Mwanga, Kilimanjaro - Nidhamu ya kifedha, utekelezaji madhubuti wa mikakati ya biashara pamoja na ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochochea ukuaji wa Benki ya Mwanga Hakika (MHB).
Benki hiyo imeendelea kuonyesha mafanikio katika utendaji wake wa kifedha baada ya kurekodi faida kabla ya kodi ya Sh18.28 bilioni mwaka 2025, ikilinganishwa na Sh14.6 bilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 25.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Sita wa Wanahisa wa benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mwanga Hakika Bank, Ridhuan Mringo, alisema mafanikio hayo yametokana na ufanisi wa mikakati ya biashara, nidhamu ya kifedha pamoja na ushirikiano mzuri kati ya menejimenti, wafanyakazi na wadau wa benki hiyo.
Alisema benki hiyo itaendelea kuimarisha huduma zake za kifedha na kuongeza ubunifu katika bidhaa zake ili kuendana na mahitaji ya soko na kuongeza ushindani katika sekta ya benki nchini.
“Faida kabla ya kodi ilifikia Sh18.28 bilioni kutoka Sh14.6 bilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 25. Ongezeko hili linaashiria ufanisi katika kuongeza mapato na kudhibiti gharama za uendeshaji,” amesema Mringo.
Aidha, alisema benki hiyo imeendelea kutoa mikopo inayochochea maendeleo ya sekta za uzalishaji huku ikizingatia athari za kimazingira na kijamii katika maamuzi yake ya kifedha.
Katika hatua nyingine, Mringo alisema benki hiyo imeanza utekelezaji wa mpango mkakati mpya wa miaka mitano wa 2026 hadi 2030 wenye lengo la kukuza benki hiyo na kufikia hadhi ya Benki ya Tier One ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye mkutano huo, amana za wateja zimeongezeka hadi kufikia Sh317.5 bilioni mwaka 2025 kutoka Sh214.8 bilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 48.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Chomete Hussein, alisema mwaka 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa benki hiyo kutokana na ukuaji wa faida na kuongezeka kwa imani ya wateja.
“Mwaka 2025 benki imeweza kupata faida kabla ya kodi ya Sh18.2 bilioni, mafanikio makubwa ukilinganisha na Sh14 bilioni mwaka 2024. Benki yetu imekua kwa zaidi ya asilimia 40, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa benki zinazokua kwa kasi nchini,” amesema Hussein.
Aliongeza kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu, benki hiyo imefikia kiwango cha mali cha zaidi ya Sh500 bilioni.
Hussein alisema mafanikio hayo yanatokana na ubunifu wa bidhaa na utoaji wa huduma bora kwa wateja walioendelea kuiamini benki hiyo.
Katika hatua nyingine, viongozi wa benki hiyo wamemkumbuka Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani wa Tanzania, Cleopa David Msuya, wakisema mchango wake uliiwezesha benki hiyo kufikia mafanikio ya sasa.
“Huu ni mwaka wa pili tunafanya mkutano mkuu pasipo uwepo wa Mzee Cleopa Msuya. Tangu benki inaanza hajawahi kukosa mkutano. Alituandaa vizuri kwa maono na miongozo yake, ndiyo maana hata pasipo yeye benki inaendelea kufanya vizuri,” amesema Hussein.
Naye Mkuu wa Idara ya Biashara wa benki hiyo, Thomas Enock, alisema benki imeendelea kusikiliza maoni ya wateja ili kuboresha huduma zake na kuongeza thamani kwa wanahisa.
“Wateja wetu wanahitaji gawio zuri na kuona thamani ya hisa zao inaongezeka. Tumekuwa tukipokea maoni kutoka kwa jamii na kufanya maboresho yatakayotuongezea wateja na kuimarisha huduma za mikopo pamoja na amana za gharama nafuu,” amesema Enock.

No comments:
Post a Comment