Foreign Exchange Rates

Absa Loan Campaign_160426

Absa Loan Campaign_160426

CRDB Bank Advert_070325

Wednesday, 20 May 2026

NBC YAZINDUA RASMI MSIMU WA SABA WA NBC DODOMA MARATHON, YALENGA WASHIRIKI ZAIDI YA 15,000

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (pichani), akiongoza zoezi la uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon uliofanyika jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zitafanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma na zinatarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 15,000, huku zikilenga kuchangisha fedha za kusaidia mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya selimundu (sickle cell).
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto), akiongoza mbio za majaribio sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benjamin Mkapa Hospital, Prof. Abel Makubi (kulia), pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge (wa pili kulia), wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam, Mei 19, 2026 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon zinazotarajiwa kufanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma, huku waandaaji wakijipanga kuweka rekodi mpya kwa kuvutia zaidi ya washiriki 15,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Baada ya mafanikio makubwa ya msimu uliopita uliovutia zaidi ya washiriki 12,000, NBC Dodoma Marathon inaendelea kujidhihirisha kama moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo nchini yenye athari chanya katika afya, jamii na maendeleo ya watu.

Marathon Inayobeba Matumaini na Kuokoa Maisha

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema msimu huu umebeba dhamira kubwa zaidi ya kugusa maisha ya Watanzania kupitia nguvu ya michezo.

Tunapoendelea kuikuza NBC Dodoma Marathon, tunataka kuona mbio hizi zikibaki kuwa zaidi ya mashindano ya riadha. Hii ni mbio ya matumaini, mbio ya afya na mbio ya kuokoa maisha,” alisema Sabi.

 

Alieleza kuwa fedha zitakazokusanywa mwaka huu zitaelekezwa katika kusaidia mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, kugharamia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na kuimarisha huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu.

Uzinduzi huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Jakaya Kikwete Cardiac Institute, Benjamin Mkapa Hospital, Benjamin Mkapa Foundation, wadhamini pamoja na wafanyakazi wa NBC.

Mbio Zitakazoshirikisha Maelfu ya Wakimbiaji

Kama ilivyozoeleka, washiriki wa NBC Dodoma Marathon mwaka huu watapata nafasi ya kushiriki katika mbio za:

  • Kilomita 5
  • Kilomita 10
  • Nusu Marathon (KM 21)
  • Marathon Kamili (KM 42)

Waandaaji wanaamini mbio hizo zitavuta ushindani mkubwa kutoka kwa wakimbiaji wa ndani pamoja na wa kimataifa.

Zaidi ya TZS Bilioni 1.5 Zimekusanywa Katika Miaka Sita

Kwa mujibu wa Sabi, tangu kuanzishwa kwa NBC Dodoma Marathon miaka sita iliyopita, mbio hizo zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zilizosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya nchini.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya fedha hizo zimeelekezwa kwenye mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kupitia ushirikiano na Ocean Road Cancer Institute, ambapo zaidi ya wanawake 200,000 wamefanyiwa uchunguzi wa afya huku wengine wakipata matibabu yaliyosaidia kupona.

Tangu mwaka 2023 tumefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 400 zilizowezesha ufadhili wa masomo ya diploma kwa wakunga 200 kupitia ushirikiano wetu na Benjamin Mkapa Foundation,” alisema Sabi.

Aliongeza kuwa NBC pia imetenga:

  • TZS milioni 200 kusaidia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo kupitia JKCI
  • TZS milioni 200 kusaidia huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye selimundu kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa

JKCI: Watoto Zaidi ya 1,500 Wanasubiri Upasuaji wa Moyo

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa JKCI, Dr. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo kwa sasa ina zaidi ya watoto 1,500 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo.

Kwa mujibu wake, gharama za matibabu hayo zinafikia kati ya shilingi milioni 4 hadi 8 kwa kila mtoto.

NBC Dodoma Marathon imeongeza matumaini kwa familia nyingi zenye watoto wenye changamoto za moyo. Mchango huu utasaidia ununuzi wa vifaa tiba na kuongeza uwezo wa utoaji huduma za matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa mbali na kusaidia matibabu, marathon hiyo imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

Hospitali ya Benjamin Mkapa Yaeleza Mafanikio ya Huduma za Upandikizaji Uloto

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi alisema gharama za huduma za upandikizaji wa uloto kwa mtoto mmoja mwenye selimundu zinaweza kufikia shilingi milioni 200.

Alisema hadi sasa watoto 30 tayari wamefanyiwa huduma hiyo na kupona, huku hospitali hiyo ikilenga kuongeza idadi ya watoto wanaopatiwa matibabu hayo kila mwaka.

Tunaamini NBC Dodoma Marathon itaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha matumaini kwa watoto hawa na familia zao,” alisema Prof. Makubi.

BMF Yafanikisha Mafunzo kwa Wakunga na Wauguzi 200

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benjamin Mkapa Foundation, Dr. Ellen Mkondya-Senkoro alisema ushirikiano wao na NBC Dodoma Marathon tangu mwaka 2023 umewezesha kutoa mafunzo kwa wakunga na wauguzi 200 kutoka hospitali mbalimbali za umma.

Kwa mujibu wake, wataalamu hao sasa wanatoa huduma katika zaidi ya vituo vya afya 150 vilivyopo katika wilaya 31 nchini.

Wadhamini Waendelea Kutoa Msaada

Wakizungumza kwa niaba ya wadhamini, viongozi kutoka Sanlam Allianz Tanzania na GSM Group walisema wameendelea kuunga mkono NBC Dodoma Marathon kutokana na mchango wake mkubwa katika kuokoa maisha na kuleta mabadiliko chanya kupitia michezo.

Usajili Wafunguliwa Rasmi

Usajili wa NBC Dodoma Marathon umefunguliwa rasmi, ambapo washiriki wanaweza kujisajili kupitia NBC Events Portal.

Ada za usajili ni:

  • TZS 45,000 kwa mshiriki mmoja mmoja
  • TZS 42,000 kwa kila mshiriki wa usajili wa kikundi chenye watu 30 au zaidi

NBC Dodoma Marathon inaendelea kuwa zaidi ya tukio la michezo — ni harakati ya kuunganisha jamii, kuhamasisha afya bora na kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, sambamba na wadau wengine wakifanya mbio za majaribio wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za NBC Dodoma Marathon, Tatiana Masimba (pichani) akizungumza kwenye hafla hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema msimu huu wa saba unakuja ukiwa na dhamira mpya ya kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi kupitia nguvu ya michezo.
Wakizungumza kwa niaba ya wadhamini wa mbio hizo, viongozi kutoka Sanlam Allianz Tanzania na GSM Group walisema wameendelea kuunga mkono NBC Dodoma Marathon kutokana na dhamira yake ya kutumia michezo kama jukwaa la kuokoa maisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

No comments:

Post a Comment