DAR ES SALAAM: Benki ya DCB imezindua kampeni maalum ya miezi sita ijulikanayo kama "Tuma Bure, Shinda Kila Wiki", inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali na kuongeza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini kwa kuwapatia wateja nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali huku wakifanya miamala bila kutozwa gharama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Sabasaba Moshingi, amesema benki hiyo imefanya maboresho makubwa ya huduma zake za kidijitali baada ya kubaini kuwa wateja wengi wanahitaji huduma za haraka, salama, nafuu na zinazopatikana muda wote. Amesema kupitia mfumo mpya wa DCB Pesa App, wateja wanaweza kufungua akaunti popote walipo nchini na kufanya miamala mbalimbali bila makato.
Moshingi amesema kampeni hiyo pia inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma rasmi za kifedha, huku akiwahimiza Watanzania kutumia huduma za benki ili kukuza biashara zao na kufikia malengo ya kiuchumi kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko wa DCB, Geofrey Magugi, amesema mteja anayefungua akaunti kupitia DCB Pesa App na kufanya angalau muamala mmoja ataingia kwenye droo ya kila wiki yenye zawadi ya Shilingi 100,000 kwa washindi 10,amesema wateja watakaofanya miamala zaidi ya mitatu kwa mwezi watapata nafasi ya kushinda zawadi kubwa zaidi ikiwemo Shilingi milioni moja kila mwezi.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Ramadhani Mganga, amesema kampeni hiyo itadumu hadi Desemba mwaka huu na inalenga kuwazawadia wateja wanaotumia huduma za benki kwa njia za kidijitali, amesema DCB imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi za fedha zinazoweka kipaumbele katika ubunifu wa huduma nafuu, huku ikitoa fursa kwa Watanzania kufungua akaunti na kufanya miamala kutoka mahali popote nchini bila kulazimika kutembelea matawi ya benki.
Mganga amesema pamoja na faida ya kutuma fedha bila makato, wateja watakaoshiriki kampeni hiyo watakuwa na nafasi ya kushinda zawadi za kila wiki, kila mwezi na zawadi kubwa itakayotolewa mwishoni mwa kampeni mwezi Desemba, akiwataka Watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa kufungua akaunti za DCB na kutumia huduma zake za kidijitali.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment