Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Wednesday, 3 December 2025

SANLAMALLIANZ IMEWASHUKURU MAWAKALA WAKE KWA MCHANGO MKUBWA KATIKA UKUAJI WA BIMA

Kampuni ya bima ya SanlamAllianz imeendelea kuwapongeza na kuwashukuru mawakala wake nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kukuza biashara ya bima na kuifikisha karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza katika hafla maalum iliyofanyika Novemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Biashara na Mawakala wa SanlamAllianzGeofray Masige, alisema kampuni hiyo inatambua na kuthamini jitihada za mawakala katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kampuni hiyo.

“SanlamAllianz inawashukuru mawakala wake wote kwa mchango mkubwa katika kukuza biashara ya bima nchini. Pia tunachukua nafasi hii kuwatambulisha kwa kina kuhusu muunganiko wetu mpya kati ya Sanlam na Allianz,” alisema Masige.

Muunganiko wa Sanlam na Allianz: Kuunda Jitu Kubwa la Bima Barani Afrika

Masige alieleza kuwa mnamo Septemba 2023, kampuni ya Sanlam, ambayo ni bingwa wa huduma za bima barani Afrika, na Allianz, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya bima duniani, ziliungana kuanzisha kampuni kubwa ya kifedha isiyo ya kibenki barani Afrika iitwayo SanlamAllianz.

Hadi sasa, SanlamAllianz inafanya kazi katika nchi 26 barani Afrika.

“Muungano huu umeunganisha uzoefu wa pamoja wa zaidi ya miaka 200 barani Afrika na duniani. Lengo letu ni kutoa huduma bora zaidi, kuunda bidhaa zinazokidhi matarajio ya wateja, na kujenga jamii yenye ulinzi wa maisha, fedha, mali, na mafanikio endelevu. Hapo ndipo inapotoka kaulimbiu yetu: ‘Ishi kwa Kujiamini – Live with Confidence’.

Kwa utani mwepesi, Masige alibainisha kuwa kaulimbiu hiyo sio ya “old school” kama enzi za Msondo au Sikinde, bali ni ya zama za hadithi kubwa kama James Bond na Titanic.

Mabadiliko ya Chapa na Kuimarika kwa Uwezo wa Uendeshaji

Baada ya uzinduzi wa chapa mpya mwishoni mwa Oktoba 2025, kampuni za Sanlam nchini zimepitia mabadiliko muhimu:

  • Sanlam General Insurance imeungana na Jubilee General Insurance kuunda
    SanlamAllianz General Insurance Tanzania.

  • Sanlam Life Insurance imebadili jina na sasa inajulikana kama
    SanlamAllianz Life Tanzania.

Masige alisema kuwa kazi kubwa ya ndani ya timu ya Tanzania pamoja na SanlamAllianz Group imerahisisha mabadiliko haya na kuongeza uwezo wa kampuni katika kutoa huduma bora zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu za soko la bima nchini:

  • SanlamAllianz Life inaendelea kuongoza katika bima za maisha.
  • SanlamAllianz General inatarajiwa kuwa kampuni inayoongoza katika bima za mali ifikapo mwisho wa mwaka 2025.

“Kupitia muunganiko wetu na Jubilee Allianz, tumepata uwezo mkubwa zaidi wa kuandikisha bima, utaalamu wa kimataifa, na nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha. Wafanyakazi wote wanaendelea na majukumu yao kama kawaida,” alisema.

Nafasi Kubwa kwa Mawakala

Masige alisisitiza kuwa mawakala wana nafasi muhimu katika ukuaji wa kampuni na soko kwa ujumla.

Kwa sasa, SanlamAllianz General Insurance ina zaidi ya mawakala 300 nchi nzima, na inalenga kufikisha mawakala 350 ifikapo mwaka 2026.

“Ninyi ni sehemu muhimu ya familia ya SanlamAllianz. Matukio kama haya yataendelea kufanyika kwenye matawi yetu makubwa ili kila wakala apate nafasi ya kushiriki na kupata mwelekeo mpya wa kampuni,”alibainisha Masige.

Mtandao wa Matawi Nchini

SanlamAllianz ina mtandao wa matawi 11 nchini, ikiwa ni pamoja na:

  • Dar es Salaam (Mbagala, Quality Center, Tegeta)
  • Mwanza
  • Arusha
  • Dodoma
  • Morogoro
  • Mbeya
  • Zanzibar
  • Moshi
  • Tanga

No comments:

Post a Comment