Blog Rebranding Teaser_030826

Blog Rebranding Teaser_030826

Stanbic Bank Banner_070826

Stanbic Bank Banner_070826

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

Friday, 28 August 2026

NMB, BUNGE KUWAKUTANISHA ZAIDI YA WASHIRIKI 1,000 MICHEZONI DODOMA

NMB BUNGE BONANZA 2026 KUHAMASISHA AFYA, MSHIKAMANO NA TIJA KAZINI

Dodoma | Agosti 28, 2026

Zaidi ya washiriki 1,000 kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wizara 14 na taasisi 10 wanatarajiwa kushiriki NMB Bunge Bonanza 2026, litakalofanyika Jumamosi, Agosti 29, 2026, jijini Dodoma.

Bonanza hilo limepata udhamini wa NMB Bank Plc wenye thamani ya Shilingi milioni 210, ukiwemo mchango wa vifaa mbalimbali vya michezo kwa ajili ya mashindano hayo.

Mwenyekiti wa Bunge Bonanza na Mbunge wa Makete, Festo Sanga, amesema mwaka huu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amezialika wizara 14 pamoja na taasisi 10 kushiriki bonanza hilo, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya washiriki ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Sanga amesema bonanza hilo litafanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini, jijini Dodoma, ambapo Spika Zungu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya udhamini huo, Mshauri Mwandamizi wa Kitengo cha Biashara za Serikali wa NMB Bank, Vicky Bishubo, amesema NMB inaendelea kuunga mkono michezo kutokana na mchango wake katika kuimarisha afya, kujenga mshikamano na kuongeza tija mahali pa kazi.

“Tunatambua umuhimu wa michezo katika kujenga afya bora, mshikamano na kuongeza tija kazini. Ndiyo maana NMB inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuhamasisha watumishi kushiriki katika michezo na shughuli za kimwili,” amesema Bishubo.

Vifaa vilivyokabidhiwa na NMB kwa ajili ya bonanza hilo ni pamoja na mipira, makombe, track suti za michezo, fulana na medali, pamoja na mahitaji mengine yatakayosaidia kufanikisha mashindano hayo.

Kabla ya kuanza kwa bonanza, wabunge watashiriki katika matembezi yatakayoanzia Chuo cha Mipango saa 12:00 asubuhi, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuhamasisha mazoezi na maisha yenye afya.

Pamoja na ushindani mkali unaotarajiwa kutoka kwa timu za Bunge, wizara, taasisi mbalimbali na NMB, Sanga amesema lengo kuu la bonanza hilo si ushindani pekee bali pia kuhamasisha watumishi kushiriki katika mazoezi, kujenga mshikamano na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Bonanza hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi na kukuza afya bora miongoni mwa watumishi wa umma, huku likitoa fursa ya kujenga mahusiano na ushirikiano zaidi kati ya Bunge, wizara, taasisi mbalimbali na sekta ya benki.

Endelea kufuatilia Kitomari Banking & Finance Blog kwa habari na taarifa mbalimbali kuhusu sekta ya benki, biashara, fedha na uchumi nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment