Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Monday, 6 July 2026

NMB YARAHISISHA USIMAMIZI WA VIKUNDI KUPITIA NMB KIKUNDI MINI APP

Dar es Salaam – Benki ya NMB imeendelea kuimarisha juhudi zake za kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali kupitia NMB Kikundi Mini App, huduma bunifu iliyopo ndani ya NMB Mkononi Super App, inayorahisisha usimamizi wa vikundi na kuwawezesha wanachama pamoja na viongozi kupata huduma za kifedha kwa usalama, uwazi na ufanisi zaidi.

Huduma hiyo inalenga kupunguza muda na gharama zinazotumika kupata huduma za benki, huku ikiimarisha usalama wa miamala na kurahisisha shughuli za kifedha za vikundi mbalimbali vya kijamii na kiuchumi nchini.

Akizungumza katika Banda la NMB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Kanda wa Huduma za Vikundi na Benki Vijijini wa NMB, Dismas Prosper, alisema ubunifu huo ni sehemu ya mkakati wa benki wa kutumia teknolojia kuwafikishia Watanzania huduma za kifedha kwa urahisi zaidi.

"NMB Kikundi Mini App imebuniwa kuwapa wanachama wa vikundi njia salama, rahisi na yenye uwazi katika kusimamia shughuli zao za kifedha, huku ikipunguza ulazima wa kutembelea matawi ya benki," alisema Prosper.

 

Huduma za Benki Mikononi mwa Wanachama

Kupitia NMB Kikundi Mini App, wanachama wa vikundi wanaweza kufungua akaunti za vikundi kidijitali bila kufika katika tawi la benki. Vilevile, mfumo huo unawawezesha kufanya miamala kwenda benki nyingine pamoja na mitandao ya simu, hivyo kurahisisha shughuli za kifedha popote walipo.

Mbali na hilo, wanachama wanaweza kuweka michango yao moja kwa moja kwenye akaunti ya kikundi. Kila mchango unaowekwa unathibitishwa kwa ujumbe mfupi wa simu (SMS), hatua inayoongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha imani katika usimamizi wa fedha za vikundi.

Kuimarisha Uwazi na Uwajibikaji

Mfumo huo pia unawawezesha wanachama kuona taarifa mbalimbali za kikundi kulingana na mamlaka waliyopewa ndani ya mfumo. Taarifa hizo ni pamoja na hisa za wanachama, idadi na majina ya wanachama wa kikundi, pamoja na taarifa binafsi za kila mwanachama.

Kwa mujibu wa NMB, uwezo huo unarahisisha usimamizi wa vikundi huku ukiongeza uwazi katika maamuzi na matumizi ya fedha.

NMB Yaendelea Kusukuma Mageuzi ya Kidijitali

Prosper alisema uzinduzi na uboreshaji wa NMB Kikundi Mini App ni sehemu ya dhamira ya benki ya kuendelea kuleta suluhisho za kidijitali zinazowawezesha wananchi, hususan vikundi vya kijamii na kiuchumi, kupata huduma za kifedha kwa urahisi, usalama na uwazi zaidi.

Kadri matumizi ya huduma za benki kwa njia ya kidijitali yanavyoendelea kukua nchini, NMB inaendelea kuwekeza katika ubunifu unaorahisisha huduma za kifedha, kuimarisha usimamizi wa fedha za vikundi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi kupitia teknolojia.




No comments:

Post a Comment