Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 7 May 2026

EXIM BANK YAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA GEITA KUPITIA MPANGO WA "EXIM CARES"

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba (kulia), akikabidhiwa moja ya vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank Tanzania, Stanley Kafu (kushoto), ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki hiyo kwa jamii kupitia mpango wa Exim Cares.

Geita, Tanzania – Mei 6, 2026 – Exim Bank Tanzania, kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii unaojulikana kama Exim Cares, imeendelea kuimarisha huduma za afya katika Hospitali ya Manispaa ya Geita kwa kutoa msaada unaolenga kuziba mapungufu muhimu katika huduma za afya ya uzazi na dharura, huku ikithibitisha tena dhamira yake ya kuboresha ustawi wa jamii inazozihudumia.

Msaada huo ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo katika uwajibikaji kwa jamii (CSR), unaolenga sekta muhimu zikiwemo afya, elimu, ubunifu, mazingira na uwezeshaji wa kiuchumi. Kupitia nguzo hizo, benki imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali yenye matokeo chanya nchini Tanzania, ikiwemo programu za msaada wa tiba, kampeni za uchangiaji damu, ufadhili wa elimu pamoja na miradi ya uwezeshaji wa jamii inayolenga kuleta maendeleo endelevu.

Hatua hiyo ya kusaidia Hospitali ya Manispaa ya Geita imechochewa na uhitaji uliobainika ndani ya hospitali hiyo, ambapo upungufu wa vifaa muhimu vya tiba umekuwa ukiathiri utoaji wa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hasa kwa wajawazito, watoto njiti pamoja na watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Kupitia msaada huu, Exim Bank inalenga kuongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma bora za afya na kuboresha matokeo ya huduma kwa jamii inayowazunguka.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba, aliipongeza Exim Bank kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha afya ya watoto, hususan watoto njiti na wale wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Pia alieleza kuwa licha ya tawi jipya la benki hiyo Geita kuwa bado katika hatua za mwanzo za shughuli zake, benki imeonyesha moyo mkubwa wa uwajibikaji kwa jamii kwa kuweka mbele mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Exim Bank Tanzania, Stanley Kafu, alisema msaada huo unaonesha namna benki hiyo inavyotekeleza mkakati wake wa kusaidia jamii kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi.

Kupitia Exim Cares, tunahakikisha tunalenga maeneo yanayogusa moja kwa moja maisha ya jamii inayotuzunguka. Hapa Geita, tulizungumza na wadau na kubaini mapungufu mahususi katika huduma za afya ya uzazi na watoto, na msaada huu unalenga kushughulikia changamoto hizo kwa njia itakayosaidia jamii kwa muda mrefu,” alisema.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Hospitali ya Manispaa ya Geita, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dr. Thomas Mauru, alisema msaada huo umefika kwa wakati muafaka na utaongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma bora zaidi.

Msaada huu utaongeza uwezo wetu wa kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususan kwa watoto wanaozaliwa na changamoto mbalimbali za kiafya. Unachangia moja kwa moja kuboresha ubora wa huduma za afya tunazotoa kwa jamii yetu,” alisema.

Hatua hii inaakisi falsafa pana ya Exim Bank ya kuhakikisha ukuaji wa benki unaenda sambamba na maendeleo ya jamii inazozihudumia, kwa kuamini kuwa mafanikio ya taasisi yanapaswa kuendana na mchango wake katika kutatua changamoto za wananchi.

Baada ya shughuli hiyo ya CSR, benki hiyo inatarajiwa pia kuzindua rasmi tawi lake jipya la Geita ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwepo wake katika mkoa huo na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watu binafsi pamoja na wafanyabiashara. Uzinduzi huo unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

Kama sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu, Exim Bank Tanzania inaendelea kuwekeza katika suluhisho na ushirikiano unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha, kuchochea ukuaji wa biashara na kuimarisha mnyororo wa thamani nchini, jambo linaloifanya benki hiyo kuwa si tu taasisi ya kifedha, bali pia mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania.


No comments:

Post a Comment