Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Friday 5 July 2024

ZAWADI ZA MILIONI 80 KUKABIDHIWA KWA WASHINDI NBC DODOMA MARATHON

Maofisa wa Benki ya NBC akiwemo Meneja Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa benki hiyo Bi. Brendansia Kileo (wa pili kulia), Meneja wa Biashara ya Kadi wa benki hiyo Bi. Esnat Holella (wa pili kushoto) pamoja na wadau wa habari akiwemo Eddo Kumwembe (katikati), Oscar Oscar (kulia) na Adela Tillya (kushoto) wakionesha viwango vya zawadi ya fedha taslimu zitakazotolewa kwa washindi mbalimbali wa msimu wa tano wa mbio za NBC Dodoma Marathon zinazotarajiwa kufanyika Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Dar es Salaam, Julai 4, 2024: Jumla ya washindi 60 wa mbio za NBC Dodoma Marathon msimu huu wanatarajiwa kuondoka na zawadi zenye jumla ya thamani ya sh milioni 82 pamoja na medali, imefahamika.

Mbio hizo zenye hadhi ya kimataifa zinatarajiwa kufanyika Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma zikiwa na lengo la kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.

Hafla ya utambulisho wa zawadi hizo imefanyika jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa kutoka benki ya NBC ambayo ndio inaratibu mbio hizo na wadau wa mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo waandishi wa habari tukio lililoshuhudiwa na maelfu ya watazamaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyokuwa vikionesha mbashara tukio hilo lenye mvuto wa aina yake.

Wakifafanua kuhusu zawadi hizo Meneja Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa benki ya NBC Bi. Brendansia Kileo na Meneja wa Biashara ya Kadi wa benki hiyo Bi. Esnat Holella walisema viwango vya zawadi hizo vimeongezwa zaidi msimu wa mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuongeza hadhi ya mbio hizo kila mwaka.

Zaidi ongezeko hilo la viwango vya zawadi linatwaja kuwa linalenga kuchochea ushiriki zaidi wa wanariadha wengi wakiwemo wa kimataifa, hatua ambayo inalenga kuongeza ushindani zaidi kwa washiriki.

“Hivyo basi taarifa njema kwa washiriki wa NBC Dodoma Marathon mwaka huu ni kwamba pamoja na medali kwa washiriki wote wa mbio hizi, washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Shilingi Milioni 11.5 kila mmoja, shilingi Milioni 5 kwa washindi wa pili, Shilingi Milioni 2.5 kwa washindi wa tatu, Shilingi Milioni 1.5 kwa washindi wanne na Shilingi Milioni 1 kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi kumi nao pia wakiibuka zawadi za na pesa taslimu.’’ Alisema Bi. Kileo.

Kwa upande wa mbio za Kilomita 21, Bi. Kileo alisema pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Shilingi Milioni 5.5 kila mmoja, Shilingi Milioni 2.5 kwa washindi wa pili, Shilingi Milioni 1.25 kwa washindi wa tatu, Shilingi 750,000 kwa washindi wanne na Shilingi 600,000 kwa washindi wa tano huku pia washindi wa sita hadi wa kumi wakiibuka na zawadi za pesa taslimu kila mmoja.

“Mbio za kilomita 10 washindi wa kwanza wanaume na wanawake watajinyakulia Shilingi Milioni 2.5 kila mmoja, Shilingi Milioni 1.5 kwa washindi wa pili, Shilingi 750,000 kwa washindi wa tatu, Shilingi 500,000 kwa washindi wanne na Shilingi 400,000 kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi kumi nao pia wakiibuka zawadi za na pesa taslimu.’’ Aliongeza Bi. Kileo.

Aidha, Bi. Kileo aliongeza kuwa vifaa maalumu vitakavyotumiwa na washiriki wa mbio hizo zikiwemo jezi vinatarajiwa kutolewa kwa washikiri katikati ya mwezi huu huku akiendelea kutoa wito kwa jamii kuendelea kujisajili kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha Shilingi 35,000 kwa usajili wa washiriki mmoja mmoja au Shilingi 25,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu wanaozidi 25 ili kuunga mkono agenda kuu ya mbio hizo.

Kwa upande wake Bi. Holella aliwashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kushiriki maandalizi ya mbio hizo yakiwemo mashirika na kampuni mbali mbali wakiwemo Sanlam Insurance ambao ni wafadhili wakuu wa mbio hizo huku wadau wengine wakiwa ni Jubilee Allianz General Insurance, Wasafi Media, Garda World, Metropolitan, SGA,SBC, Benki za CRDB na NMB, Computech Solutions na Hans-Paul.

“Aidha kupitia ushirikiano wetu na Shirika la Reli Tanzania (TRC) tunatarajia kwamba washiriki zaidi ya 1,000 watasafiri kutoka jijini Dar es Salaam hadi Dodoma na kurudi kwa kutumia treni ya kisasa ya mwendokasi (SGR) ya shirika hilo hatua ambayo inatarajiwa kuongeza radha zaidi ya mbio hizi msimu huu wa tano,’’ alisema.

Utoaji wa zawadi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 80 kwa washindi 60 kuinaifanya mbio hiyo kuwa ndio mbio ya kwanza hapa nchini kutoa kiwango cha zawadi kwa washindi wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment