Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Absa Banner_301026_111126

Stanbic Bank Banner_201026

Saturday, 14 November 2026

WAZIRI DKT. DOROTHY GWAJIMA AWAHIMIZA WASTAAFU KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI NA MIKOPO CRDB

Dar es Salaam, Novemba 13, 2026: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewahimiza wastaafu nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji, mikopo na huduma mbalimbali za kifedha zinazotolewa na Benki ya CRDB ili kuimarisha hali zao za kiuchumi, kuongeza vyanzo vya mapato na kuendelea kutimiza ndoto zao hata baada ya kustaafu kazi.

Akizungumza katika Kongamano la Wastaafu lililoandaliwa na Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, Novemba 13, 2026, Waziri Gwajima aliipongeza Benki hiyo kwa kubuni huduma zinazozingatia mahitaji maalumu ya wastaafu.

Alisema huduma hizo zinaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha ustawi wa wazee na kuwawezesha kuendelea kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa, licha ya kuwa wamemaliza utumishi wao rasmi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa, alisema Benki hiyo kupitia mpango wake wa Swaiba Mstaafu inatoa huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga kuwawezesha wastaafu kuendelea kuwa na maisha yenye ustawi na uhakika wa kiuchumi.

Alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na Akaunti ya Wastaafu isiyokuwa na ada za uendeshaji za kila mwezi na inayojumuisha bima ya maisha, pamoja na Akaunti ya Thamani inayowawezesha wastaafu kuwekeza fedha zao na kupata malipo ya riba kila mwezi.

Aidha, alisema CRDB inatoa mikopo kwa wastaafu ya hadi shilingi milioni 200, yenye muda wa marejesho wa hadi miaka tisa, pamoja na huduma ya Pension Advance inayowawezesha kupata mikopo ya muda mfupi kwa njia ya kidijitali kupitia huduma ya SimBanking.

Kongamano hilo lililofanyika chini ya kaulimbiu “Ndoto Zako Hazistaafu” liliwakutanisha wastaafu, viongozi wa Serikali na wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii kwa lengo la kuwapatia elimu ya fedha, kuwafahamisha fursa mbalimbali za uwekezaji na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi.

Mbali na kutoa elimu na kufungua fursa za kifedha, kongamano hilo pia lilikuwa jukwaa muhimu kwa Benki ya CRDB kusikiliza maoni, matarajio na mahitaji ya wastaafu ili kuendelea kuboresha huduma zake.

Kupitia mpango wa Swaiba Mstaafu, CRDB inalenga kuwa mshirika muhimu wa wastaafu katika safari yao ya maisha baada ya utumishi, ikiwasaidia kutumia vizuri rasilimali walizonazo, kuwekeza, kupata kipato na kuendelea kutimiza malengo yao.

Hatua hiyo inaonesha umuhimu wa huduma za kifedha zinazozingatia makundi mbalimbali ya jamii, hususan wastaafu, ambao bado wana nafasi na uwezo wa kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.

Kwa CRDB, kustaafu kazi si mwisho wa ndoto, bali ni mwanzo wa fursa nyingine za kiuchumi.





No comments:

Post a Comment