pia inasaidia kutoa ajira kwa Watanzania.
Akizungumza juu ya matumizi ya mifumo hii ya kidijitali katika kipindi hiki ambacho taifa linapambana na janga la ugonjwa wa corona, Dkt. Witts alisema Benki hiyo imekuwa ikiwasisitiza wateja wake kutumia mifumo hiyo ambayo hamhitaji mteja kufunga safari kwenda benki.
“Tunashukuru changamoto hii imetukuta tukiwa na mifumo bora zaidi ya kidijitali, haikutulazimu kufanya mabadiliko au maboresho makubwa kwa tayari tuna mifumo imara ya SimBanking, SimAccount, Internet Banking, CRDB Wakala na TemboCard, hivyo tunaendelea kuwasihi wateja kutumia mifumo hii kupata huduma katika kipindi hiki,” alisema Dkt. Witts.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Masoko, Joe Bendera alisema benki hiyo inatambua vijana ndio wamekuwa mstari wa mbele zaidi katika kutumia mifumo ya kidijitali na hiyo ndiyo sababu kubwa benki hiyo imeamua kumtumia msanii kijana ‘Harmonize’ katika kuhamasisha na kueleimisha jamii juu ya matumizi ya mifumo ya upatikanaji huduma kwa njia ya kidijitali ya Benki ya CRDB.
“Tukifanikiwa kuwafikia vijana tutakuwa tumeweza kuifikia jamii yote, Harmonize ni kijana anayejituma na ushawishi mkubwa kwa vijana na hata watu wenye umri mkubwa, ni imani yangu kwa kushirikiana naye tutakwenda kubadilisha mtazamo wa jamii juu ya matumizi ya mifumo ya kidijitali ya benki,” alisema Bendera.
Naye msanii Harmonize aliishikuru sana Benki ya CRDB kwa nafasi ya kuwa balozi wa benki hiyo huku akielezea ni ndoto ya kila msanii wa Tanzania. Harmonize alisema yeye binafsi amekuwa mteja wa Benki ya CRDB kwa muda mrefu na amekuwa akitumia njia mbadala za kupata huduma hususani SimBanking, CRDB Wakala, ATMs na Internet Banking.
“Ni najua vilivyo faida ya kutumia njia hizi kupata huduma, ni njia rahisi, nafuu na salama zaidi kwa mteja. Nitumie fursa hii kuwahamasisha wateja wote kuwa hakuna haja ya kwenda tawini kufanya miamala kwani ukiwa na Benki ya CRDB ‘POPOTE INATIKI’ kupitia SimBanking, SimAccount, Internet Banking, CRDB Wakala na TemboCard,” alisema Harmonize.
No comments:
Post a Comment