Dar es Salaam: Benki ya NMB imetangaza udhamini wa Shilingi milioni 150 kwa ajili ya kufanikisha msimu wa nane wa Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup) 2026, yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 6 hadi 17 mwaka huu.
Udhamini huo unaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya NMB na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kuendeleza michezo, kuimarisha afya za washiriki na kukuza mshikamano miongoni mwa wanajeshi.
Mashindano ya mwaka huu yatahusisha michezo 13 mbalimbali, yakishirikisha timu kutoka Kamandi ya Makao Makuu ya JWTZ, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Kamandi ya Jeshi la Akiba pamoja na Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Akizungumza kuhusu udhamini huo, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Aikansia Muro, alisema benki hiyo inaamini michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga afya bora, nidhamu, ushirikiano na umoja katika jamii.
Alisema kupitia udhamini huo, NMB inalenga kuendelea kuunga mkono juhudi za JWTZ za kukuza vipaji vya michezo, kuimarisha ushindani wa kirafiki na kujenga mshikamano miongoni mwa washiriki kutoka vikosi mbalimbali vya jeshi.
“Mashindano haya yanatoa fursa muhimu ya kuimarisha afya ya mwili na akili, kukuza vipaji vya wanamichezo pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya washiriki kutoka kamandi tofauti,” alisema Muro.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 6 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, na kushirikisha mamia ya wanamichezo wa JWTZ kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mbali na kutoa burudani na ushindani wa hali ya juu, CDF Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji vya michezo ndani ya majeshi, huku ikichangia kuimarisha utimamu wa mwili, afya ya akili na mshikamano miongoni mwa wanajeshi.
Udhamini wa NMB unaonesha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo nchini na kusaidia programu zinazochangia ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment