Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 29 August 2023

RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI SKULI YA MIL. 600 INAYOJENGWA NA NMB



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Skuli ya Maandalizi Tasani, iliyopo Shehia ya Tasani, Makunduchi, inayojengwa na Benki ya NMB, ikitarajia kugharimu Sh. Milioni 600 hadi itakapokamilika Disemba 2023.



Mradi huo umezinduliwa ikiwa sehemu ya Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival 2023), linaloendelea Paje, Mkoa wa Kusini Unguja, visiwani Zanzibar.



Tamasha hilo lililozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Agosti 26 mwaka huu, linafanyika chini ya kauli mbiu 'Tuwalinde Kimaadili Watoto Wetu kwa Maslahi ya Taifa,' na linatumika kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.



Akitoa maelezo ya awali ya mradi huo wa Tasani kwa Rais Samia, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, amesema ujenzi huo ambao ni sehemu ya Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), ni kati ya jitihada za wazi za benki yake katika kumuunga mkono kufanikisha maendeleo ya elimu nchini.



Bi. Zaipuna alimueleza Dkt. Samia kwamba ujenzi huo utakaojumuisha madarasa matano yatakayochukua wanafunzi 200 kwa mkupuo mmoja, utakamilika Disemba mwaka huu, tayari kabisa kwa Mwaka wa Masomo wa 2024, ambao utaanza Januari mwakani, na kwamba Skuli ya Maandalizi Tasani itakuwa ni shule ya kwanza katika eneo hilo, ikiwa ni ya tatu kwa Makunduchi.



"Ujenzi wa majengo na samani za ndani kama vile viti, meza na madawati, utaigharimu Benki ya NMB Shilingi Milioni 600, ambazo ni sehemu ya faida yetu tunayoitoa kila mwaka kurejesha kwa jamii.



"Mradi huu ulio kwenye eneo la mita za mraba 467, utajumuisha madarasa matano yatakayobeba wanafunzi 40 kila moja, Ofisi ya Mwalimu Mkuu, Ofisi ya Walimu, jiko, vyoo vya walimu, wafanyakazi na wanafunzi, stoo, Mifumo ya Kisasa ya Maji Safi na Majitaka, pamoja na sehemu ya michezo.



"Mheshimiwa Rais, mradi wa Skuli hii ni uthibitisho wa utayari wa NMB kusapoti Serikali ya Tanzania katika juhudi zake za kuboresha Elimu nchini.

"Tunatambua jitihada zako katika Sekta ya Elimu, nasi tukiwa wadau na washirika muhimu, tukaona ni vema kuunga mkono maono yako ya Elimu Bure. NMB tunajivunia kuwa washirika vinara wa hilo, tukiamini Skuli ya Maandalizi Tasani inaweza kuibua wasomi watakaokuja kuwa viongozi wakubwa," amebainisha Bi. Zaipuna.

Akizungumza baada ya maelezo hayo, Rais Samia aliishukuru Benki ya NMB kwa namna inavyounga mkono jitihada za Serikali yake na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kuboresha Mazingira ya watoto kupata Elimu, huku akiweka ahadi ya kurudi Tasani Januari mwakani wakati wa kuzindua shule hiyo.

"Tunaishukuru sana Benki ya NMB kwa kuamua kutuunga mkono kwa kufanya hili la Ujenzi wa Skuli hii kwa ajili ya watoto wetu. Nilikuwa hapa mwaka jana kuzindua Ofisi ya Shehia, niko hapa kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi huu na utakapokamilika, nitarudi Januari mwakani kuja kuizindua skuli hii.

"Niwakumbushe Wana Tasani kwamba niliwaahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali na huu ndio muendelezo wa hilo. Sisi ni viongozi wenu, na sio watawala wenu. Tuko kazini kila uchao kutatua kero zenu, jukumu lenu ni kushirikiana na Serikali kwa kuwasikiliza viongozi wa ngazi mbalimbali. NMB watapokamilisha, yatunzeni majengo haya muhimu kwa elimu ya watoto wetu," alimalizia Rais Samia.

No comments:

Post a Comment