Dar es Salaam, 31 Mei 2025
Benki ya Absa kwa kushirikiana na klabu ya The Runners wamekabidhi msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, hususan kwa ajili ya wodi ya wazazi na dharura. Msaada huu ni sehemu ya jitihada zao za kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua ubora wa huduma za afya nchini, hasa kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Ujumbe wa kuinua afya ya jamii
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Makamu wa Rais wa The Runners, Bw. Godfrey Mwangungulu, alieleza kuwa huu ni mwaka wa sita mfululizo kwa taasisi hiyo kutoa msaada katika kituo hicho.
“Tunaamini kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii yoyote. Kwa hiyo, tunajivunia kushiriki moja kwa moja katika kusaidia huduma za afya, hususan kwa mama wajawazito na wagonjwa wa dharura,” alisema Mwangungulu.
Absa na dhamira ya maendeleo endelevu
Kwa upande wake, Meneja wa Masuala Endelevu na Matukio wa Absa Bank Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi, alieleza kuwa Absa imekuwa mshirika mkuu wa The Runners kupitia mbio za Absa Dar City Marathon, ambazo zimekuwa chachu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia miradi ya afya.
“Sambamba na utoaji wa vifaa hivi tiba, pia tunachangia damu katika mfuko wa taifa. Hii ni sehemu ya dhamira yetu kama chapa – 'Stori yako ina thamani' – ambapo tunalenga kuwa sehemu ya safari za watu katika kupata huduma stahiki za afya na kuokoa maisha,” alisema Lukuvi.
Mchango wenye tija kwa huduma za dharura
Akitoa shukrani kwa niaba ya Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dkt. Linda Mutasa, ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, alibainisha kuwa msaada huo umewafikia kwa wakati muafaka.
.jpeg)
“Huduma za dharura na za akina mama wajawazito huhitaji vifaa tiba vya kutosha na vya kisasa. Msaada huu utasaidia sana kupunguza changamoto tulizokuwa tunakabiliana nazo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” alisema Dkt. Mutasa.
Mbio za hisani zinavyosaidia ustawi wa jamii
Vifaa tiba vilivyokabidhiwa vimenunuliwa kwa fedha zilizopatikana kupitia Absa Dar City Marathon, mbio za hisani zilizolenga kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ya mwili kama njia ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu, kisukari, na magonjwa ya moyo.
Kwa kushirikiana, Absa na The Runners wameonyesha namna taasisi binafsi zinavyoweza kuwa wadau wa maendeleo katika sekta ya afya kupitia ushiriki wa kijamii, uwajibikaji wa kampuni (CSR), na ubunifu wa kuchangisha rasilimali kwa njia endelevu.
No comments:
Post a Comment