Dar es Salaam, Mei 12, 2026 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kampeni mpya ijulikanayo kama “Shinda Trip ya Mauritius”, yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kupitia kadi za NBC Visa huku ikiwapa wateja nafasi ya kujishindia safari ya kifahari kwenda visiwa vya Mauritius.
Kampeni hiyo ya miezi mitatu ilizinduliwa rasmi katika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa benki, wafanyakazi, waandishi wa habari pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya huduma za kifedha.
NBC Yaongeza Kasi ya Uchumi Usio wa Fedha Taslimu
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond alisema kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha wateja kutumia zaidi mifumo ya malipo ya kidijitali kwa kufanya manunuzi na miamala mbalimbali kupitia kadi za NBC Visa ndani na nje ya Tanzania.
Alieleza kuwa mpango huo ni sehemu ya dhamira pana ya NBC katika kuendeleza uchumi usiotegemea fedha taslimu pamoja na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kupitia huduma za kisasa, salama na rahisi kutumia.
“Tunalenga kuona wateja wetu wanakumbatia kikamilifu matumizi ya malipo ya kidijitali kwa sababu ni salama zaidi, yanafanyika kwa haraka na ni rahisi zaidi katika maisha ya sasa. Dunia inaelekea katika matumizi ya mifumo janja ya kifedha, na sisi NBC tunataka kuhakikisha wateja wetu wanakuwa sehemu ya safari hiyo,” alisema Raymond.
Namna ya Kushiriki Kampeni
Kupitia kampeni hiyo, kila mteja atakayefanya miamala mitano au zaidi kwa kutumia kadi ya NBC Visa ataingia moja kwa moja kwenye droo ya kila mwezi.
Washindi watakaobahatika watajishindia safari ya gharama zote kulipiwa kwenda Mauritius. Jumla ya washindi watatu wanatarajiwa kupatikana katika kipindi chote cha kampeni, huku kila mshindi akipata nafasi ya kusafiri akiwa ameambatana na mtu mmoja wa chaguo lake.
Safari hiyo ya kifahari inatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Faida za Kutumia Kadi za NBC Visa
Kwa mujibu wa Raymond, mbali na nafasi ya kushinda safari hiyo, watumiaji wa kadi za NBC Visa wanaendelea kufurahia manufaa mbalimbali yanayoendana na matumizi ya malipo ya kidijitali.
Miongoni mwa faida hizo ni pamoja na:
- Kuimarishwa kwa usalama wa fedha
- Urahisi wa kufanya malipo popote duniani
- Malipo ya haraka bila kubeba fedha taslimu
- Uwezo wa kufanya miamala mtandaoni kwa usalama
- Punguzo na ofa maalum kupitia mtandao wa kimataifa wa Visa
Aliongeza kuwa wateja wanaweza kupata punguzo mbalimbali ikiwemo hadi asilimia 40 katika huduma za CIP Lounge, hadi asilimia 20 kwenye hoteli, shopping na vivutio vya utalii jijini Paris, hadi asilimia 15 London pamoja na hadi asilimia 25 nchini Thailand.
Aidha, watumiaji wa kadi ya Platinum Business watanufaika na punguzo la hadi asilimia 50 kwenye safari, hoteli na manunuzi sambamba na huduma za bima na matibabu wanapokuwa nje ya nchi.
NBC Yaendeleza Mageuzi ya Kidijitali
Raymond alisema kampeni hiyo pia inaendana na mkakati wa muda mrefu wa NBC wa kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika sekta ya huduma za kifedha nchini kwa kupanua upatikanaji wa huduma bunifu za kifedha na kuwahamasisha Watanzania wengi zaidi kutumia mifumo rasmi ya kibenki inayotumia teknolojia.
“Kadiri huduma za benki za kidijitali zinavyoendelea kubadilisha taswira ya sekta ya fedha nchini Tanzania na duniani kote, sisi tunaendelea kuwa na dhamira ya kuanzisha suluhisho zinazomlenga mteja ambazo zinarahisisha huduma za kila siku za kibenki huku zikitoa uzoefu wenye manufaa kwa wateja wetu,” alihitimisha.
No comments:
Post a Comment