Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday 9 February 2022

BENKI YA DCB YAINGIA VISIWANI ZANZIBAR KWA KISHINDO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga akipokea mfuko kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa (kushoto), wakati Mkurugenzi huyo pamoja na ujumbe wake wakitembelea ofisi za Waziri huyo mjini Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha, kutoa taarifa za huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na DCB na pia kujadili fursa za uwekezaji zilizopo visiwani humo. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Rahma Ngassa na nyuma ya mheshimiwa Waziri ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Zanzibar, Arafat A. Haji.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Wazee wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui (katikati) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa pamoja na ujumbe wake walipomtembea ofisini kwake, Zanzibar jana katika mazungumzo ambayo yalilenga katika kuangalia fursa za uwekezaji katika utoaji wa huduma za kibenki visiwani humo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Zanzibar anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga (katikati) akipozi kwa picha ya kumbukumbu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa (wa tatu kushoto), wakati Mkurugenzi huyo pamoja na ujumbe wake wakitembelea ofisi za Waziri huyo mjini Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha, kutoa taarifa za huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na DCB na pia kujadili fursa za uwekezaji zilizopo visiwani humo. Wa tatu Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Rahma Ngassa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (UWAMWIMA), Salum Rehani (kushoto), akizungumza na ujumbe wa Benki ya DCB, ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Godfrey Ndalahwa mjini Zanzibar. Kulia ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, Rahma Ngassa. Mazungumzo ya Mkurugenzi wa DCB yalilenga katika kuangalia fursa za uwekezaji katika utoaji wa huduma za kibenki visiwani humo.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Wazee wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui (katikati) akipiga picha ya kumbukumbu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Godfrey Ndalahwa (wa tatu kushoto) pamoja na ujumbe wake walipomtembea ofisini kwake, Zanzibar katika mazungumzo ambayo pamoja na kujitambulisha yalilenga katika kuangalia fursa za uwekezaji katika utoaji wa huduma za kibenki visiwani humo.

Benki ya Biashara ya DCB imesema imejipanga kufungua tawi la benki visiwani humo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika azma yake ya kukuza uchumi wa visiwa hivyo kwa kupitia ajenda maarufu ya ‘Uchumi wa Buluu’.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa visiwani humo wakati akiendelea na ziara yake ya wiki nzima pamoja na ujumbe wake kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji katika visiwa hivyo.

Alisema DCB imejipanga katika kila idara kusapoti dhana ya Uchumi wa Buluu wa Zanzibar unaojikita katika kipato kinachotokana na rasilimali zipatikanazo baharini katika kuhakikisha inaingiza bidhaa bora za kibenki kwa wananchi wote visiwani humo zinazokidhi mahitaji ya mtu mmoja mmoja na katika makundi yote.

“DCB tumekuja Zanzibar kwa nia ya dhati ya kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuhakikisha Uchumi wa Buluu unakuwa na tija kwa wananchi wa Zanzibar.

“Kuna fursa nyingi zipatikanazo ndani ya Uchumi wa Buluu ambapo sisi kama DCB tumejizatiti katika kutoa huduma za kifedha kuanzia chini kabisa, kwa wajasiriamali wadogowadogo na wa kati, kwa vikundi vya wajasiriamali, wanawake na vijana”, alisema Bwana Ndalahwa.

Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa DCB aliyeongozana na wakuu wa idara za biashara, mauzo, mawasiliano na masoko, Waziri katika Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga alisema wizara yake ipo tayari kushirikiana na DCB pamoja na wawekezaji wengine kwa kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji visiwani humo.

“Tunaikaribisha Benki ya DCB visiwani humu ili kuja kutuongezea kasi yetu ya kuupaisha uchumi wa Zanzibar, sisi kama serikali milango ipo wazi katika kupokea na kushughulikia changamoto zozote mtakazoweza kukutana nazo”, alisema Waziri Soraga.

Naye Waziri wa Afya, aliipongeza Benki ya DCB kwa mikakati yake ilivyojipanga katika kutoa huduma za kifedha kwa wananchi kuanzia kwa wenye vipato vya chini visiwani humo.

“Mmekuja wakati muafaka kuna fursa nyingi mno za kiuwekezaji katika huduma za kibenki, njooni mje kuwakopesha wateja wadogo, njooni muwanyanyue watanzania wa chini”, alisema mheshimiwa waziri.

Aidha Akizungumzia historia fupi ya DCB Bwana Ndalahwa alisema benki imekuwa ikipiga hatua mwaka hadi mwaka tokea ilipoanzishwa Mwaka 2002 ikijulikana kama Benki ya Watu wa Dar es Salaam (Dar es Salaam Community Bank) ikiwa na lengo la kutatua changamoto za mitaji kwa wajasiliamali wadogo wadogo.

Alisema kutoka na mipango thabiti ya uongozi wa DCB pamoja na menejimenti yake, benki iliendelea kukua na kufanya vizuri katika soko hadi mwaka 2012 ilipokidhi vigezo vya benki kuu (BoT) na kupewa leseni ya kuwa benki kamili ya biashara (DCB Commecial Bank) sasa ikiruhusiwa kutoa huduma na kuendesha shughuli zake za kibenki nchini kote.

“Kwa kipindi cha miaka 20 tokea imeanzishwa, DCB imepata mafanikio mengi, DCB imeendelea kukua kifaida mwaka hadi mwaka na kuendelea kutanua mtandao wake wa matawi hadi kufikia nane katika sehemu mbalimbali za Tanzania Bara huku hivi karibuni tukizindua muonekano mpya wa benki yetu.

“Tumeendelea kuboresha huduma zetu za kibenki kwa kupitia huduma za kidigitali pamoja na DCB Wakala ili kuhakikisha hata mahali ambapo hatuna tawi la benki watanzania waweze kufurahia huduma zetu bora za kibenki.

“Huu ni wakati sasa wananchi wa visiwa hivi kufurahia na kunufaika na huduma zetu za kibenki zikiwemo huduma za kibenki kwa njia ya simu za mkononi ya DCB Digital, huduma za mikopo mbalimbali kama mikopo ya ada, mikopo ya waalimu, mikopo ya vikundi vya wajasiriamali, vikundi vya wanawake, vijana na mikopo mingine ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa”, aliongeza Bwana Ndalahwa.

Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine mkurugenzi huyo pamoja na ujumbe wake amekuwa akifanya mikutano pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja wa sekta binafsi.

No comments:

Post a Comment