Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Saturday, 14 November 2026

PUMA ENERGY YAINGIZA HUNGRY LION TANZANIA, YAFUNGUA MGAHAWA WAKE WA KWANZA OYSTERBAY

Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi mgahawa wa Hungry Lion katika kituo cha Puma Energy Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Novemba 13, 2026. Ushirikiano huo unaimarisha nafasi ya Puma Energy kama kampuni inayotoa huduma mbalimbali zaidi ya mafuta, huku ukiboresha uzoefu wa wateja, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za ajira nchini.

Wanaoshuhudia uzinduzi huo ni pamoja na Mkuu wa Hungry Lion Tanzania, Gladstone Okumu (wa pili kulia), Katibu wa Pili wa Masuala ya Siasa katika Ubalozi wa Afrika Kusini, Ndumiso Mngadi (wa kwanza kulia), pamoja na viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo.

TANZANIA, 14 Novemba 2026 – Puma Energy Tanzania imezindua rasmi mgahawa wa Hungry Lion katika kituo chake cha huduma cha Oysterbay jijini Dar es Salaam, hatua inayoweka alama ya kuingia kwa chapa hiyo ya migahawa katika soko la Tanzania na Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza.

Ushirikiano huo unalenga kuongeza huduma zinazopatikana katika vituo vya Puma Energy, kuwawezesha wateja kupata huduma za chakula kwa haraka na urahisi wanapotembelea vituo hivyo, huku ukifungua fursa mpya za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.

Tanzania inakuwa nchi ya nne ambayo Hungry Lion inafanya kazi kwa kushirikiana na Puma Energy, baada ya Namibia, Zambia na Botswana. Kampuni hiyo pia ina mpango wa kupanua shughuli zake hadi Zimbabwe na Eswatini mwaka 2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara katika masoko mbalimbali barani Afrika.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema kuanzishwa kwa Hungry Lion katika kituo cha Oysterbay ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kuboresha vituo vyake na kuvifanya kuwa maeneo yanayotoa huduma mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya wateja.

Alisema pamoja na biashara yake kuu ya mafuta, Puma Energy inaendelea kuongeza huduma nyingine ili kurahisisha maisha ya wateja na kuwapatia fursa ya kupata huduma mbalimbali katika eneo moja.

“Biashara yetu kuu ni mafuta, lakini tunatambua kuwa mahitaji ya wateja yanaenda zaidi ya hapo. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika huduma zinazorahisisha maisha yao ya kila siku na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Kuanzishwa kwa Hungry Lion katika kituo chetu cha Oysterbay ni hatua nyingine katika juhudi hizo, kwani sasa wateja wetu wanaweza kupata huduma za chakula wanapotembelea kituo hicho,” alisema Fatma.

Aliongeza kuwa mkakati wa kampuni ni kuendelea kuboresha vituo vyake ili wateja waweze kupata huduma mbalimbali katika eneo moja, zikiwemo za kujaza mafuta, kununua vilainishi vya magari, kufanya manunuzi katika maduka ya Shop Express, kupata huduma za kifedha kupitia ATM na mawakala, pamoja na huduma za chakula kupitia Hungry Lion.

Fatma alisema Puma Energy Tanzania itaendelea kuwekeza katika kupanua na kuboresha mtandao wake wa vituo vya huduma, ambao kwa sasa una zaidi ya vituo 105 vya mafuta nchini.

Mbali na huduma za mafuta, kampuni hiyo pia inaendelea kuwekeza katika suluhisho za nishati mbadala, zikiwemo Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) na Gesi ya Petroli Iliyoyeyushwa (LPG). Pia inaendelea kuboresha miundombinu yake na kuongeza huduma za kidijitali kupitia programu ya Puma PRIS, inayowazawadia wateja wanapotumia bidhaa na huduma zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hungry Lion, Adrian Basson, alisema upanuzi wa biashara ya kampuni hiyo katika masoko mbalimbali barani Afrika unaenda sambamba na dhamira ya kuongeza ajira, kukuza vipaji vya ndani na kuchangia maendeleo ya jamii.

“Ukuaji wa biashara una maana zaidi pale unapozalisha ajira. Ndiyo maana tunazingatia upanuzi endelevu wa biashara yetu. Kila mgahawa mpya tunaofungua unatoa nafasi ya kuajiri watu zaidi, kukuza vipaji vya ndani na kuchangia maendeleo ya jamii tunakofanyia kazi,” alisema Basson.

Alisema kampuni inalenga kujenga biashara imara ya Kiafrika ambayo, pamoja na kuwapatia wateja bidhaa zake, inachangia pia upatikanaji wa fursa za kiuchumi katika maeneo inakofanyia shughuli zake.

“Tanzania ni soko lenye fursa nzuri kwetu na tunafurahi kuanza safari yetu katika Afrika Mashariki kupitia nchi hii. Ushirikiano wetu na Puma Energy unatupa nafasi nzuri ya kukuza biashara yetu, na tunatarajia kuwa sehemu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” alisema.

Uzinduzi wa mgahawa huo unakuja baada ya Puma Energy kufanya maboresho katika kituo chake cha Oysterbay ili kukiandaa kwa ajili ya huduma za Hungry Lion. Uwekezaji huo pia umechangia upatikanaji wa ajira kupitia shughuli za ujenzi na maandalizi ya mgahawa, pamoja na nafasi nyingine zinazotokana na uendeshaji wake.

Hatua hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati kati ya kampuni katika kuvutia uwekezaji, kupanua huduma kwa wateja, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa kuanzishwa kwa Hungry Lion katika kituo cha Puma Energy Oysterbay, wateja sasa wanapata huduma za chakula sambamba na huduma nyingine za nishati, manunuzi na kifedha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kampuni kuendelea kuboresha uzoefu wa wateja nchini.


No comments:

Post a Comment