Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Saturday, 4 July 2026

NMB YASOGEZA HUDUMA ZA BIMA KIDIJITALI KUPITIA UMEBIMA MINI APP

DAR ES SALAAM – Benki ya NMB imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za bima kwa njia ya kidijitali kupitia Umebima Mini App, huduma iliyounganishwa ndani ya programu ya NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kununua bima kwa urahisi, usalama na haraka kupitia simu zao za mkononi.

NMB ilitoa taarifa hiyo wakati wa Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo benki hiyo imeendelea kuonesha ubunifu wa huduma za kifedha zinazochochea uchumi wa kidijitali, sambamba na kauli mbiu ndogo ya maonesho ya mwaka huu, "Biashara za Tanzania Kidijitali Zaidi."

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo, Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martin Massawe, alisema kuwa Umebima Mini App ni sehemu ya mkakati wa benki wa kurahisisha upatikanaji wa huduma za bima kwa Watanzania kupitia teknolojia.

Alieleza kuwa huduma hiyo imeondoa ulazima kwa mteja kufika katika tawi la benki au ofisi za kampuni za bima ili kupata huduma. Badala yake, mteja anaweza kuchagua na kununua bima inayokidhi mahitaji yake popote alipo kupitia programu ya NMB Mkononi.

"Kwa kutumia Umebima Mini App, mchakato wa kupata bima umekuwa rahisi zaidi, salama na wa haraka, hivyo kuwawezesha wateja kupata kinga ya kifedha kwa urahisi kupitia simu zao," alisema Massawe.

Alisisitiza kuwa bima ni nyenzo muhimu ya usalama wa kifedha kwa watu binafsi, familia na biashara, kwani huwasaidia kukabiliana na athari za majanga na matukio yasiyotegemewa ambayo yanaweza kusababisha hasara kubwa za kifedha.

Kwa kutambua mahitaji tofauti ya wateja, NMB imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali za bima zinazolenga makundi mbalimbali ya jamii. Miongoni mwa bidhaa hizo ni Matching Insurance, inayolenga wafanyabiashara wadogo na wamiliki wa biashara ndogo ndogo kwa kuwapatia kinga ya bima kwa gharama nafuu kupitia mfumo wa kidijitali.

Hatua hii inaonesha dhamira ya NMB ya kutumia teknolojia kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza ujumuishaji wa kifedha nchini. Kupitia Umebima Mini App, benki hiyo inaendelea kuwezesha wananchi na wafanyabiashara kupata huduma za bima kwa urahisi zaidi, huku ikichangia juhudi za Tanzania katika kujenga uchumi wa kidijitali unaojumuisha kila mwananchi.

Kadri matumizi ya huduma za kidijitali yanavyozidi kuongezeka nchini, ubunifu kama Umebima Mini App unaonesha nafasi muhimu ya sekta ya benki katika kuleta suluhisho bunifu zinazorahisisha maisha ya wananchi na kuongeza ustahimilivu wa kifedha kwa watu binafsi na biashara.









No comments:

Post a Comment