Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Thursday, 1 January 2026

NMB YAJIVUNIA USHIRIKI NA UDHAMINI WA MATUKIO YA SHEREHE ZA MAPINDUZI ZANZIBAR

ZANZIBAR — Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya jamii kwa kujivunia ushiriki na udhamini wake katika matukio mbalimbali yanayoambatana na Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ikiwemo Siku ya Kitaifa ya Mazoezi.

Hayo yamebainika baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuitunuku benki hiyo Cheti cha Shukrani na Pongezi kwa kufadhili, kudhamini na kushiriki kikamilifu katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi. Cheti hicho kilitolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kufuatia kukamilika kwa matembezi maalum yaliyoanzia Viwanja vya Mapinduzi Square Michezani hadi Uwanja wa New Amaan, ambapo mazoezi ya viungo ya pamoja yalifanyika.

Katika kufanikisha matembezi na mazoezi hayo yaliyoshirikisha zaidi ya watu 6,000 kutoka vikundi zaidi ya 170 vya mazoezi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, NMB ilikabidhi tracksuit 100 kwa viongozi waandamizi wa SMZ wakiongozwa na Rais Dk. Mwinyi pamoja na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.

Akihutubia washiriki wa mazoezi hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza wadhamini wote kwa mchango wao katika kufanikisha Siku ya Kitaifa ya Mazoezi, akisisitiza kuwa mchango huo una thamani kubwa kwa ustawi wa afya za Wazanzibar. Aliwahimiza wananchi kudumisha utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara.

Nawashukuru wadau na wafadhili wote waliotoa michango yao katika kufanikisha bonanza hili linaloandaliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Mchezo wa Mazoezi Zanzibar (ZABESA). Mazoezi ya viungo ni muhimu kwa afya ya mwili na akili, na husaidia kukinga magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo,” alisema Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwa bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kuwakumbusha wananchi kuwa afya njema ni nyenzo ya msingi ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, huku akisisitiza ushiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kikapu, wavu, riadha na michezo ya majini.