DAR ES SALAAM - November 13, 2026: Vodacom Tanzania Foundation imekabidhi rasmi Jengo la Kituo cha Rasilimali za Walimu (Teachers Resource Centre – TRC) katika Shule ya Msingi na Ufundi Mbezi, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, baada ya kulifanyia maboresho makubwa yanayolenga kuimarisha maendeleo ya kitaaluma ya walimu na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
Uzinduzi wa kituo hicho umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ambaye alikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo hicho kilichoboreshwa kwa ufadhili wa Vodacom Tanzania Foundation.
![]() |
| Mkuu wa Idara ya Uendelevu na Ubia wa Vodacom Tanzania Foundation, Pauline Koola, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya Kituo cha Rasilimali za Walimu (TRC) Mbezi, Ubungo. |
Katika makabidhiano hayo, Vodacom Tanzania Foundation pia ilikabidhi vifaa mbalimbali vya kisasa vya TEHAMA na samani kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kituo hicho na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kompyuta 30 za mezani zilizounganishwa na intaneti, vifaa 30 vya akiba ya umeme (UPS), seti 30 za meza na viti, televisheni janja ya inchi 75 pamoja na madawati 90 kwa ajili ya wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Uendelevu na Ubia wa Vodacom Tanzania Foundation, Pauline Koola, alisema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kusaidia kuboresha elimu nchini kwa kuwezesha walimu kupata maarifa, ujuzi na teknolojia zinazohitajika katika mazingira ya elimu yanayobadilika.
Kupitia ushirikiano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) katika programu ya MEWAKA, Vodacom Tanzania Foundation imewezesha zaidi ya walimu 100,000 kupata mafunzo kupitia mfumo wa Learning Management System (LMS) bila gharama za data wanapotumia mtandao wa Vodacom.
Mpango huo unalenga kuwafikia walimu 300,000 nchini kote, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mafunzo endelevu na kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma kwa kutumia teknolojia ya kidijitali.
Maboresho ya kituo hicho cha Mbezi yamehusisha uwekaji wa dari na viyoyozi pamoja na vifaa vya kisasa vinavyolenga kutengeneza mazingira bora ya kujifunzia, kushirikishana maarifa na kufanya mafunzo ya kitaaluma.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Meneja Mauzo wa Vodacom Tanzania eneo la Kibaha, Fadhili Linga, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi, Lois Bawazir Hassani, pamoja na mwakilishi wa Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Ubungo, Hamida Semkuya.
Uwekezaji huo unaonesha mchango wa Vodacom Tanzania Foundation katika kuunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya elimu kupitia uwezeshaji wa walimu, upatikanaji wa teknolojia na uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia.
Kwa kuimarisha vituo vya rasilimali za walimu na kupanua upatikanaji wa mafunzo ya kidijitali, juhudi hizi zinatoa fursa zaidi kwa walimu kujiendeleza na hatimaye kuchangia kuboresha ubora wa elimu nchini Tanzania.





No comments:
Post a Comment