Foreign Exchange Rates

DStv Advert_010224

DStv Advert_010224

SBT Tanzania Advert_291123

Monday 25 February 2019

TANZANIA NA UFARANSA USHIRIKIANO WAZIDI KUIMARIKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akipokelewa na mwenyeji wake, Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mhe. Jean-Yves Le Drian jijini Paris. Dkt. Mahiga yupo nchini Ufaransa kwa ziara ya siku mbili tarehe 21 na 22 Februari 2019. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mhe. Jean-Yves Le Drian.
Tanzania na Ufaransa zimeahidi kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo; kuongeza uwekezaji na biashara; na kutafuta ufumbuzi wa migogoro inayozikabili nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Ukanda wa Bahari ya Hindi na changamoto nyingine za kiusalama katika maeneo hayo.

Ahadi hiyo ilitolewa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo jijini Paris leo walipokutana kwa ajili ya mazungumzo. Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yupo nchini Ufaransa kwa ziara ya kikazi siku siku mbili 21 na 22 Februari 2019 kufuatia mwaliko wa Waziri wa Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa, Mhe. Jean- Yves Le Drian ambaye ameahidi pia kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania hivi karibuni.

Kabla ya mazungumzo hayo, Mheshimiwa Balozi Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na kundi la Maseneta wa Ufaransa ambao ni marafiki wa Tanzania wakiongozwa na Seneta Ronan Dantec ambaye ni Mwenyekiti wa Maseneta hao. Maseneta hao walipendekeza kuanzishwa kwa ushirikiano dada kati ya jiji la Paris na Dodoma. Ushirikiano huo ujikite zaidi katika matumizi bora ya ardhi, mipango miji na kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile, Maseneta hao wameelezea dhamira yao ya kutaka kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuibua vipaji vya mchezo wa mpira wa miguu katika shule mbalimbali nchini.

Wakati huo huo, Mhe. Mahiga alifanya mazungumzo na Bibi Marie Audouard, Naibu Mshauri wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Afrika. Katika mazungumzo yao, Bibi Audouard aliainisha maeneo ya kipaumbele ya Mhe. Rais Emmanuel Macron katika mahusiano yake na nchi za Afrika. Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuimarisha zaidi mahusiano na nchi zinazoongea lugha ya kiingereza na kireno; kuendelea kushirikiana katika usuluhishi wa migogoro ya kikanda na kimataifa; kuhamasisha sekta binafsi ya Ufaransa kwenda kuwekeza Afrika; na kubadilishana uzoefu katika nyanja za utamaduni hasa kwa vijana.

Viongozi wengine aliofanya nao mazungumzo Mhe. Waziri ni pamoja na Bibi Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO; na Bw. Bertrand Walckenaer, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

Katika mazungumzo na Mkurugenzi wa UNESCO, Waziri Mahiga alilishukuru Shirika hilo kwa kuwa mshirika wa Tanzania kwa miaka mingi kwenye masuala ya elimu, sayansi na utamaduni na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali yanayohusu elimu, sayansi na utamaduni.

Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa AFD, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, kutokana na ushirikiano mzuri uliopo wameongeza mara mbili kiwango cha fedha za maendeleo nchini Tanzania ambazo zitatumika kufadhili miradi katika sekta za uchukuzi, nishati, maji safi na taka, kilimo, afya na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Waziri anahitimisha ziara yake leo kwa kukutana na Jumuiya ya Wawekezaji na wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF) na Bi. Luise Mushikiwabo, Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya nchi zinazozungumza Kifaransa (IOF).

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma.
22 Februari 2019

No comments:

Post a Comment